TUSIMCHEKE WALA TUSIMDHIHAKI CHID BENZ

chidbenz

TUSIMCHEKE WALA TUSIMDHIHAKI CHID BENZ

Poleni rafiki zangu mliopotea kwa madawa Hii ni kwa mujibu ya Mr Blue ambaye alisema maneno hayo katika wimbo wa 26 number ambao ni wimbo halali wa Nyandu Tozi, ambapo katika nyakati hizi pia Mr Blue alikuwa akipokea shutuma kutoka kwa baadhi ya mashabiki kuwa anatumia madawa ya kulevya.

Kesi ya madawa imeendelea kukua katika muziki wa kizazi kipya, wasanii wengi waeonekana kutumia, wapo waliamua kukiri na hata kutaka kuacha ila wapo ambao mpaka sasa hawajakiri lakini ni wazi wanatumia. Ila wapo wengine ambao sina imani kama kweli wanatumia licha ya mashabiki kuhisi na hata kuwashambulia katika mitandao ya kijamii kama wanatumia, mmoja ya watu ambao mara nyingi amekuwa akikumbana na adha ya kushambuliwa ni Young Dee, wengi wamekuwa wakihisi kama anatumia licha ya yeye mara nyingi kutoa ufafanuzi kuwa hajawai kutumia na hatakuja atumie.

Chid Benz ni moja kati ya wahanga wakubwa wa madawa ya kulevya, binafsi namuona ni shujaa. Unaweza ukapata mashaka kwanini namuona shujaa Chid Benz? Katika uhalisia mtu ambaye anakiri kwa kinywa chake kwamba alikuwa natumia ni wazi amekubali tatizo lake. Na katika hali ya kawaida hata katika mafundisho ya wazazi iko wazi kama mtu anakiri kosa lake ni wazi sasa ameamua kuondokana na tatizo hilo.

Hivyo kinachofuata baada ya mtu kukiri kosa lake ni kupata msaada kama ni wa mafundisho au ukaribu na watu ambao si rahisi ya yeye kufanya aliyokuwa anafanya.

Hainishangazi kwa walio wengi kuwa na tabia za kutenga wahanga wa madawa na hata wengine kudiriki kusema hana akili, hajitambui. Kwangu huwa naona kama si jambo jema pale mtu anapopata tatizo kumsema vibaya au hata kumtenga, kama sio kumsaidia kuondokana na tatizo.

Ujana una mambo mengi, marafiki pia wana mambo mengi. Wengi wakati wanaanza huanza kwa kutokujua wapo ambao wanaweka hata katika sigara hivyo wengi wao huanzia humo bila ya wao wenyewe kujijua. Na muda wanaokuja kustuka basi huwa tayari wameshaingia katika dimwi la madawa ya kulevya (Uteja)

Sitaki kujua Chid Benz alianzaje ila namuita shujaa ambapo ni wazi ameamua kuacha matumizi hayo na hata siku ya ijumaa ya wiki ya jana alizungumza mengi katika kituo cha Ea radio katika kipindi cha Plannet Bongo.

Moja ya mambo mazuri aliyosema ni “Mwaka huu narudi rasmi kwenye kazi yangu ya muziki na tayari nimesharekodi imebaki verse ya Mr Blue tu, ukweli kazi hii itakuwa moto moto maana kaka amekutana na mdogo wake “ Kwa maneno haya ni wazi ameonyesha utofauti kwamba sasa ni kufanya kazi zaidi na si mengine.

Wengi walionekana kushangazwa na picha ambayo ilisambaa ikimuonesha Chid Benz akiwa katika studio hizo, lakini ni kawaida kwa kila radio kumpiga picha msanii na kupost katika mitandao ya kijamii. Mara nyingi post hiyo huonyesha kama yupo katika kituo husika. Katika uhalisia ni picha ilionyesha utofauti wa mabadiliko makubwa ya muonekano wa Chid Benz si kama wengi walivyomzoea.

