Shabiki amuandikia barua msanii wa hiphop Tz

images

Shabiki amuandikia barua msanii wa hiphop Tz

Mambo vipi Kaka Nash Mc Zuzu… Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri na shughuli zako za kila siku pamoja na mfungo wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kwa kuwa wewe ni muislamu kama sikosei. Kwa Jina la humu facebook naitwa @nyumbani kwanza Stanley, ni mmoja Kati ya mashabiki wako wa dhati kabisa au kwa namna nyingine naweza kusema mimi ni MFUASI wako kwenye masuala ya sanaa na utamaduni wa HIPHOP wa kwa ujumla, yaani ukija kuacha na mimi naacha kusikiliza HIPHOP ya Bongo. Nasema mimi ni mfuasi wako kwa sababu nina kazi zako nyingi sana kama vile TABIA, MITIHANI, NAANDIKA, KAKA SUMA, HASI KUMI NA TANO, PENATI YA MWISHO na zinginezo nyingi, na hata fulana zako ninazo mbili (ile ya kiswahili lugha yangu na ya Nash Mc) ambazo nilimuagiza ndugu yangu Ally Arsenal Podolski na ni kweli aliniletea. Bila Shaka hunijui na hata tukikutana huwezi kudhani kama na mimi ni mmoja Kati ya mashabiki zako wa kweli, ila binafsi nishawahi kukuona kama Mara tatu nne hivi, Mara ya mwisho ilikuwa kwenye “mkesha wa pasaka na wana” pale uwanja wa nyumbani maarufu kama KILINGENI au new msasani club, halafu hakuna siku ambayo niliumia sana kwa kushindwa kuhudhuria tamasha lako la mwaka juzi la NASH MC TEMEKE SHOW kwa sababu nilikuwa naumwa sana. Kwa ufupi niseme tu nakukubali sana japo kwa bahati mbaya nilichelewa kukujua ila nadhani ni kwa sababu miaka ya nyuma nilikuwa naishi nje ya Dar,na nilikokuwa naishi kulikuwa na uwezekano mdogo sana kupata nyimbo zako ila tangu nikujue sijawahi kujutia.
Dhumuni la barua hii Kaka, ni kukupa Hai tu, mwingine anaweza kujiuliza “kwanini asimpigie simu amjulie hali mpaka aandike barua”?,..jibu ni kwamba sina namba yako na ukweli ni kwamba nimejikuta tu kuandika barua kuweka bayana ili na wengine wasome wapate kujua kuwa nina mapenzi ya dhati na aina ya muziki unaofanya wewe kwa kuwa sio dhambi kwangu kufanya hivi.
Kaka, bila shaka unajua kuwa miaka ya hivi karibuni kulikuwa na wimbi la ongezeko la maemcee na marapa kibao kwenye utamaduni wetu wa HIPHOP, ongezeko ambalo lilileta chachu ya mapinduzi makubwa katika sanaa mpaka mashabiki wakaanza kujivunia kiasi cha wengine kuthubutu hata kuandika kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya mistari ya wasanii wao waliokuwa wanawakubali mimi mwenyewe ni mmojawapo, Hili liliashiria ukuaji wa sanaa, ila redio nazo hazikuwa mbali kuanza kugawa matabaka ya wasanii kwa kucheza baadhi tu ya nyimbo zao na aina fulani ya muziki hasa Bongo Fleva. Kitendo hiki kiliwaumiza sana wasanii ndio maana Taratiibu baadhi ya wasanii walianza kubadilika kutoka kwenye kuchana mpaka kuimba ili waweze kupata air time redioni na shoo mbali mbali ikiwemo Fiesta.
Nasikitika sana kumbe utamaduni wetu uliingiliwa na mamluki, ona sasa wanavyosaliti kambi yaani mpaka yule emcee aliekubalika kwa utunzi mzuri wa mashairi na mtindo wake wa kughani Sasa hana jipya na kasaliti kweli daah!! Inasikitisha sana kwa kweli, cha ajabu nae siku hizi anachana kwenye midundo ya ajabu sijui wanaita Trap wenyewe eti ndo mabadiliko hayo na wanameungana na wenzake kufanya hivyo ili kuendana na soko la muziki hakika kinachowatesa ni SOKO NA PESA kama ulivyowahi kuandika.. kwamba wanataka nyimbo zao zipigwe redioni, yaani kwa tafsiri yangu ni kwamba watafanya kile ambacho redio zitataka ili waweze kuendana vizuri na mfumo wa soko, hivi ni kweli kabisa wamesahau redio hizo hizo ndo zinawachagulia mashabiki nyimbo za kusikiliza? Ni Mara ngapi tumekuwa tukisikia redio zikiwa’promote wasanii hata wanaofanya ovyo na kuwaaminisha kuwa ndo vinara wa HIPHOP wakati kumbe ni uongo?.. Binafsi Sina tatizo nao, kwani vipaji ni vyao na wameamua kubadilika kwa manufaa yao wenyewe, ila cha ajabu ni pale wanapogeuka kuwa wakosoaji wa utamaduni halisi wakilazimisha tukubaliane na mabadiliko yao. Mimi nadhani ingekuwa busara wao kukaa kimya tu na waendelee kufanya wanachotaka wao, ila ngoja tuone kama kweli kuna Mafanikio japo mimi binafsi siamini sana, kwani wako wapi akina Z’ANTO, MARLAW, SAM WA UKWELI sijui PNC na wengine wengi si walikuwa wanaimba wale na redio ziliwasapoti sana au? sasa hivi mbona hawasikiki au ndio kusema wamepata Mafanikio wamejikataa?…Bila Shaka kuna kitu hapa.
Kaka,wewe ni mkongwe sana katika utamaduni huu, miaka kumi na tano kwenye hili game si kitoto, kuna waliokuja wakakukuta na ukawafundisha mengi kuhusu utamaduni na wamekuacha bado upo katika ubora ule ule, labda niseme tu kwamba mpasuko huu hauna madhara yoyote kwenye Chama letu kwani sisi mashabiki wako wa dhati bado tuna imani kubwa sana na wewe na tunajua una msimamo sana huwa hauyumbishwi na mfumo unaotawala Sasa, nakumbuka siku moja katika mahojiano yako kwenye redio fulani ulikataa kuchana kisa mdundo mbovu wa kimwanayumba,hivyo ndio inavyotakiwa sio kila ukiambiwa uchane basi unachana tuuuuu hata kama limdundo la kigasho.
Kabla sijahitimisha barua hii, nirudie tu kusema kwamba “sijutii kukufahamu” sio mimi tu bali lundo la mashabiki wanakuunga mkono kwenye sanaa yako, najua sasa upo kwenye matayarisho ya VITASAMOTO EP yaani mimi na mashabiki wenzangu kila kona ya Dunia tunasubiri kwa hamu sana. Endelea kutumia kiswahili fasaha kwenye nyimbo zako ili kila mmoja apate kukuelewa vizuri, mpe hai sana mwanao Sallii Teknik mwambie naikubali sana mikono yake.
Ni mimi mfuasi wako wa dhati,
Nyumbani Kwanza Stanley.

HIZI NDIZO TUZO ZA MTAAA
GAME INAHITAJI UVUMILIVU

NASH MC