Wasanii wanaangamia kwa kukosa maarifa

10312604_10207130018722325_7878957141649917082_n

Wasanii wanaangamia kwa kukosa maarifa

Swala la kuambiana ukweli ni jambo jema na zuri, na kuelezana ukweli yapasa iwe katika kila siku katika namna yoyote ya maisha yetu.

Kuwa na maarifa inafanya uweze kufanikiwa katika mambo yote ambayo utakuwa ukifanya katika shughuli zako za kila siku. Yamkini wengi hawajui maana ya neno “Maarifa”

Maana ya neno “Maarifa” ni hekima au ufahamu au uwezo wa kutambua jambo na kukabiliana na jambo hilo. Ninapozungumzia kuhusu maarifa ni maana ya wasanii wanavyokabiliana na maisha yao ya kisanii ni wazi wengi wao wamekosa kabisa maarifa juu ya kazi zao na hata haki zao bila kusahau umoja wao.

Kwa kukosa kwao maarifa tumeendelea kuona wasanii wakiendela kuwa watumwa mbele ya watu wachache ambao kupitia wasanii hao wameweza kufaidika kwa kiwango cha juu. Na wakati huo msanii akibaki mwenye shida na dhiki kumtawala.

Ni wazi kasumba kubwa waliyonayo ni kupinga ukweli mbele ya watu ila kuukubali ukweli wakiwa wamejifungia ndani.

Vipaji walivyonavyo ni vipaji vya hali ya juu, ila utumwa wa kifikra yani kukosa maarifa ndio sababu kubwa inayopelekea kuwaona wakiendelea kuangamia kila iitwapo leo.

Katika ramani ya muziki wa kizazi kipya kama ikitokea msanii mmoja kujitambua na kudai haki zake basi mtengano kati yake yeye na wasanii wengine huwa ni mkubwa na wawazi. Jambo hili hunisikitisha mno na kuona ni jinsi gani wasanii wengi wamekuwa na fikra mgando.

Mioyo yao imejaa uoga, lakini hawajui “Uoga hauna msaada zaidi ya kukuvuruga akili”

Tuna mifano mingi na yenye tija, wapo wasanii ambao walikuwa na vipaji vikubwa ila waliweza kupotea katika uso wa dunia bila kuwa na chochote kile katika mlengo wa mafanikio yani malipo stahiki juu ya kipaji chake.

Kwa ukubwa wa Sanaa ya muziki kwasasa katika upande wa muziki wa kizazi kipya ni kichekesho kuona bado wasanii wamekuwa hawana hata maarifa yakutambua haki zao za msingi.

Lakini pia katika swala zima la kukosa maarifa tumeona mpaka leo bado wasanii wamekuwa hawajui wala kujali kuhusu umuhimu wa chama chao TUMA yani Tanzania Urban Music Association.

Kwa kukosa kwao maarifa tumeona wakionekana wakiwa wenye furaha kwa kupiga picha na viongozi wakubwa wakiwa wameshika  grasi za juisi, na hata kama wakiambiwa kueleza matatizo ya kwenye muziki basi hupatiwa hotuba wasome bila kujua hotuba inakwenda kumnufaisha mtu mwingine na sio wao wasanii. Kama wangekuwa ni watu wenye maarifa hakika hotuba ingeandaliwa na chama chao TUMA maana ndio kitu pekee chenye dhamana juu yao. Lakini je hayo wanayafanya?

Si kificho mtu mwenye maarifa hujali haki zake zote kwa ujumla bila kujali ni nani anataka kuzichukua kwa wakati gani. Bali asiye na maarifa hubaki akitumika bila kujali haki zake.

Amka msanii ni muda wa kuifaidika na kipaji chako, ni muda wa kuacha kutumika bila malipo

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube Tizneez