Wimbo wa Joh Makini “Ufalme” ni jibu tosha kwa Chid Benz.

joh-makini

Wimbo wa Joh Makini “Ufalme” ni jibu tosha kwa Chid Benz.

Ni alhamis ya tarehe 21/7/2016 msanii Chid Benz alikuwa akifanya mahojiano katika kituo cha radio Uhuru FM kilichopo Jijini Dar es Salaam, ambapo kwasasa amekuwa akizunguka katika vituo vingi vya radio katika kutambulisha wimbo wake mpya aliyomshirikisha Ray Mond.

Katika mahojiano hayo alizungumza mengi ila moja lililostua wengi ni lile swala la kusema kuwa “Nay wa Mitego na Joh Makini ni wasanii wa kutengenezwa.Na baadae swala hilo kuchukua nafasi katika mitandao ya kijamii hususani “Instragram” na kila mtu akawa na maono yake kwenye hili jambo.

Ukitazama katika mawazo mapana huwezi kushangaa kutaja jina la Nay ila imeshangaza kumtaja Joh Makini. Chid Benz na Nay wa Mitego wamekuwa katika vita ya maneno kwa muda mrefu, lakini pia Nay wa Mitego muziki wake ni muziki wa maneno mengi ya kugusa watu katika mlengo wa kukosoa.

Chuki kati ya Nay Wa Mitego na Chid Benz ilizidi baada ya Nay kumuimba Chid wakati ametoboa pua “Chid Benz katoboa sijui ana maanisha nini” Jambo hilo halikumfurahisha Chid Benz ambaye baadae alimjibu Nay katika wimbo wake wa Nimerudi aliyomshirikisha Dully Sykes “Yule neema anasema nimetoboa pua yule mtoto mshamba mtoto anazingua yule mtoto mastar anatujua yule mtoto anataka mua”

Kwa upande wa Joh Makini si msanii wa kusema hovyo juu ya wasanii wenzake. Isipokuwa kusema kile ambacho kimempeleka katika mahojiano, ila pia ni msanii aliyesimamia muziki wake zaidi na ndio sababu ya kupanda kisanii kila siku inapoitwa siku.

Niliwahi kuandika makala moja ambayo ilikuwa na kichwa cha habari kinachosema “Kurudi ghafla na kupotea ghafla kwa Chid Benz” ndani yake nilihoji Tukitoa swala la matumizi ya madawa ya kulevya.Je! Mashabiki na wadau wanajua kitu kilichompoteza Chid Benz kwenye muziki hapo awali?

Kusimama kwenye ukweli ni jambo jema na la kumpendeza mungu. Huwezi kupinga kipaji cha Chid Benz ila neno lenye herufi chache ndilo lililomuangusha kimuziki “Nidhamu” na asipokuwa makini ataanguka tena. Na wala sitaki kukumbusha mabaya yake kama lile la kuwahi kumrushia makonde Prof Jay, Black Rhino na hata marehemu Arbet Magweair katika nyakati tofauti.

Chid Benz katika mahojiano aliyofanya Uhuru Fm hakusita kusema “Mpaka sasa hakuna msanii ambaye ameweza kufanikiwa na kufikia mafanikio ambayo nilifikia katika kipindi cha nyuma. Sijamsikia yule mtu ambaye anafanya matukio kama mimi, yakuwa na msafara wa gari kumi, kusafiri kwenye show na watu 30, ukasikia watu 7 wamezimia kwenye show, bado sijawahi kusikia matukio kama hayo labda bwana Joh Makini amefanya show Arusha wakazimia watu 9 lakini nawasikia hao, kama Joh Makini namsikia na namuona kwenye muziki huu the way wametengeneza yeye ndo awe ameshika hili game, lakini hana nguvu”

Sidhani kama yupo anaepinga kuhusu mafanikio ambayo aliwahi kupata Chid Benz. Lakini pia ni vyema kumkumbusha kila jambo lina wakati wake lakini wakati ni ukuta. Na mara zote ukipewa nafasi itumie vyema

Leo hii huwezi kutaja wasanii wa hiphop 10 bora wa Afrika mashariki bila kutaja jina lake Joh Makini. Ila pia ni moja kati ya wasanii wachache mno wanaofanya vyema kwenye vituo vya runinga vikubwa barani Afrika kutoka hapa nchini Tanzania.