Wengi walimcheka na hata kumdhihaki Chid Benz, lakini sishangai kwa mashabiki ambapo wengi huwa wakicomment mambo mengi ambayo hayana msingi ila huwa imradi tu aonekane amecomment, bila kujali maneno anayoyatumia kama yana jenga au yanabomoa.

Ila nashangwa na mtu kama Soudy Brown ambaye ni mtangazaji wa kituo kikubwa anapokuwa mastari wa mbele katika kumdhihaki Chid Benz, kwa nguvu aliyonayo/walionayo wana uwezo mkubwa wa kumsaidia.

Unapost hivi ila siku hakiwa hayupo katika uso wa dunia mtakuwa wa kwanza kushikiria bango kujifanya mnamsifia zaidi, haileti maana kumpost hivi maana alitoa wimbo wala hukusuppot sio fair” Maneno ya shabiki mmoja kati ya wale wengi waliocoment katika post hiyo.

“Breaking News Ilalaaaa unayemuona hapo sio fidodido ni rapper Chuma Chid Benz ameamua kupunguza uzito ili aweze kwenda sawa na wakati kwasababu kitambi kilikuwa kinamkata pumzi anapokuwa stejini sembenoma usifuatemkumbo”

Hii post ya Soudy Brown ambayo iliambata na picha Chid Benz.

Ni wazi kwa meneno yake amemletea dhihaka Chid Benz, kitu ambacho hakileti maana katika jamii. Hii ni sababu moja wapo ya kusema Tusimcheke wala Tusimdhihaki Chid Benz. Wakati alionao ni mgumu hivyo ukaribu na maneno yenye faraja ndiyo pekee yanayoweza kumsaidia na kurudi katika maisha yake ya kawaida.

Unadhani kumcheka na kumdhihaki kutamsaidia? Ili kuepukana na tatizo lazima watu wawe nae karibu sio kuleta maneno yenye kumvunja moyo zaidi.Ila maneno yenye maana na kujenga ndiyo dawa ya mtu kuacha mambo yaliyo mabaya.

Ray C alikuwa mtu wa kwanza kulalamika kuhusu dhihaka na kebehi anazopata toka wa watu wa magazeti ya udaku, ambapo alisema “Unaponiandika navuta unga ni wazi unazidi kunichafulia hata mtu akaitaka kunisaidia kwa kitu anasema mtu mwenyewe bado anatumia”

Ifike wakati watu wa media mfahamu nafasi mlizonazo ni kubwa na kuna watu wanapata taarifa kupitia nyinyi, hivyo mnapaswa kuwa katika mlengo wa kujenga zaidi, sitaacha kusema jamii inahitaji mambo ya msingi zaidi sio umbea pekee ambao mwisho wa siku hauna faida yoyote katika maendeleo.

Nafikiria kwa undani zaidi kipi kimemfanya apost na aandike dhihaka? Wapo wanaosema watu wanapenda coment nyingi hasa katika mtandao wa picha, Hivi hizi comment nyingi zinawasaidia nini? Ni vyema kuchukua muda wa kujenga zaidi na sio kubomoa.

Nani hajui kipaji cha Chid Benz, ni moja katia wasanii waliokuwa starter ya wasanii wengi, kuna wakati ilikuwa ila msanii mchanga atoke lazima afanye kazi na Chid Benz. Lakini pia alikuwa kinara katika muziki wa hiphop na hata kuwa msanii wa kwanza kuanzia Tv show hivyo ni msanii mwenye uwezo mkubwa.

Tusimvunje moyo ila tumjenge ajione ni muhimu katika muziki huu, kejeli na dhihaka haziwezi kumsaidia bali kumpoteza zaidi, wenye nafasi za kusikika, na watu husika ni vyema kuzungumza na wenye msaada zaidi na sio muda mwingi kutumia mitandao ya kijamii kwa kutoa kashfa tu, ilihali muonekane katika mlengo wa umbea. Kuna mengi ya kujenga zaidi, jamii bado inahitaji mambo mengi ya msingi si umbea kama wengi wafikiriavyo.

 

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez