Watangazaji na Madj walioko kinyume na mdau mwenye kuangusha hiphop

radio-microphone

Watangazaji na Madj walioko kinyume na mdau mwenye kuangusha hiphop

Kwasasa kumekuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wasanii wa hiphop mpaka kwa mashabiki wake. Malalamiko mengi ni kukosa kwa kupewa nafasi kwa muziki wa hiphop kwenye vituo vya radio na runinga, lakini muziki wa hiphop ndiyo muziki wenye nguvu katika mitaa iliyomingi na haya huwa tunaona wakati wa matumbuizo mengi kwenye viwanja tofauti.

Ila ukirudi katika historia yani mwaka 1990 mpaka mwaka 2000 muziki uliokuwa umetawala katika ramani ya muziki wa kizazi kipya ilikuwa ni hiphop. Miaka ya 2000 hapa waliibuka wapiga miluzi ambao walivutwa na muziki kuingia katika muziki lakini ni wazi kwa nafasi waliyopewa wemeweza kubadili upepo kwa kiasi kikubwa.

Moja ya vitu ambavyo vinanifanya nijue historia nzuri na mwenendo wa muziki huu wa kizazi kipya (Bongo Fleva/Hiphop) ni uwepo wangu karibu na wasanii wakongwe ambao si wachoyo katika kuongea ile kweli.

Moja ya kitu ambacho niliwahi kuambiwa na mkongwe wa muziki huu Fredrick Malick maarufu kama Mgosi Mkoloni ambaye ni moja kati ya wasanii wawili wanaunda kundi la Wagosi wa Kaya. Mkoloni aliwahi kuniambia “Batro huyu mdau ambaye amejiaminisha wazi sasa kuua hiphop hajaanza leo. Ila tangu mwaka 2000 aliwahi kusema tukiwa kwa Mj Record pale kuwa “Lazima niue muziki wa hiphop” ingawa sikuacha kusema hawezi kuua muziki wa hiphop hata siku moja.

Ni ukweli usipingika ni ngumu kuua muziki ambao jamii inahitaji. Licha ya kuwa na muda mdogo kwenye vyombo vya habari lakini bado jamii imeweza kuelewa kwa kiasi kikubwa muziki huu wa hiphop.

Ni wazi mdau ameshindwa kudidimiza kama sio kuua kabisa, na muziki wa hiphop umendelea kutengeneza heshima hata kwa kuweza kutoa viongozi kadhaa wa serikali ambao wamepitishwa na wananchi. Hii inaonyesha hiphop ina nguvu kwa namna gani. Na hata katika uchaguzi mkuu mwaka jana tumeona mkongwe wa hiphop Mr Sugu akiwa ni mbunge aliyechaguliwa kwa kura nyingi kuliko wabunge wote.

Katika historia inatuonyesha kuwepo kwa mtangazaji Taji Liundi ambaye kwa nguvu yake amechangia vyema kuenea kwa muziki wa hiphop. Na mpaka leo huwezi kuzungumzia kuenea kwa muziki huu kupitia katika vyombo vya habari bila kumtaja mtu huyu. Lakini pia walikuwepo wengine wengi ambao kwa mchango wao wamefanya muziki wa hiphop ufike ulipofika. Mtu kama John Dilinga ni moja kati ya wengi.

Hakika wapo watangazaji na Madj ambao wameweza kupokea kijiti vizuri katika upande wa kuendelea kutoa ushirikiano wa kuendeleza muziki wa hiphop kila iitwapo leo.

Vita ya kuangusha hiphop ni kubwa ni si kama wanaonavyo mashabiki walio mbali katika vyombo vya habari. Iko wazi hata Madee alivyosema hiphop haiuzi ni wazi aliongea hoja ndogo mno, na hoja hii wenye uelewa mpana walishindwa kumuelewa. Kimsingi hakuna muziki usiokuwa biashara, bali hauwezi kuwa biashara kama haupati matangazo ya kutosha.

“Ukweli lazima usemwe” nguvu ya mdau katika vyombo vya habari ni kubwa mno. Wapo wanaoamini kuwa uwezo wake umefanya awe na nguvu hata katika baadhi ya vyombo vingine.

Licha ya nguvu hiyo ya mdau ila wapo watangazaji kadhaa na Madj ambao ni wazi wanawakilisha vyema hiphop katika vipindi vyao. Na kiuhalisia wameweza kukubalika na mashabiki walio wengi kwa jinsi vile wanavyoweza kusukumua gurudumu la muziki wa hiphop.

Jabir Saleh ni moja kati ya watangazaji ambao wanatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha hiphop inapata nafasi kama ilivyokuwa awali. Jabir amewahi kuanzisha chati pekee ya muziki wa hiphop ambayo ilikuwa ikifanyaika kila ijumaa na hii ilikuwa ikichukua nyimbo 10 za bongo hiphop pekee.

Huo ni wakati yupo Times Fm katika kipindi cha The Jump Off. Kabla ya sasa kuhamia katika kituo cha radio Efm.

