BONTA NA MZIMU WA NIKKI MBISHI (sehemu ya II)

Bonta+ 6
Sehemu ya Pili
_____________________
Ilipoishia…..
Naweza kutumia maneno mengi kuelezea sifa za Bonta lakini leo itoshe tu kwa hizo nilizozitaja hapo juu. Sijui kilitokea kipi? na sijui chanzo kilikuwa ni nini? Kwani ndani ya Mwezi March, 2012 sanaa ya Bonta ilikumbwa na dhoruba pengine hata Nahodha mwenyewe alikuwa hajajiandaa kukutana nayo.
Endelea……….
Nasema Bonta alikumbwa na dhoruba mwezi huo kwa sababu; ndani ya mwezi huo nakumbuka tulikuwa na Nash mc na watu wengine katika eneo la shule ya msingi Madenge, tukirekodi kipindi cha Hip Hop. Tukiwa katikati ya zoezi ndipo Nash Mc akapokea simu kutoka kwa mtu ambaye wakati Nash mc akiendelea kuzungumza nae kwenye simu ni kama alikuwa akilalamika na Nash Mc akijaribu kumtuliza kwa ushauri wa hapa na pale huku jina la nikki likitajwa tajwa mara nyingi. Baadaye Nash alikuja kunieleza alikuwa anaongea na Bonta akilalamika baada ya Nikki kumchana redio kwamba “Bonta ni whack”.
Ilikuwa ni Jumamosi katika Kipindi cha Bongo Fleva cha Dj Fetty ambapo Nikki Mbishi aliamua kufunguka hayo. Hushangai au hujiulizi inakuaje mambo ya Hip Hop yanajadiliwa kwenye kipindi cha Bongo Fleva. Enewei Nikki alifunguka wakati ambao hakuna aliyetaraji ingawa hapo kabla katika kibao chake kiitwacho “Undisputed” alikuwa amemchana kwamba “ukitaja conscious please usimuweke Bonta” lakini haikuchuliwa “siriazi” kiasi hicho wengi wetu tuliamini ni changamoto za kisanaa tu kupitia mistari.
Ufafanuzi kuhusu kauli yake Nikki Mbishi alishawahi kunukuliwa akisema “Ninaposema Bonta hayupo conscious namaanisha kuwa naheshimu anachofanya, ana ujumbe wa maana lakini uwasilishaji wa ujumbe wake kwa umma ndio tatizo. Kwa neno moja naweza kusema Bonta ni MC mbovu,na ninaposema hivyo namaanisha kuwa hajui kurap, anachofanya nikuongea na wakati mwingine anapata beat nzuri za kuongelea. Nadhani huu ni muda wa kuwaambia ukweli” (Bundala, 2012)
Unaweza kuona Nikki Mbishi alikuwa anamkubali bonta kama msanii mwenye mawazo na mashairi makali lakini hapendi namna alivyokuwa akichana. Hii ni changamoto ambayo Bonta hakuikubali na sidhani kama ameshawahi kuikubali. Na hapo ndipo ulipokuwa mwanzo na muendelezo wa Nikki Mbishi kutupa mistari ya kumdiss bonta. Naweza kusema pia ndio mwanzo wa Mzimu wa Nikki Mbishi kuanza kutokea katika mistari ya bonta.
Toka mwezi wa tatu mwaka 2012 mpaka leo Disemba 2015 sasa ni miaka mitatu na miezi tisa imepita. Bonta ametoa nyimbo sio chini ya tano ambazo ninazifahamu. Nyimbo hizo ni Tukutane maktaba, Mitaani watu Buu, Walaumiwa, Mauwongo na Mapenzi Matamu uliotoka juzi juzi. Bonta kwa muda wote anaonesha amekuwa akisumbuliwa na mzimu wa diss za Nikki mbishi ambazo ni nyingi. Kiukweli Nikki Mbishi amemdiss Bonta kwenye nyimbo nyingi pengine kuliko msanii yeyote wa Bongo.
Katika hizo nyimbo tano ambazo Bonta ametoa ni nyimbo mbili tu ambazo ameukwepa mzimu wa Nikki Mbishi. Nyimbo hizo ni Walaumiwa na Mauwongo. Ingawa mara zote Bonta amekuwa akikwepa kulitaja jina la Nikki Mbishi moja kwa moja lakini amekuwa amekuwa akimtaja kwa kificho kwa kumfumba kwenye mistari ingawa alishawahi kumwambia ”
Ongea tu ongea tu dogo mafumbo woga, sikio halipimi neno kama ulimi uonjavyo mboga”.
Nyimbo nyingine tatu ambazo ni Tukutane maktaba, Watu buu na Mapenzi zote zimekumbwa na mzimu wa Nikki Mbishi kama ambavyo nitazifafanua kwenye aya zinazofuata chini.
Baada ya Nikki Mbishi kumdiss Bonta; wimbo wa Bonta uliofuata ulikuwa unaitwa “Tukutane Maktaba” ambao watu wengi walitegemea angemjibu Nikki lakini alichokifanya ni kukwepa kumtaja na kumzungumzia kiufundi. Bonta alimtazama Nikki kama mtu “aliyekomaa tu sura ila hajakomaa akili”. Hata idea ya “Tukutane Maktaba” ni kudhihirisha kwamba Nikki Mbishi akili yake haikuwa imekomaa kukosoa sanaa ya Bonta hivyo wakutane maktaba ili amsome amuelewe kama Booth ameshindwa kunielewa. Wimbo huo wa Bonta ulikuja kujibiwa na Nikki kwamba “Fake Mc Bonta, Nikki is off Campus”.
Bonta alikwepa kujibizana na Nikki kwa kwa kuamini kwamba yeye hayuko levo moja na Nikki. Bonta anaamini Nikki alitakiwa “kumchapa Shah Bang” kwanza kisha amchape Nikki wa Pili ndipo akutane nae. Nikiskiaga huo mstari huo swali la kipumbavu huwa linanijia “ina maana pale kambi ya mtoni Shah Bang ndio wakujifunzia kubato? Ina maana ndio kibonde wao” Hapo alimshusha vyeo sana mshikaji wake.
Katika wimbo huo wa “tukutane maktaba” Bonta aliapa kwamba Nikki akitaka kumtukana atamchagulia tusi na akizidisha chokokocho atamvungia lakini hakuweza kuustahimili mzimu wa Nikki Mbishi ulioendelea kumtokea. Katika kibao “mtaani watu buu” aliendelea kumchana kwa kificho hasa katika ubeti wa kwanza. Bonta alitumia msemo wa kiswahili kwamba “kiporo hakihitaji moto mwingi” kwahiyo hahitaji nguvu kupambana na mbishi.
Bonta alienda mbali zaidi ya muziki na sijui alikuwa anataja maisha gani ya nikki aliposema “Anajifanya mwanahip maisha yake hayana hope”. Bonta anaamini anakubalika hata Nikki akisema yeye sio Conscious mtaani watu watapiga buuu (watamzomea) na ndio kisa cha kuhojiwa na kumwambia Nikki kuwa “at the end of the day unajua mashabiki wako ndio mashabiki wangu, mashabiki wangu wataendelea kuwa mashabiki wangu na mashabiki wako wachache watakuja kwangu” (Chiwile, 2012).
Katika kipindi “Mtaani watu buu” imetoka ni kipindi hicho hicho pia Nikki Mbishi alikuwa ameingia kwenye kile kilichoitwa bifu na wasanii wengine wawili ambao ni Ney wa Mitego na Kimbunga. Nikki alikuwa ametoa wimbo wa kumdiss Ney ulioitwa Ney wa mitego na Kimbunga alikuwa ametoa wimbo wa kumdiss Nikki ulioitwa Nikki Mbichi. Kwa hewani kuliko na nyimbo tatu za wachanaji wakidisiana na zote zikipewa airtime si unajua habari mbaya ndio nzuri kwenye vyombo vya habari.
Nash mc alishawahi kuzizungumzia nyimbo hizo kwa kusema “Nimesikia Nikki Mbichi ya Kimbunga, nimesikia Nay wa Mitego ya Nikki Mbishi, sasa hivi Bonta ana wimbo unaitwa Mtaani Watu Boo, ambayo ni ngoma inayoelekea kwa Nikki Mbishi moja kwa moja….. watu wanalalamika kuwa imekuwa kama mipasho, kwanza kabisa hazijakaa kama inavyotakiwa kwenye hip hop zikae hizo nyimbo ambazo watu wanatoleana kwa ajili ya kusemana ama kutusiana…. Nikitazama kabisa naona bado zina mapungufu, bado nyimbo zenyewe zina mashaka” (Times, 2013)
Wimbo wa “Mapenzi Matamu” ambao umetoka 2015, Bonta ametupa tena kijembe kwa Nikki pale anaposema kwa kujiuliza “Weusi watu wa Media hawapendwi?” alafu anajijibu mwenyewe “Hupendi wewe baba”. Katika jibu la Bonta ametumia Nafsi ya pili umoja. Kwanini atumie umoja kama kuna watu wengi wanaowachukia weusi. Bonta anajua kuna wengi wanaowachukia weusi hawaathiri sanaa yao kama ambavyo mbishi anaweza kuathiri. Kwa hiyo hakuona umuhimu wa kuwaattack watu wasio na madhara ndio maana akatumia umoja. Hakuna asiyejua kwamba Nikki ndio adui namba moja wa sanaa ya Bonta.
Miaka mitatu na ushee ya mgogoro wa kisanaa kati ya Nikki Mbishi na Bonta tumeshuhudia baadhi ya mashabiki wa Nikki Mbishi wakimchukulia Bonta kama Mc mbovu na baadhi yao wakiona Nikki Mbishi anazingua tu na wanaobaki hawajui washike lipi waache lipi.
Kwa mtazamo wangu mimi na napenda uheshimiwe kama mtazamo wangu na sio vinginevyo. Bonta kabla hajakosolewa na Nikki alikuwa ni bora zaidi ya huyu Bonta nayemsikia kwa sasa. Inawezekana changamoto ambayo ameipata kutoka kwa Nikki imemfanya apoteze umahiri katika sanaa kwa kiasi fulani ndio maana nasema mzimu wa diss za Nikki mbishi bado unamuandama Bonta.
Ukiondoa wimbo wa “Mapenzi matamu” nyimbo zingine nne alizozitoa baada ya diss ya Nikki haziko katika viwango vile vya Bonta wa Macho yangu, kila kitu nyerere, nauza kura yangu etc. Walaumiwa na Mauwongo zina maudhui mazuri lakini hakuna kemia kati ya mchanaji na midundo na hii imesababishwa na uwasilishaji pamoja na uchaguzi mbovu wa midundo. Naanza kuamini pengine ni Nas Escobar pekee ndiyo mwenye uwezo wa kuchagua mdundo mbovu na kutengeneza ngoma kali.
Sauti ya Ghetto ya Profesa Jay Ishawahi kusema itafikia wakati maadui wako wataulizana eti.. “unaimba au unachana”. Sitaki kuamini kwamba ndivyo nikki mbishi anajiuliza lakini karibu katika nyimbo zote Bonta alizozitoa michano yake mingi inategemea uitikiwaji ili kukamilisha beti zake. Kwa mfano: mistari hii hapa chini ya wimbo wa mauwongo :-
Maji safi…. mauwongo
Maisha bora, mauwongo
Kwenye jimbo, mauwongo
Kwenye kata, mauwongo
Kwenye mtaa, mauwongo
Kitongoji, mauwongo
Nyumba kumi, mauwongo
Nyumba moja, mauwongo
Huo ni mfano tu lakini amekuwa akifanya katika nyimbo mbalimbali hata hii ya hivi karibuni kafanya hivyo. Kwa hiyo; kutegemea uitikiwaji alafu ukichanganya na midundo sampuli ya mauwongo ile ladha ya michano inakuwa inapungua.
Bonta amefikia wakati sasa kabla hajatoa wimbo anatengeneza sijui “skendo” sijui “kiki” ili kuipa promo ngoma yake. Juzi juzi hapa kabla ya kutoa wimbo wake wa “Mapenzi Matamu” alitangaza kuachana Hip Hop na kuhamia kwenye Bongo fleva na kuthibitisha hilo alisema anatoa wimbo wa kuimba uitwao “Mapenzi Matamu”. Lakini haikuwa kweli bali ilikuwa ni kuipa nguvu ngoma yake. Najiuliza je ni kweli Bonta kafikia huku? Kujidhalilisha/kujishushia heshima kwa kutafuta kiki na kuwafanya mashabiki wake wamtolee matusi ya nguoni; ndugu George Kyomushula ni mhanga wa hilo.
Amini nakuambia kuna mashabiki wengine wanaamini kwa sasa unafanya Bongo fleva na wala hawakujisumbua kupakua wimbo wako. Naamini pia utakuwa unaukumbuka ujumbe mfupi niliokuinbox uliposema unaacha Hip Hop, Unahamia Bongo Fleva. Nilikuambia kwamba “..kama unafanya hivi for promo…. then u have choosen a wrong technique..” na wewe ukanijibu niweke “akiba ya maneno”. Nisamehe kama ntakuwa nakosea ila hii ndio akiba ya maneno niliyoiweka.
Nihitimishe kwa kukukumbusha meseji yangu ya Tarehe 01/04/2012 siku chache baada ya mgogoro na Nikki kuanza “..Kuna namna nzuri za kuonyeshana, kufundishana, kukosoana na kuelimishana… Mi siko upande wowote..” tafadhali pigia mstari kwenye sentensi ya mwisho ya nukuu ya meseji hiyo. Natumai ipo siku ntamsikia tena Bonta wa macho yangu. Kama nitakuwa siko sahihi, kaka Bonta atanisamehe kwa uwezo mdogo wa kufikiri. Bai ze wei Mwandishi huwa hauwawi.
Mwisho.
Imeandikwa na
Malle Hanzi
O715076444
©2015