PROFFESSOR JAY – NI KWELI SANAA YA BONGO YATAKA MOYO

IMG_3025
Mwaka 2014 bwana Lucas Mkenda maarufu kama “Mr Nice” aliwahi kunukuliwa katika intavyuu moja akisema “niliwahi kumiliki zaidi ya million elfu moja na mia tano (sawa na Bilioni 1.5) kwenye bank tofauti… pesa hizo zilitokana na kufanya shoo nyingi za nje ya nchi kama marekani, uingereza, ujerumani, Sweden, Holland, Dubai, South Africa na kwingineko”.

Wakati ambao Mr Nice alikuwa akimiliki billion 1.5, Dola moja ya marekani ilikuwa sawa na Tsh 950, Nauli ya mwanafunzi ilikuwa Tsh 50, ya mtu mzima Tsh 150 na mkate mmoja ulikuwa Tsh 250. Mchele kilo 1 ilikuwa Tsh 400, Unga kilo 1 ilikuwa Tsh 200, Sukari kilo 1 ilikuwa Tsh 400, Nyama kilo 1 ilikuwa Tsh 3000, maharage (mboga ya taifa) kilo 1 ilikuwa Tsh 200, lita moja ya petrol ilikuwa Tsh 860 na mfuko mmoja wa cement ulikuwa unauzwa Tsh 5,600 (kibiriti, 2015).

Ni wakati ambao Proffesor Jay alikuwa ametoka kutoa wimbo wa YATAKA MOYO akilalamika kwamba wasanii wa mtoni wanakula kuku kwa mrija wakati wasanii wa bongo wakiendelea kufa maskini. Moja kati ya vifo vya wasanii kilichomgusa ni kifo cha anayeitwa “Jabali la Muziki” Hayati Marijani Rajabu.

Ni miaka 19 imepita tangu Marijani Rajabu alipofariki 23/3/1995 na kuzikwa makaburi ya Kisutu, Dar es salaam akiwa na umri wa miaka 40 tu. Hayati Marijani katika uhai wake alitoa vibao maarufu ambavyo havijawahi kuchuja mpaka leo. Ni bar gani Tanzania hii uende halafu usiskie nyimbo kama zuwena, Georgina n.k si utaona bia chungu japo ni chungu kweli.

Kilichompa gadhabu Profesa Jay ni kwamba licha ya Marijani Rajabu kushika chati na kutamba vilivyo lakini Marijani Rajabu amekufa na dhiki kwa sababu sanaa ya Bongo hailipi. “Inasemekana kuwa kufikia mwaka 1992, hali ya maisha ya Marijani Rajabu ilkuwa ngumu kupita kiasi. Alifikia kuendesha maisha yake kwa kuuza kanda za nyimbo zake. Alijenga kibanda nje ya nyumba yao maeneo ya kariakoo, jijini Dar es salaam. Pamoja na kuimba nyimbo nyingi za kukisifu chama cha mapinduzi” (Kiyungi, 2014).

Wakati Profesa Jay akigadhibika na sanaa ya bongo kuwa hailipi kipindi hicho hata ukiwa muigizaji kama Bishanga Bashaija ambacho ungeweza kufaidika umaarufu na kupata nafasi ya kuwa Mc kwenye harusi, kipaimara, send off, kitchen part, komunio, ubatizo n.k Ni wakati huo huo pia Mr nice “..aliwahi kusema kwamba alikuwa anaingiza Milioni 40 kwa wiki” lakini kwa sasa ameporomoka vibaya kiuchumi.

Natumai Profesa Jay haakukosea kusema wasanii “kiasi wanachokipata kinaishia kwenye bia na ngono” Kwa maana Mr nice “..alikuwa anaingiza pesa na….. alijua kuzitumia… msafara mkubwa alikuwa akiambatana nao katika harakati zake za kula maisha. Ungeweza kumkuta Club Ambiance.. amezungukwa na idadi kubwa ya wapambe… hali kama hiyo ungemkuta nayo pia kwa macheni… Club Billicanas, Maisha Club na sehemu nyinginezo. Wapambe… hawakuwahi kupungukiwa… vinywaji au chakula, achilia mbali wale wasio na aibu walioambatana na mademu za… bili zao zote zililipwa bila matatizo” (GPL, 2014)

Profesa Jay anatuambia kwamba “Umoja wa wasanii wa Bongo hiyo ndiyo njia” ya kuepuka changamoto zote zinazoikumba tasnia ya sanaa. Hili litakuwa ajabu lingine la tisa, hebu tazama; wakati Nash Mc akitangaza nyimbo zake zisipigwe na baadhi ya radio, Mapacha walikuwa kwenye moja ya redio iliyopingwa na nash mc wakisuluhisha mgogoro wao na baadaye ikatafsiriwa na mashabiki kama kuomba msamaha.

Wakati wasanii wakiwakataa mameneja wa kibongo, PNC anampigia magoti meneja wake ili asamehewe. Wasanii mnataka umoja wakati Vinega na harakati ya Antivirus walipokuwa wakipambana na mfumo wa kinyonyaji wa sanaa ya Tanzania wengine wamekaa kwenye mitandao ya kijamii na vijiweni wakibeza “Oooh wale jamaa wana pointi ya msingi lakini wanatukana sana”. Mnataka umoja wakati huo huo msanii wa Hip Hop hawezi kukaa meza moja na msanii wa Bongo Fleva au Bongo Muvi.

Katika karne ya hii ya utumishi wa tumbo, Tanzania ni nchi ambayo baadhi ya wasanii hasa wenye ushawishi kwenye jamii akili zao zipo tumboni kuliko kichwani. Msanii kama huyo umuelezee habari za kupambana na mfumo ambao unamfanya ashibe hamuwezi kuelewana. Lakini pia Umoja wa wasanii wa bongo umeshindikana kutokana na wasanii kutokuwa na uelewa wa changamoto zinazokumba kwa pamoja licha ya tofauti ya sanaa wanazofanya.

Nasikitika kusema UMOJA ni msamiati ambao umekosekana kwenye kamusi ya sanaa Tanzania na kama umo basi utakuwa haujapewa maana. Katika hali kama hii ukiwa mpigania maendeleo ya sanaa Tanzania yapasa kuwa na moyo kweli kweli.

Ni wakati ambao profesa jay anasema ndio watakao kuacha kukujumuisha kwenye shoo na kuwaleta wasanii wa nje. Wasanii hawa wa nje wengine hata hawafikii vigezo vya kuperfom Tanzania. Chukua mfano wa msanii kama huyu aliyepafom kwenye Bongo star search (2015) anayeitwa RUN TOWN kwa kweli alishindwa hata ku-run ukumbi mdogo tu na hapo akipewa tafu ya playback yake najiuliza kimombo “how can he run town?’.

Alikuja Lil Kim shoo ikamshinda ikabidi amuite Juma Nature ampe tafu. Unabaki kujiuliza hivi kwanini msiwape pesa nyingi wasanii wa kibongo wakafanya shoo nzuri tu ambazo mashabiki wanazielewa kuliko kuleta wasanii ambao wanashindwa kukidhi hitaji la burudani kwa mashabiki.

Professor jay juzi juzi amechaguliwa kuwa mbunge jimbo la mikumi. Nitumie waraka huu kumpongeza kwa kuchaguliwa maana ulishakataa kwamba hapa Jasho la mtu haliliwi wala mtu haibiwi. Jasho lako ulilolitoa kwenye muziki ndilo limekupa nafasi kubwa ya kuwa mbunge wa mikumi. Utakua huna shukrani usiposema muziki umekusaidia kwenye kampeni zako kwa kiasi kikubwa.

Najua kwa sasa hutofanya muziki kama ulivyokuwa ukifanya ukiwa sio mbunge na nategemea huwezi kutoa nyimbo zaidi ya mbili katika kipindi chako cha ubunge (2015 – 2020). Wasanii na mashabiki mkumbuke kwamba professa jay sio mbunge wa wasanii (kama aliyosema sugu) profesa ni mbunge wa mikumi anawakilisha wananchi wa kawaida. Hivyo baada ya miaka mitano msije kumuuliza mbona haki zetu wasanii hukutetea.

Namaliza kwa kusema HONGERA SANA Profesa Jay, bora ukawe mbunge tu, maana sanaa yetu ya Tanzania wakati Msanii mmoja anapambana na mnyonyaji wakati huo huo Msanii mwingine anapita pembeni kumuomba msamaha mnyonyaji Yule Yule…. Ni kweli kuendelea kufanya sanaa ya bongo YATAKA MOYO…

Imeandikwa na
MALLE HANZI
0715076444
©2015