The jump Off ilikuwa ni moja kati ya vipindi vichache ambavyo pia viliingia mtaani kutafuta vipaji vya muziki wa hiphop. Hakika hii ilikuwa nguvu ya mtu mmoja Jabir Saleh ambaye ni maarufu kwa jina la Kibonge Tozi au Kuvichaka.

Tumeona sasa ameanzisha kipindi cha Ladha 3600 pale Efm, pia hasiti kutoa nafasi kwa kuendeleza muziki wa hiphop na sasa kipindi chake ni moja kati ya vipindi pendwa vya burudani nyakati za mchana.

Licha ya kuwepo kwa kipindi cha Hiphop tu kila jumamosi katika kituo cha Efm kipindi hicho kinaitwa X RAY Mionzi. Na sasa hakina mtangazaji bali nhupigwa nyimbo tu za hiphop. Lakini ni wazi mashabiki wamekuwa wakitamani zaidi kipindi hiki akabidhiwe jabir Saleh wakiamini kuwa ni moja kati ya watu muhimu kwenye hiphop mwenye kujua mengi katika upande huo.

DJ Tass mwenyewe hupenda kujiita “Nyota wa mchezo”Wengi wananfahamu kama ni Dj lakini jamaa ana uwezo wa kutangaza vizuri na sasa amekuwa akishikilia kipindi cha Kwetu Fleva ndani ya Magic Fm. Jamaa anatumia nguvu kubwa mno katika kuhakikisha hiphop inasimama vyema kwenye mitaa, mara nyingi amekuwa akipiga zaidi nyimbo za hiphop. Na hilo limemfanya awe mashabiki wengi katika mitaa ya wapenda muziki huo ambao kwa mujibu wa matumbuizo mengi inaonyesha ni muziki pendwa.

Ncha Kali, wengi wanamfahamu kwa jina hilo lakini jina lake kamili Ruben Ndege. Kwa wakati wake ameweza kusukuma vyema muziki wa hiphop. Na ndiye mtu ambaye aliweza kufanya tukawajua vyema wakina Nikki Mbishi, Godzilla, Stereo, One Incredible na wengine wengi. Wakati huo alikuwa akifanya kipindi cha So So Fresh pale Clouds Fm. Kuondoka kwake ni wazi kumefanya kushuka kwa grafu ya kuchezwa hiphop kama awali ilivyokuwa.

Wengi walikuwa wakitabiri kuwa Adam Mchomv ataweza kuendelea kijiti cha Ncha Kali lakini imekuwa ndivyo sivyo. Adam Mchomv ni wazi amekuwa msemaji wa hiphop ya Arusha na si hiphop kwa ujumla. Hivyo kwa sisi wachambuzi hatuwezi kumuweka kama anasaidia muziki wa hiphop isipokuwa Arusha.

Ezden The Rocker, Kiss Calloba ni kipindi kilichompa umaarufu kwa wapenzi wa muzuki wa hiphop. Huwezi kupinga mchango wa Ezden wakati yuko Kiss Fm Mwanza. Lakini hata sasa tumeona mara nyingi akija katika Kilinge pale Msasani na kushirikia na wasanii wachanga hata wakubwa katika ushauri na mahojiano katika kipindi chake cha runinga ambacho ni About Bongo.

Dj Mafuvu ni moja kati ya madj bora tuliobarikiwa kuwa nao kwenye muziki wetu mzuri wa hiphop. Mafuvu aliwahi kutajwa mpaka na shirika la utangazaji BBC kuwa ndiye Dj anatoa nguvu yake katika muziki wa hiphop Afrika ya Mashariki. Na wakati huo alikuwa katika kituo cha East Africa Radio ambapo tangu kuondoka kwake ni wazi pengo la hiphop linaonekana bila kificho. Hiphop Base ni moja kati ya vipindi ambavyo vilikuwa ni bora kwenye Runinga katika kupaisha hiphop mbali zaidi. Wakati huo usukani ulishikwa na mkongwe Saigoni na hakika kwa namna yake amechangia kukua na kuenea kwa bongo hiphop. Lakini kipindi hiki kilifutwa miaka kadhaa nyuma. Ila nguvu yake Saigon itabaki kuwa alama tosha kwenye muziki huu wa hiphop.

D7, African Beat ni kipindi ambacho kilikuwa kikiruka kila siku za wiki saa 12.00 jioni mpaka sa 2.00 usiku. Na hapa ulikuwa unakutana na D7 ambaye mapenzi yake kwenye muziki wa hiphop hayakuwa madogo. Mchango wake ni mkubwa mpaka sasa hiphop ilipo. Lakini sasa hayupo Kiss Fm, na mashabiki wa hiphop wanakosa kile walichokuwa wanakipata awali.

Jeff Jery, ni dj kutoka Rfa na Kiss Fm. Wasanii na mashabiki wa hiphop wanajua kile anachokifanya Jeff Jery. Ni miongoni mwa watu wanatoa nguvu yao katika muziki wa hiphop na mpaka sasa na kilinge cha hiphop kinahofanyika kila jumamosi pale Jijini Mwanza.

Itaendelea…. Kaa karibu na www.tizneez.com

Kama una maoni yako tuandikie chini hapo.

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez