Diamond Platnumz tupe talaka tatu

Diamond Platnumz tupe talaka tatu
Diamond yupo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. .Anawatazama Watanzania na wanamuziki wenzake kwenye viunga vya mji wa Moshi. Game la muziki liko chini ya soksi zake. Analiendesha. Analiamrisha na linamtii. Anajituma.
Ana pesa. Ana mwanamke mzuri kwa maana ya uzuri. Ni maarufu na anapendwa. Unaweza kuwa maarufu lakini hupendwi. Hata Hitler alikuwa maarufu. Hata shetani ni maarufu lakini hapendwi. Na unaweza kuwa na pesa na usiwe maarufu. Kuna matajiri wangapi Bongo wakipita Kariakoo hakuna anayewatazama? Na unaweza kuwa na kila kitu maishani lakini usifanikiwe kuwa na mwanamke mzuri. Zari kakupa watoto wawili. Mheshimu.
Hakuna uchawi kama kujituma na kujitambua. Utafanikiwa tu. Diamond anavyo vyote hivyo.
Moja kati ya akili mbovu tuliyonayo waswahili ni kutopenda mtu awe juu kila siku. Tunataka kuona mtu anapanda na kushuka. Furaha ya Waswahili ni kuzalisha Mr Nice mwingine. Tunakerwa na kuona Diamond anaendelea kupaa kila siku. Hatupendi mtu mmoja kuwa juu kila siku. Hata kama huyo mtu anajituma na kupambana. Tunapenda na kufurahia kuona mtu anapaa juu na kushuka chini ghafla.
Hasira za kutopenda hilo tunalihamishia katika kutafuta mtu wa kumfunika Diamond.
Wabongo wamelazimisha upinzani wa Kiba na Diamond. Wamelazimisha hata wimbo wa Darassa kuwa ni dongo kwa Diamond.
Hakuna lolote zaidi ya kuona anapatikana mtu wa kuwa juu ya Diamond.
Wabongo baadhi siyo wote, wanakerwa na umaarufu wa Diamond. Mafanikio ya Diamond. Na hata uwepo wake duniani. Kuna watu wanaongea vibaya kuhusu yeye mpaka mtu unalazimika kuamini kuwa hawapendi hata yeye kuendelea kuwa hai.
Sasa watu wenye mioyo hiyo ya kipuuzi wanatulazimisha tuamini kuwa Diamond hana mashairi mazuri kama zamani wakati anaanza muziki. Wanatulazimisha tuamini kuwa hana sauti nzuri wala uwezo wa kuimba.
Wanasahau kuwa walimpenda mwanamuziki aliyeimba Parakatatumba. Bila kuelewa lugha yake wala ubora wa sauti yake. Makhirikhiri walibamba Bongo bila kuelewa lugha walizotumia. Ila Wabongo wanataka kuona Diamond anaimba kama nyimbo zake za Mbagala au Nitarejea.
Wanajisahaulisha kuwa watu wanataka fleva tu. Sauti? Davido hafikii hata robo ya sauti ya Barnaba. Lakini nani mwenye mafanikio na umaarufu kati yao? Daraja la Diamond hivi sasa siyo la kuimba shida za Mwananyamala au Matombo. Ni midundo mizuri na mtiririko mtamu wa maneno ili hata asieelewa lugha basi afurahie midundo na melody. Mwacheni dogo apige pesa. Mwacheni dogo awakilishe taifa. Mwacheni dogo afurahie kujituma kwake. Mwacheni dogo atimize dua za mama yake juu yake. Ni dogo flani hivi asiye na elimu kubwa wala kukulia katika maisha bora. Anachofanya na kuingiza pesa hajarithi kwa baba kama Mohamed Enterprises.
Ni dogo flani aliyekuwa na ndoto za kuingia kwa pesa yake kwenye shoo za Fiesta, achilia mbali kuimba kwenye Jukwaa la Fiesta. Leo anatumbuiza kwenye jukwaa kubwa Nigeria na Gabon. Leo ananunua nyumba South Africa badala ya ndoto yake ya kupanga Sinza chumba kimoja. Furahia mafanikio yake badala ya kuchukia.
Mnachukia Mrisho Ngassa kutopita njia alizopita Mbwana Samatta. Lakini mnapinga Kiba kupita alikopita Diamond. Eti imani yenu ni kuwa Kiba anatakiwa kuigwa na Diamond. Acheni kulazimisha mtu aende kucheza mpira kwa kujifurahisha na washikaji Bonde la Msimbazi badala ya kupiga stori kwenye simu na NE-YO.
DIAMOND ulitupa talaka mbili ambazo ni talaka rejea. Usisikilize na kujibishana na washikaji wa Manzese, Mwanjelwa, Ngarenaro, Makoroboi, Chumbageni, Kibororoni wala Kihonda. Piga pesa dogo. Zile talaka mbili ni talaka rejea.
Wapige TALAKA TATU WABONGO.
Mungu akubariki.
Follow Twitter Tizneez
Facebook page Tizneez
Instagram Tizneez
Tuachie maoni yako hapa

By Dk Levy