Usipojua maana ya “Sanaa ya muziki” Weusi watakuwa ni chukizo kwako.

Usipojua maana ya “Sanaa ya muziki” Weusi watakuwa ni chukizo kwako.

Daima Tizneez huhubiri #TuzungumzeMuziki kwa maana ya kueleza kwa upana uhalisi wa Sanaa ya muziki.

Ni ufundi ambao anatumia msanii ili kuwasilisha fikra/mawazo yaliyoko ndani yake, vilevile Sanaa ya muziki ni uzuri unaojibua katika umbo lililosanifiwa. Ilihali kusanifu ni kuumba au kufanya jambo au kitu  kwa kutumia ustadi ili kiweze kuvutia kwa hadhira.

Msanii hueleza hisia zake katika upana wa Sanaa ya muziki, na katika uhalisi yaweza kuwa kwa ala za muziki au bila hata ala za muziki.

Je!katika upana huu wa Sanaa ya muziki kuna haja ya kuwashangaa Weusi katika wimbo wao wa mdundiko?

Sanaa ya muziki ina upana mno katika kutafakari, ndiyo maana zipo nyimbo ambazo zimepigwa ala ya kinanda na msanii akaweka mashairi yake na ukawa wimbo kamili.

Kwa upana huu wa Sanaa ya muziki inaonyesha namna ya wasanii na mashabiki wengine wajue yakuwa ‘Sanaa ya muziki’ ni pana mno. Na je!tunatafakari juu ya Sanaa nyingine?

Mfano ipo Sanaa ya uchoraji, je!tunaweza sema mchoraji aliyechora picha bila kupaka rangi si mchoraji? na amekosea? Ni wazi hapana isipokuwa tunapaswa kutazama ni kipi ambacho alitaka kuwasilisha kwa hadhira.

Changamoto ya wengi ni Weusi kutumia mdundo wenye mfanano wa kapuka, lakini je!tumesikiliza kile ambacho wametaka kuwakilisha kwa hadhira kupitia wimbo huu wa mdundiko?

Weusi wamesawiri maisha ya wengi katika mengi yenye uhalisi, nasi hatuachi kukumbuka semi ya mswahili ambayo yanena yakuwa “Mpumbavu asipoelewa jambo hugadhibika, ilihali mwerevu hukuna kichwa”

Tuache Sanaa za watu zifanye kazi katika hali ya upana, na kumpangia msanii cha kufanya ni kuweka mipaka katika kipaji chake.

#TuzungumzeMuziki.