Ujinga ni nini? Ujinga ni kumlaumu Ruge (Clouds Media Group)

Hakika ni ujinga ulioje kumlaumu Ruge (Clouds Media), kwani ni dhahiri kuwa cha kuazima kamwe hakisitiri makalio. Ni jambo lililowazi kabisa, kwamba kiu ya wasanii walio wengi hususani wachanga ni kusikika Clouds! Lakini sidhani kama wamewahi kujiuliza kwanini wanatamani kusikika mahala hapo kwa ukubwa zaidi na si kwingineko?
Hili linanirejeshea msemo wa wahenga walionena “Usione vyaelea, ujue vimeundwa” basi ndugu zangu yawapasa mtambue kuwa umahiri wa Clouds haukuja kama pepo za bahari ziletwazo na kupwa na kujaa kwa maji yake. Bali kwa machozi, jasho na damu vya wanaClouds wenyewe ndio yaliyoweza kuijenga mpaka kufikia pale.

Wasanii wanapaswa mtambue kuwa Ruge ni mfanyabiashara, na kanuni kuu ya biashara ni kutengeneza FAIDA. Pasi na faida hiyo si biashara, ni chuma ulete…Hasara si ajabu. Wakati Ruge anatimiliza kanuni ya kibiashara, wengine tunampa tuhuma za unyonyaji. Siwezi kusema kwamba sio kweli kwasababu sina ushahidi, yumkini ni kweli akawa mnyonyaji lakini je, ni nani anayependa kuona haki ya mwenye haki inadhurumiwa? Je mwenye haki amekatazwa kufikisha shauri hili mbele ya mabaraza ya waamua haki(Mahakama)?

Hakuna bure, ukiona umepewa bure, ni wazi kuna mtu sehemu amegharamia hicho upewacho. Wakati nafsi yako inajiongopea yenywewe kuwa unasaidiwa, na kwa makusudi ikijisahaulisha kuwa Clouds  sio mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wala Ndugu Ruge Mutahaba sio Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo. Na hata kwa bahati mbaya hautaki kukumbuka kuwa Clouds Media ni kampuni binafsi inayoendeshwa kibiashara na Ndugu Ruge ni Mkurugenzi wake wa vipindi na uzalishaji. (Ni jukumu lake la kila siku kuongeza uzalishaji ambao utaleta tunu kwa kampuni akiwa kama Mkurugenzi wa kurugenzi ya Uzalishaji)

Hadithi inaanzia pale unaposogea katika viunga vya Clouds na kuomba usaidiwe, na kurugenzi ya uzalishaji unajiridhisha kuwa kuwekaza kwako hakutakuwa kazi bure, ni wazi uliondoka ukiwa na tabasamu lenye bashasha ukijihisi una bahati ya mtende(kumea jangwani)! Lakini ujinga unautawala ufahamu wako na kuona si busara kuhoji kuhusu makubaliano yenu, wao (Clouds) watakupa utakacho, je umeshafikiri jinsi gani wao watanufaika vipi na uwepo wako? (Bure gharama)

Taharuki, taharuki huja pale ambapo wewe umekwisha timiziwa mahitaji yako, na muda wa Ruge kurejesha mtaji wake pamoja na faida umewadia (biashara). Ghafla unajitia uhayawani na kupiga kelele za kuomba msaada kwa jamii. Na kwakuwa sisi nasi tumeamua kujitia upofu wa mawazo tusiokuwa nao, tunaanza kulishikia bango swala hili, na kumpa Ruge ushetani (Kutoka kuwa Malaika mkombozi, mpaka malaika muhasi(Lucifer), ambaye hastahili tena). TUACHE UNAFIKI!

Fahamu kuwa unaruhusiwa kuvunja mkataba muda wowote, endapo tu utaona kuna haja ya kufanya hivyo na hautakiuka kifungu chochote cha mkataba huo. (Rubby aliamua kuuvunja kwa ulimi wake…)

Baniani Mbaya, Kiatu Chake Dawa, Unaomba/kuombwa uimbe bure, baadae unasema umeimbishwa bure. Huku ukitoa tuhuma zako zilizosheheni maelezo kedekede, Acha unafiki hakuna aliyekuimbisha, bali uliimba mwenyewe bure. Kwakuwa uliona fursa ya kufanya hivyo, ulifikiri kibishara faida ambayo ungeipata siku za usoni. Sasa umekwisha ipata hiyo faida unamuona aliyekupa jukwaa la kuimba alikunyanyasa (Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni)

Mfanyabiashara anaweza kuacha biashara aifanyayo mara tu anapoona haina tena tija kwake. Lakini pia anaweza kuendelea nayo endapo ataona tija iliyopo ni kubwa. Nadhani Ruge naye anafanya hivyo akiwa kama mfanya biashara, SIO KOSA.

Fahari wawili hawakai zizi moja, WCB imekuwa chapa kubwa ya biashara (Kongole). Na hiki hasa ndicho kiini cha mgogoro, kwa kuwa tayari misuli ya fahamu za WCB imetanuka vya kutosha na kujizolea uzoefu katika biashara. Hivyo katika kila kazi watakayoifanya wanatanguliza mbele kanuni kuu ya biashara(faida). Hivyo basi, wakati Ruge anataka kutengeneza faida kutoka kwa WCB, na WCB wanataka kutengeneza faida kutoka kwa Ruge (Zogo) kila mtu anataka kumzidi kete mwenzie.

Mtenda Akitendewa, huisi kaonewa! Ruge naweza kusema ni mbobezi katika biashara, kwani alivyoona hawezi kutengeneza faida kutokana na WCB akaamua kuachana nao. Lakini sasa WCB wakaona kuwa wameonewa na Ruge kwa kuwa hawatosikika tena Clouds. Dhambi ya kujisahaulisha kuwa Clouds ni kampuni binafsi na inayojiendesha kibiashara inawatafuna. Wanadhani ni haki yao kuendelea kusikika(Ujinga). Badala yake wanaomba msaada kwa jamii kupitia mitandao ya kijamii wakitishia kuweka bayana maovu ya Ruge katika Muziki. Kama kuna maovu ambayo yamefanywa na Ruge nadhani huu ni wakati muafaka wa WCB na wasanii wote wanaomshutumu Ruge kwenda kwenye mabaraza ya haki kudai haki zao. Swali je, siku zote Salam (WCB) alikuwa wapi kutuo huo uovu? Au ndio sizitaki mbichi hizi?

Tafakuri ‘Ukisema Muziki ni biashara, fanya na ufikiri kama mfanyabiashara. Wekeza, usisubiri hisani’