Sioni msaada kwa Ray C naona udhalilishaji

index

Sioni msaada kwa Ray C naona udhalilishaji

Rehema Chalamila ni jina lake kamili lakini anafahamika zaidi kwa jina la Ray C, ambaye ni mzaliwa wa Iringa. Ni moja kati ya wasanii wa mwanzoni katika kukua na kueneza muziki wa kizazi kipya.

Huwezi kutaja wadada walichangia kukua na kueneza muziki huu wa kizazi kipya bila kumtaja Ray C. Ni moja kati ya wasanii ambao wamefanya matumbuizo mengi nje ya nchi katika miaka ya kung’aa kwa nyota yake kwenye muziki.

Ni wazi maisha yana mambo mengi, hakuna aliyeamini anguko la Ray C kimuziki. Anguko hili lilikuja baada ya kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, ambapo ni wazi Rais mstaafu Mh Jakaya Kikwete alijitolea katika swala zima la matibabu.

Wakati wa matibabu hakika alikua vyema na hata kuona mabadiliko. Ni katika kipindi cha Planet Bongo cha EATV ambapo alipata wasaa mzuri wa kuzungumza mengi. Moja kati ya mengi ilikuwa ni “Inaniuma kuona watu bado wananisingizia uongo, haswa magazeti ya udaku. Naona ni jinsi gani wananikandamiza zaidi”

Hizo zilikuwa ni lawama zake juu ya magazeti ambayo yalikuwa yalikendelea kumchafua zaidi lakini wakati huo hakika alikuwa ni mwenye afya njema na hata kurudi studio na kurekodi baadhi ya nyimbo.

Maneno kwenye mtandao wa picha “Instagram” juu ya Ray C yamekuwa mengi zaidi, ila kama haitoshi hata video inayomuonyesha katika gari la polisi imeweza kutawala katika mtandao huo.

“Hakuna video zinaleta followers kama hizi za kiki” ni baada ya kumuuliza mmoja aliyeweka video ya Ray C katika mtandao wa picha Instagram.

Ni wazi watu wanatumia matatizo haya ya Ray C wapate kiki na followers, lakini je hayo mambo yanakusaidia nini katika maisha yako? . Tunajua tupo kwenye kizazi cha teknolojia lakini hakika swala la video za udhalilishaji kama hizi si jambo jema.

Inashangaza kuona mtu ameandika waraka mkubwa kwenye mtandao wa picha huku akitaka mtu fulani amsaidie Ray C. Nafikiri juu ya uelewa wa huyu mtu ni mdogo kiasi gani? Je hakuwa na uwezo wa kupata namba ya simu ya huyo mtu aliyetaka ampe msaada Ray C? sasa ameweka posti katika mtandao wa kijamii ili iweje?.Bali isipokuwa ni ufinyu wa mawazo mapana.

Ni wazi ni mtu aliyetaka kuonekana zaidi si kama analo lengo la kumsaidi Ray C. Je angekuwa ni dada yake wa damu angeweza kuandika kwenye mtandao? Nafikiri angetumia njia sahihi ya kumtafuta huyo mtu anaemini anaweza kumsaidia bila hata kuhusisha mtandao wa picha.

Naona wengi bado wanaendelea kupost video ya Ray C,  hakika sioni msaada juu yake bali udhalilishaji wa kiwango cha juu. Inabidi ujiulize katika nafsi yako je ukiweka video hiyo mtandaoni inakusaidia nini?

Lakini pia ujumbe umefika jinsi ambavyo Ray C yupo sasa, hivyo ni vyema kuchukua nafasi hii kwa wahusika na wadau ambao wana uwezo wa kumsaidia hili waweze kumpa msaada unaostahili. Tusihesabu amesaidiwa mara ngapi, isipokuwa ni vyema kuhakikisha kama anarejea vyema katika afya yake njema.

Tujifunze kuishi kwa kutafakari si kila kitu lazima kihusishe mitandao ya kijamii.

Mungu mbariki Ray C na pia mrudishie maisha yake.

HIVI NDIVYO JINSI TEKNOLOJIA INAVYOPIGA TAFU MZIKI WETU

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez