Tuyatafakari ya G Nako tujenge yenye tija

index

Tuyatafakari ya G Nako tujenge yenye tija

Muziki ni moja kati ya njia inayotumika kufikisha ujumbe katika mambo mbalimbali. Kupitia muziki unaweza ukafahamu mengi yenye tija na hata kukusaidia kupambua mengi katika maisha ya kila siku.

Katika upenzi na muziki kila mtu huvutiwa na jambo lake katika wimbo fulani. Wapo ambao huvutiwa na Ala, wengine huvutiwa na jinsi ya msanii alivyoweza kuweka maneno yake juu ya Ala hiyo. Na wengine huvutiwa na kila kitu anachokuwa anakisikia katika wimbo huo.

G nako ni moja kati ya wasanii wenye vipaji vya hali ya juu katika ramani ya muziki wa kizazi kipya. Pia Arosto ni wimbo wake unaofanya vyema sasa katika Radio na Runinga mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

OG ni wimbo ambao uliweza kushikika haraka katika mitaa mingi ya vijiwe vya wapenda muziki wa kizazi kipya. Wengi wao wanaguswa na Ala jinsi ambavyo zimepigwa na vile ambavyo G nako ameweza kucheza na maneno vyema. Hakika ni wimbo mzuri.

Lakini si katika kucheza na maneno ila hata alichokuwa anakisema ni chenye maana.

Moja kati ya mengi ambayo ameimba ni “Na huu si muziki wa kizazi kipya! Mtaani vipaji vinakufa”

Unaweza kuchukulia ni sentensi ndogo katika wimbo huo, lakini katika maisha ya kila siku katika ramani ya muziki wa kizazi kipya ni sentensi iliyobeba maana na uzito ndani ya muziki na hata nje ya muziki.

Ni ukweli ambao wasanii, watangazaji, waandishi na hata wachambuzi wa muziki wa kizazi kipya hawausemi. Ila ni uwazi ambao mtaani tunauona na hata katika majukwaa mengi ya mtaani huwa tunaona vipaji vingi ambavyo hupotea mithiri ya upepo. Vipaji hivyo hupotea kwa kukosa kupata msaada maana wengi wao hutokea katika familia duni, lakini pia watu wa kuwashika mikono ili kufikia mahali stahiki.

Ila katika kauli ya Gnako “Mtaani vipaji vinakufa” ukitazama kwa uelewa mpana ni ukweli usiopingika watu wa Blog, Radio, Runinga na hata magazeti hakika wamekuwa na watu wenye kufinya nafasi kwa watu wenye vipaji vya kweli.Bali hupenda upuuzi wa wadada wenye makalio makubwa ambao hujinadi kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia watu wachache wenye upuuzi usiofaa mbele ya jamii lakini cha kushangaza ndio wenye kupewa nafasi kubwa katika ngazi ya Runinga, Radio, na Blogs.(Mohajiano)

Naamini watanzania wapo wenye vipaji vingi, lakini pia wenye kuua vipaji hivyo nao wamekuwa wengi, hata leo tunaona wengi wao kupitia upuuzi wao wameweza kupata nafasi kadhaa kwenye mambo mengi. Hii inanifanya nihoji je ili upate nafasi ni lazima ufanye jambo la kipuuzi?

Hakika kwa hilo tutaendelea kuona vipaji vinakufa kila iitwapo leo, maana mtaani vipaji vipo na vina uwezo wa kufanya makubwa mara tu wakipewa nafasi.

Wengi wameamini katika kujuana huyu ni nani, ila kama kweli wahusika waliopo katika nafasi yenye uwezo wa kusaidia watu katika kuonyesha vipaji vyao hawatakuwa na mambo mengi yasiyofaa hakika naamini kuna vipaji vingi tutaviona na vitachangia kuokoa wengi walioko mtaani.

Ili vipaji visipotee ni vyema kutoa muda wa kumsikiliza mtu pale ambapo anakuwa amekuletea kazi yake ya aina yoyote ile. Mpe muda wako msikilize, kumsaidia mtu si pesa bali ushauri tu ni kitu kikubwa.

Amini kwenye kipaji chake, kishike kipaji chake akomboe familia yake.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez