“Wanatugawa kimakundi ili watumeze” Roma Mkatoliki.

“Wanatugawa kimakundi ili watumeze” Roma Mkatoliki.

KKK ni wimbo wake Roma ambao ulifanya vyema zaidi mtaani kuliko katika vituo vingi vya radio. Hii inanifanya niendelee kuamini kauli ya King Moruo ambaye ni moja kati ya mashabiki wakubwa wa muziki wa kizazi kipya. Yeye husema “Radioni hakuna muziki mzuri”

Roma anabaki kuwa msanii wa hiphop ambaye tungo zake nyingi zinaegemea kwenye kugusa mambo yenye ukweli ndani yake, si msanii wa kusifu pombe na ngono kama walivyo wasanii wengi sasa.

Mdau ameonekana ni mwenye kujua ni jinsi gani ya kuwatumia wasanii vyema ili kutimiza malengo yake zaidi kuliko msanii husika. Roma aligundua hili pale ambapo alisema katika wimbo wake wa KKK “Mdau anachenga nyingi kama alichezea Tukuyu”

Lakini pia Roma hakuacha kusema “Wanatugawa kimakundi ili watumeze ona Anaconda” Huu ni wakati ambao lady Jaydee alikuwa akitumia jina hilo katika kuweka ukweli ulipo katika ramani ya muziki wa kizazi kipya.

Fikra za mdau zinaonekana ni kubwa hivyo amejua ni  jinsi gani ya kucheza  na akili za wasanii wengi katika muziki wa kizazi kipya. Na mdau hutumia staili ya kuwagawa wasanii ili aweze kuwatawala zaidi, maana leo hii kama utakuwa umejitambua na kupinga unyonyaji wake basi mdau hutumia nguvu kubwa ya wasanii wengine wakutenge katika mambo mengi.

Hivyo wengi hubaki na malalamiko katika mioyo yao, na wengine husema wakati mpo katika mazungumzo ya kawaida, ila hata acha kukueleza kuwa yaishie hapa hapa. Hii inaonyesha ni jinsi gani mioyo yao imejaa hofu juu ya mdau. Na hofu yao ndio humpa nguvu mdau aendelee kuwatawala siku baada ya siku.

Mdau amejivika mabavu,  na hata kuona baadhi ya wasanii wakidiliki kusema “Bila yeye huwezi” hizi ni kauli za kinyonge na fikra ndogo mno. Lakini ni nani amewaroga wasanii hao ambao wanaamini bila mdau hawezi?

Msanii hawezi bila kipaji chake tu, mimi siamini katika mdau huyu ambaye katika Makala ya Jinamizi nyuma ya mwanazuoni nilipata kumuelezea vyema jinsi anavyomtumia vyema msanii mwenye elimu asiye na ufahamu. Ambaye amegeuka kuwa kibaraka mzuri wa mdau na kuwa dalali wa wasanii wengine katika kupinga uhalisia wa kudai maslahi yao. (Kikao cha wasanii cha kisanii)

Fitna za mdau zitakufunga kama msanii hujaamua kweli kueleza ukweli. Miaka hii sio miaka ya Uhuru na Mzalendo, kama msanii/wasanii wataamua kuweka wazi kila kitu kuhusu mdau hakika wataishi maisha mazuri kupitia kazi zao za muziki. Pia siachi kusema mashabiki mlionao ni wengi kuliko mdau, kwanini hamtumii mtaji wa mashabiki mlionao katika mambo mengi ya msingi?

Ni vyema kuunda umoja wenu wenye maana na malengo ya kukomboa sanaa yenu kutoka mikononi mwa mtu mmoja. Ambaye kupitia jasho lenu yeye amenufaika zaidi.

Amka msanii Muda ndio huu.

Kwa maoni tafadhali tuandikie hapa chini.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube Tizneez