Kauli ya Chid Benzi kusema Joh Makini ni msanii wa kutengeneza zinaonyesha ni wazi bado hayupo kimuziki bali anataka kuleta ubishani usio na tija wala maana. Kweli wapo wasanii wa kutengenezwa ila sio Joh Makini, ukitazama tangu wimbo wa Hao mpaka sasa Perfect Combo hakika uwezo na ukubwa wa kipaji unaonekana.

Ukisikiliza wimbo wa Joh Makini unaitwa “Ufalme” ambao ulitoka mwaka 2010 utajua ni jinsi gani Chid Benz hakupaswa kusema Joh Makini ni msanii wa kutengenezwa. Pia ni jinsi gani msanii unatakiwa usimame katika njia zako bila kugusa wengine katika mlengo wa matatizo. Sioni kama ni vyema kutumia neno kuwa Chid Benz anatafuta kiki ya Joh Makini.

Tukirudi katika wimbo wa ufalme kuna mistari mingi aliyoisema Joh Makini ila katika michache ambayo imeweza kubeba uhalisia wa hili ni jambo ni “Hiphop sio mistari miwili mitatu snitch/ vita vya kweli ni dhidi ujinga na umasikini/ sio vita na joh makin mwanao atarithi nini/ sipendi tuishie uadui kama wa nesta na tosh/ uwanja bado mpana kuna mengi ya kufanya/ saka maushindi hata ikibidi kwa njia za panya/ kiumri ni watu wazima kiakili watoto wa juzi/

Hayo ni machache kati ya mengi aliyoweza kuzungumza Joh Makin katika verse ya kwanza. Ukitazama hoja ya Chid Benz kuwa Joh ni msanii wa kutengenezwa utaona ni jinsi gani alikuwa amepotoka. Ni wazi uwanja wa muziki wa kizazi kipya ni mpana hivyo hakuna haja ya kusema fulani anatengenezwa au kuleta malalamiko kama sio kufanya muziki mzuri.

Katika wimbo huu wa ufalme Joh aliendelea kusema mengi ambayo ni “Kazi ndio zinaongea/ Wanapata homa jinsi flow zangu zilivyohot/ niko hapa kwa ushindi sio kwa dro/ ni joh ninae waharibia kuanzia studio mpaka show/ wanasingizia media zinabana hii ni soo/ leo game ni tofauti na michezo ya meto/ level hizi haufiki, hauna bifu ni jelous acha na ongeza bidii.

Ni wazi Chid Benz anatakiwa kufanya kazi ya muziki mzuri, na si kusema hovyo juu ya wasanii wengine wanaofanya vyema sasa kwenye ramani ya Afrika.

Chid Benz sasa yuko chini ya Babu Tale kila mmoja anafahamu hilo. Lakini tusiwe waoga wa kusema kweli, kusimamamia msanii si pesa tu bali kumjenga awe katika picha ya biashara pia hata kumuelekeza katika kujibu maswali katika mahojiano.

Iko wazi wengi hawajui kama mahojiano yanachangia kukupandisha kisanii na hata kukushusha. Na si lazima kwenye mahojiano ujibu kila swali yapo maswali ambayo watangazaji na waandishi uuliza tu imradi kupima uelewa wako. Pia ukumbuke wakati unajibu kile ulichosema ndio jamii itachukua kama kilivyo.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwenye moja ya hotuba yake mwaka 1995 “ni bora uwe masikini wa kila kitu lakini usiwe na umasikini wa mawazo na kufikiri.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez