Wasanii na maisha ya usanii mbele ya mikataba.

Wasanii na maisha ya usanii mbele ya mikataba.

Kuna nyakati tuliwahi kuandika yakuwa “Wasanii wengi wanaangamia kwa kukosa maarifa” na semi hii ikawa chukizo kwa wasanii wengi ambao wamejaa uzito katika semi zenye tafakari.

Lakini maana ya neno ‘Maarifa’ Ni utambuzi au ujuzi wa jambo katika kupata ufahamu wa leo na kesho yako katika usawa wa usawia wa yote.

Hakika mtu akosapo maarifa ni rahisi mno kuangamia. Na hata neno kuu la nena yakuwa “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Naam! Sasa ni uhalisia wa uhalisi wa maisha ya wasanii wengi katika usanii mbele ya mikataba.

Hakuna jambo jema kama tafakari yenye maarifa kabla ya kusaini mkataba wowote ule, na pia ni vyema zaidi kuwaona wajuzi wenye ujuzi na maswala ya mikataba. (Sheria)

Wapo wasanii ambao wao hunena yakuwa “Dhiki ilifanya nikasaini mkataba” kwa maana ya tazamo la dhiki ya nyakati hiyo. Hivyo husaini mkataba kwa upana wa kula tamu katika nyakati hizo bila tafakari ya mbele.

Hakika sasa tunaamini vyema yakuwa “Mwenye njaa hana miiko” lakini yapasa wasanii walio wengi wajue yakuwa “Si kila kiliwacho kinafaa” (Uhalisi).

Tumeona pupa ya mikataba kwa wasanii wengi mno, na baada ya nyakati fupi zogo huibuka katika mengi. Na tokeo la zogo huwa ni hali ya mfadhaiko kwa msanii katika fedheha kubwa.

Kwani tumesahau mfadhaiko wa Q Chief?, Je!Chemical nae? Lakini Mo Music, na katika upana wa Rich Mavoko je? Ilihali Omg  wakiwa bado havieleweki mbivu na mbichi kwa mapana yao.

Ni vyema wasanii wapunguze pupa katika kusaini mikataba, maana katika uwazi maarifa lazima yachukue nafasi kwa hali kubwa ili kuondoa mifadhaiko ambayo haina maana katika nyakati zijazo.

Pupa haina maana katika kukomboa njaa uliyonayo kwa nyakati hizo, lakini ni vyema wasanii wajue yakuwa “Mwenye pupa hadiliki kula tamu”  Zuri ni maarifa katika sainio la mkataba ni vyema makaratasi yapewe heshima kubwa bila tafakari ya njaa kwa nyakati hizo.

Na fedheha za sasa kwa wasanii hawa ni vyema ziwe somo lenye maana na kueleweka kwa wasanii wengine juu ya upana wa mikataba katika uingiaji na watu wengine katika usimamizi wa kazi zao na mengine mengi.

#TuzungumzeMuziki