BONTA NA MZIMU WA NIKKI MBISHI

bonta


BONTA NA MZIMU WA NIKKI MBISHI

Sehemu ya Kwanza.
_____________________

Nyakati ambazo mtangazaji wa maarufu aitwaye Fred Fidelis (Fredwaa) alikuwa akitangaza kipindi cha asubuhi (sikikumbuki jina) ila kilikuwa kina segmenti inaitwa ‘Sindano Tano za Moto’, ni nyakati ambazo mtangazaji mwingine ndugu Sandhu G maarufu kama ‘Kid Bway’ ilikuwa ikimlazimu kusubiri masaa manne baadaye ili aingie kwenye kipindi cha mchana (na chenyewe sikikumbuki jina) katika redio hiyo hiyo. Kwa mpenzi wa muziki wa vijana ilikubidi usubiri kwa masaa mawili mengine baada ya Kid bway kumaliza kutangaza ndipo uwasikilize Dee Seven na Dj (sijui maliz/marlis/mars???) kwenye redio dada na ile.

Enewei, hapo nazungumzia Radio Free Africa na Kiss Fm kuanzia robo ya pili ya miaka ya 2000 kuelekea mwishoni. Nimezizungumzia redio hizo kwa sababu mtu nayemzungumzia katika makala haya kwa mara ya kwanza nilianza kumsikia katika redio mojawapo kati hizo na bila shaka itakuwa RFA. Ni mwendawazimu pekee ndiye anaweza kusema “hupaswi kumzungumzia jamaa, mtu mwenyewe umemfahamia kwenye redio tu…”. Sawa na nyie mnapowazungumzia kina 2pac na Biggie mlikuwa mnaishi nao uswahilini au?

Msanii nayemzungumzia ni bwana Godfrey Nyahongo a.k.a Bonta. Kwa mara ya kwanza kabisa namsikia Bonta ni katika kibao cha kiitwacho ‘Macho Yangu’ kilichotayarishwa na prodyuza Q The Don. Kuhusu a.k.a ya The Don Hivi unakumbuka nyakati flani hivi Fid Q akawa anajiita the don na Mwana FA nae akawa anajiita the don na Baadaye tena Fid Q akajiita ‘Jeshi la mtu mmoja’ na Mwana FA akajiita ‘One Man Army’. Enewei kufanana majina/mawazo kunatokeaga tu, tuyaache hayo hayahusiani na mada nilikuwa nachangamsha genge tu.

Bonta alishawahi kusema tusisubiri mpaka afe ndipo tumpe sifa zake, mimi ngoja nimsifie leo akiwa hai. Kibao cha ‘macho yangu’ kilikuwa kibao kikali na ndicho kilichonifanya nianza kumfuatilia Bonta kwa ukaribu. “Jasti imajini” mtu anakwambia anaamka asubuhi anaona jua linazama huyo mtu atakuwa hana macho ya kawaida yakupasa kutumia jicho la tatu kugundua kaona nini. Mimi ni mpenzi mkubwa wa hiki kibao hata bonta mwenyewe anajua hilo.

Wakati kibao hiko (macho yangu) kinatoka ni nyakati ambazo Prodyuza Q The Don wa MO Records (enzi hizo) alikuwa ameanza kufanya vizuri katika utayarishaji wa vibao. Kwa nyakati zile ilikuwa wasanii wanatoka Mwanza kwenda Dar es salaam kurekodi sasa wasanii wakawa wanatoka Dar es salaam kuja Mwanza kurekodi. Unazikumbuka nyimbo kama Mchizi wangu na Bang remix za N2N, Sauti ya G nako, Muda na Dakika Tisini za Joh Makini, Tusonge ya Jay mo na Chid Benz na nyinginezo nyingi.

Ni katika kipindi hicho ambacho unamsikia Bonta, unamsikia pia na mwanakikundi mwenzie waliye mstari wa mbele (Front line) kuanzia River Camp Soldiers na sasa Weusi bwana Joh Makini akiwa katika ubora wake; ubora ambao sidhani kama atakuja kuufikia tena. Joh alikuwa hatari bwana; yaani kama ulimsikiliza Joh wa Hao, Muda, Ufalme, zamu yangu n.k alafu ulazimike tena kumsikilza Joh wa Don’t bother, bei ya mkaa, nusu nusu n.k lazima ukatike stimu kiaina haijulishi umezilipia au umezikopa.

Hebu fikiria; litokee jibaba la miraba saba liseme “Dar nyumbani sasa anitishe nani?” watu wote waogope alafu atokee bwana mdogo mwili wake wenyewe Malle na robo hivi alafu ajibu “nawapigia nyumbani, nawapigia ugenini?”. Lile jibaba miraba saba liseme tena “mimi ndio imoto tekniki wa bongo” alafu yule bwana mdogo aseme “uwezo wao upo chini zaidi ya soksi zangu”. Sio hatari hiyo?

Bonta ameanza kujihusisha na muziki wa Hip Hop tangu mwaka 1997 akipishana miaka miwili na swahiba wake Joh makini ambaye ameanza mwaka 1995. Bonta ameshawahi kutoa santuri (album) moja tu inayokwenda kwa jina “Kila Kitu Nyerere” iliyotoka mwanzoni mwa miaka ya 2010 na kuzinduliwa mkoani Morogoro. Nyimbo ambazo amewahi kuachia hewani ukiondoa macho yangu ni kama Mganga wa Mtoni, mti wenye matunda, Nauza kura yangu, Hip Hop baby, Kila kitu Nyerere, Matusi, Walaumiwa, B3 n.k. Wimbo wake wa mwisho kuutoa ni Mapenzi Matamu uliotoka miezi michache iliyopita.

Bonta ni msanii ambaye anaungana kimtazamo na Afande sele kuhusu suala la mapenzi katika muziki ingawa wanatofautiana sababu za misimamo yao. Kwa mfano; Bonta mpaka sasa amegoma kutoa wimbo wenye maudhui ya kimapenzi kutokana na kuamini kuwa Mapenzi hayatakiwi kuoneshwa/kufanywa hadharani, mapenzi ni mambo ya chumbani wakati Afande sele yeye hawezi kuimba nyimbo za kusifu Ngono na Pombe katika nchi maskini ya pili kutoka chini.

Kwa miaka mingi ambayo nimekuwa nikimskiza Bonta amekuwa ni msanii ambaye akijitanabaisha katika nyimbo kwa kuelezea mambo ya kijamii na kisiasa zaidi. Nyimbo kama bwana Malaria, Nauza kura yangu, Kila kitu Nyerere nk ni nyimbo zinazotoa elimu kwa jamii kuhusiana na mambo ya afya na uraia. Katika nyanja hiyo Bonta kafaulu sana inawezekana pia na usomi wake wa udaktari unachangia kumpa uwezo mkubwa wa kupambanua mambo.

Naweza kutumia maneno mengi kuelezea sifa za Bonta lakini leo itoshe tu kwa hizo nilizozitaja hapo juu. Sijui kilitokea kipi? na sijui chanzo kilikuwa ni nini? Ndani ya Mwezi March, 2012 sanaa ya Bonta ilikumbwa na dhoruba pengine hata Nahodha mwenyewe alikuwa hajajiandaa kukutana nayo.

Itaendelea……….

Imeandikwa na
Malle Hanzi
O715076444
©2015