Tafakari kuu ya kukosa album kwenye muziki kizazi kipya.

jumanature

Tafakari kuu ya kukosa album kwenye muziki kizazi kipya.

Malalamiko sio njia ya kutatua tatizo, bali tatizo hutatuliwa kwa kutazama chanzo cha tatizo na jinsi gani unaweza kuliweka sawa lisiwe tatizo tena au hata kulipatia unafuu kama sio usumbuzi.

Muziki wa kizazi kipya ni muziki unaochezwa zaidi katika vyombo vya habari hapa nchini, na hili halina ubishi maana tumeona malalamiko mengi kutoka kwenye aina nyingine ya muziki kama bolingo, taarabu na rege kuwa ni wazi muziki wa kizazi kipya unapendelewa katika vyombo vya habari.

Ni mwaka 2010 msanii Ambwene Yesaya maarufu kama A.Y ndiye aliyekuwa msanii wa kwanza kutangaza kuto kutoa album katika soko la muziki wa kizazi kipya. Hakika alikuwa na hoja zenye mashiko, na haikuwa na ugumu kwangu kupinga kile alichokisema kuhusu changamoto za mauzo ya album.

Ni mwaka 2011 tukaona wasanii walio wengi nao wakifuata nyayo za A.Y juu ya maamuzi ya kuachana na mauzo ya album. Lakini hapa wapo chipukizi wengi walioibuka mwaka 2011 ambao ni wazi walifuata mkumbo bila hata kujua nini ni nini. Pia ni wazi wameendelea kubaki chipukizi maana ni wazi hawana album. Album ni njia moja wapo ya kuonyesha ukubwa wa msanii.

Ni wazi mimi ni mmoja wa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya, hivyo ni wazi sasa tumekosa mambo mengi mazuri ikiwemo la album. Pengine wengi wetu hatufahamu kuwa ili uweze kutatua tatizo ni lazima ufahamu chanzo chake. Hii ndio maana hata ukienda hospitali lazima upatiwe vipimo ndiyo matibabu yafuate.

Hakika kuna mambo sita (6) yanafanya tunakosa album katika muziki wetu mzuri wa kizazi kipya yani Bongo Fleva/Hiphop.

Msambazaji, huyu ni mtu wa kwanza ambaye anachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza muelekeo wa muziki, maana ni wazi malalamiko mengi yamekuja kwake. Ni wazi msambazaji amekuwa sio mwaminifu pia kuto kutoa hesabu zisizo eleweka.Mfano msanii fulani ameuza kopi kadhaa, hili ni jambo lisilosemwa kabisa hivyo wasanii waliowengi wamekosa imani.

Wasanii, huyu ni mhusika mkuu katika hili. Maana wasanii wengi wa sasa wamekuwa wakitamani pesa za haraka haraka, na kweli wanazipata kupitia matumbiuzo yao wanayofanya. Na kutokana wanapata pesa kupitia nyimbo zao ambazo hupigwa kwenye vyombo vya habari basi ni wazi hawaoni tena umuhimu wa kuwa na album. Maana hata Abdu Kiba ameeleza katika kipindi cha Ladha 3600 kuwa “Kama wimbo mmoja unaweza kunipa pesa nyingi nifanye album ya nini”

Washika dau, hawa ni watu ambao hujiweka kama nguzo ya msanii. Ambao ni wazi hawa ndio husababisha anguko la wasanii waliowengi. Ni watu wenye kukwamisha mambo mengi mazuri, ila cha ajabu wasanii ni kama wametiwa upofu mbele ya mtu anaeitwa mdau. Maana wapo pia wanaomwita mdau” baba wa muziki” hiki ni kichekesho kabisa. Lakini washika dau ndio watu wakubwa wanaozuia mambo yote kuhusu album maana ni wazi msanii atafaidika bila kumuhusisha. Na mdau kugundua hilo ni wazi anatumia akili ya ziada ili kudidimiza hili.

Vyombo vya habari, inashangaza kuona vyombo vya habari kuhubiri album haiuzi lakini kwanini hawasemi njia za wasanii kufanya ili waweze kuuza? Pia ni wazi hata kama msanii akifanya album hawana muda wa kumzungumzia zaidi ya kusema tu album haiuzi. Wapo wasanii walioamua kuuza wenyewe miaka kadhaa nyuma, ila baadhi ya watangazaji walisema “Ataweza wapi yule atatembea mpaka basi” Sasa hapa inanipa mashaka juu ya vyombo vya habari wapo kwajili ya kukosoa? Nilitegemea kuona hata wakitoa mialiko kadhaa ya watu wenye ufahamu juu ya mambo ya masoko ili waeleze jinsi ya kukomboa hili, ila naona vyombo vya habari vingi vipo kwaajili ya kuwavunja mioyo wasanii.Pia kufuata kile ambacho wao wanataka kiwe au wanachokuaminisha

Tuzo, hili halina kificho wapo wasanii ambao wanafanya kitu kwaajili ya tuzo. Hivyo wengi wao walivyoona hata katika tuzo za KTMA hakuna tena kipengele cha album bora wakaona ni wazi haina maana tena ya album. Wala hainipi shida kusema wengi wanaosimamia tuzo za KTMA si watu wajuao muziki kiundani. Hivi tangu 2010 hakuna wasanii waliotoa album? Sasa kama wapo kwanini wao walifuta kile kipengele?

Wateja, ni wazi uzalendo ulipotea kwa kiasi kikubwa. Mashabiki wengi wa sasa si watu wa kununua kazi za wasanii bali hupenda bure kuzipata ila ni mabingwa wa kutukana katika mitandao ya kijamii kuwa fulana hana hela wakati ni wazi kazi yake hununui hata kwa bahati mbaya.

Hakika kama tunataka kupata album katika muziki wa kizazi kipya ni vyema kuyatazama haya machache yenye kubomoa muziki wetu mzuri.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez