Sababu za kutokuongezeka kwa idadi watazamaji (views) Youtube

Kutokuongezeka kwa idadi watazamaji katika video mpya ya msanii Ali Kiba (Mvumo wa Radi) kumezua taharuki miongoni mwa mashabiki na wapenzi wa muziki nchini. Lakini ikumbukwe hii sio mara ya kwanza kutokea kwa wasanii wetu, msanii Baraka Da Prince amekuwa akililalamikia swala hili mara kadhaa. Mpaka kufikia hatua ya kutangaza zawadi kwa mtu atakaye mbaini anayemfanyia fitina hiyo. Baraka aliamini kabisa kuwa kuna mtu anayemfanyia uhuni katika video zake.

Youtube ni mtandao ambao upo makini katika kuwatendea haki watengenezaji wa video, watazamaji pamoja na watu au chapa zinazotumia mtandao huo kuweka matangazo yao ya biashara. Ndio maana imeweka juhudi za makusudi katika kuhakikisha pande zote hizi tatu zinaridhika na kunufaika na matandao huu.

Youtube inatumia program za kompyuta (algorithm) kubaini watazamaji wa ukweli na bandia watokanao na program za kompyuta katika video zote zinazowekwa.  Kama inavyoeleza picha kutoka katika ukurasa wao wa msaada kwa watumiaji.

 

Tunataka kuhakikisha video zinatazamwa na wanadamu sio programu za kompyuta. Katika masaa ya kwanza baada ya video kuwekwa, tutaonesha watazamaji ambao mfumo wetu utaamini kuwa ni halisi. Na kwa wakati huo tunaweza tusioneshe idadi yote ya watazamaji. Baada ya watazamaji halisi kuhesabiwa, idadi ya watazamaji itakuwa ikiongezeka mara kwa mara. Mchakato wa kukusanya watazamaji wote unachukua muda kwa kuzingatia umaarufu na umiliki wa video husika. Pamoja ya kuwa na ongezeko la mara kwa mara la idadi ya watazamaji, zingatia kuwa tunataendelea kufanya upembuzi wa watazamaji, hivyo basi idadi ya watazamaji wako itakuwa ikibadilika. Imeeleza taarifa hii

Hili linaweza kuwa jibu kwa baadhi ya maswali ambayo yamekuwa yakijitokeza kuhusu kutoongezeka kwa idadi ya watazamaji kwenye baadhi ya video za wasanii wetu. Kwa kawaida kabisa Youtube huanza mchakato huu video inapofikisha watazamaji 301.

Nini kinasababisha watazamaji kutokuongezeka katika video? Ukurasa wa msaada wa kwa watumiaji wa Youtube umeweka bayana.

Wakati mwingine kunaweza kusiwe na ongezeko la idadi ya watazamaji katika baadhi ya video, au video kutoonesha idadi ya watazamaji uliyokuwa ikitarajiwa. Watazamaji wanapembuliwa kwa kutumia programu za kompyuta (algorithm) ili kuhakikisha haki inatendeka kwa watengenezaji, watangazaji na watumiaji wa Youtube. Ili kuhakikisha kama video yako ina watazamaji halisi, Youtube itapunguza kasi ya ongezeko la watazamaji au kuto ongeza kabisa idadi ya watazamaji kwa muda, lakini pia itafuta watazamaji ambao walitazama kwa kurudia rudia kwa mazumuni ya kuongeza idadi ya watazamaji. Imeeleza taarifa hii.

Nini kinawakuta wasanii wetu? Awali ilikuwa kwa Baraka Da Prince, lakini sasa imedondokea kwa Ali Kiba. Pamoja na kutumia mitandao mingine kutangaza video zao ili kuongeza idadi ya watazamaji (ambapo ndio njia salama ya kukuza chapa ya msanii na kuongeza idadi ya watazamaji). Lakini pia kumezuka tabia ya kuwa na timu ambazo hatuna uhakika kama zinatumwa na wahusika au ni mahaba waliyonayo kwa msanii husika. Timu hizi zimekuwa na tabia ya kutazama video mara nyingi wakiamini wanamsaidia msanii husika kuongeza idadi ya watazamaji wake Youtube.

Kinachotokea, kundi hili likishakuwa kubwa progamu ya kusimamia uhalisia wa watazamaji inagundua huo udanganyifu na kulazimika kuanza kufanya upembuzi yakinifu kwa idadi yote ya watazamaji wa video husika. Hapo ndipo kunakuwa na kutokuongezeka kwa idadi ya watazamaji mpaka mfumo wa Youtube ujiridhishe kuwa hakuna udanganyifu. Na mchakato huu unachukua muda hivyo kusababisha taharuki kwa wahusika.

Endapo Youtube itagundua udangayifu matokeo yake  huwa mabaya zaidi, ambayo yanapelekea video husika kufutwa au chaneli ya msanii husika kufungwa kama itaonekana kuwa na tabia hiyo mara kwa mara.

Ushauri, tusitazame video kwa ushabiki ili kuongeza idadi ya watazamaji. Hii inaathiri hadhi ya msanii ndani na nje ya mtandao wa Youtube. Epuka kurudia rudia kutazama video kwa madhuni hayo hayo ya kuongeza watazamaji. Fuata kiunga http://bit.ly/2GidnVo kusoma Zaidi kuhusu sababu za kutokuongezeka kwa idadi ya watazamaji.