Watangazaji kuwa mameneja ni kukua kwa muziki au kuua muziki?

Watangazaji kuwa mameneja ni kukua kwa muziki au kuua muziki?

Waswahili husema “Kidogo ni tamu na kingi ni chungu”. Ni wazi nyakati za kuchangamka kwa muziki kuliibuka watangazaji lakini na madj kuwa mameneja wa wasanii kadhaa, lakini ilikuwa katika uchache mno.

Lakini nyakati hizi imekuwa ni kawaida na idadi ya watangazaji kuwa mameneja imekuwa kubwa mno.

Jambo hili limeleta mijadala katika vijiwe vingi  vya muziki, wengi wao wakiwa na hofu kubwa juu ya muziki kuharibika kwa watangazaji kuvamia umeneja kwa kasi kubwa.

Watangazaji kuwa mameneja si kigezo cha muziki kukua kama wengi wasemavyo bali ku kurudisha muziki nyuma katika kasi kubwa tu. Na lazima jamii ya muziki ijue yakuwa katika vigezo vya muziki kukua hakuna kigezo cha watangazaji kuwa mameneja.

Lakini waswahili wakati wote husema “Lake mtu halimtapishi” Ni vyema kutafakari neno hili ambalo ni fupi lakini maana yake ni ndefu iliojaa upana.

Kitendo cha mtangazaji kuwa meneja ni wazi upendeleo katika biashara yake ya muziki kutoka kwa msanii wake itakuwa kubwa kwa maana ya kupiga wimbo wake kila wakati wa kipindi chake, lakini hata watangazaji wenzake kufanya hivyo ili kumsaidia msanii wake.

Ikumbukwe biashara yoyote inahitaji matangazo hivyo muda ambao atakuwa anapewa hewani utafanya aonekane bora Zaidi ilihali ni upendeleo kwaajili ya manufaa ya biashara yao ya muziki.

Na huenda wakati huo msanii husika kawa na wimbo ambao ni mbaya usio vigezo lakini yakuwa yu sehemu ya mtangazaji ni wazi utapewa nafasi. Ndiyo maana halisi ya “Lake mtu halimtapishi”

Hivyo watangazaji ni vyema wangebaki kuwa watangazaji na jamii yapaswa ijue si lazima wao kuwekeza katika uwanja wa muziki. Ni vyema kuwekeza sehemu nyingine tofauti maana uwekezaji ni mahala popote pale.

Hakuna mipaka katika uwekezaji lakini katika muziki kwa upande wa watangazaji ni wazi mvurugano wa upandeleo utatawala kwa upana mkubwa mno.

Lakini nani aseme haya miaka hii ya wasanii waliojaa hofu bali wepese kusema pembeni. Lakini twaambieni wasanii yakuwa waswahili husema na huamini yakuwa “Kinolewacho hukata”

Follow Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Youtube Tizneez

Tuachie maoni yako hapa