Basata yamfungulia Nay wa Mitego, yamweka kwenye uangalizi

IMG_2581

BASATA YAMFUNGULIA NAY WA MITEGO, YAMWEKA KWENYE UANGALIZI

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungulia Msanii wa muziki wa kizazi kipya

Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego kuendelea na shughuli za Sanaa

baada ya kuwa ametekeleza adhabu (maagizo) zote alizopewa kama masharti ya

kumfungulia.

Aidha, BASATA kama mlezi wa wasanii linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe (Nay wa

Mitego) kujutia na kukiri kwamba amejifunza na yuko tayari kubadilika na kwamba

hatarudia makosa aliyoyafanya

Hata hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na shughuli za Sanaa Baraza linamweka

kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama sehemu ya kuhakikisha anaendesha

shughuli za Sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu sambamba na kuzingatia

maadili katika kazi zake.

Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 27/07/2016 Baraza lilimfungia Msanii Nay wa

Mitego kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo:

1. Kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa

2. Kulipa faini ya shilingi milioni moja (1,000,000/-)

3. Kuomba radhi watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye

akaunti zake za mitandao ya kijamii

4. Kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’ ili ubebe maudhui yenye maadili

Msanii Nay wa Mitego ametekeleza adhabu zote tajwa hapo juu. Leo hii tunamkabidhi

rasmi cheti chake cha usajili na kibali cha BASATA.

Hata hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’ Baraza

bado halijaridhishwa na marekebisho hayo hivyo linaendelea kuufungia wimbo huu hadi

hapo litakapojiridhisha umekidhi vigezo vya kimaadili.

Katika kikao na Msanii Nay wa Mitego cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa adhabu

yake kilichofanyika tarehe 12/08/2016 Ofisi za BASATA ameagizwa kuendelea kuufanyia

marekebisho wimbo wake huo kama bado anaona anauhitaji.

Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla kuacha

kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo. Hatua na adhabu za

kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha habari kitakachokiuka agizo hili.

Aidha, katika kikao hicho cha tathimini ilibainika kwamba Msanii Nay wa Mitego kwa

taarifa potofu alizopewa alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo Kasi la tarehe

30/07/2016 akiwa katika adhabu. Kwa kosa hili ameandika barua ya kuomba radhi na

Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa waandaaji wa tamasha hili.

Baraza linatoa wito kwa wasanii kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za

uendeshaji shughuli za Sanaa sambamba na kuhakikisha wanazingatia maadili katika

kila kazi wanazobuni ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao

kwa kiasi kikubwa sana.

SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI