Ruby amejitafakari, ilihali Clouds Media Group ni vyema kujitathimini.

Ruby amejitafakari ilihali Clouds Media Group ni vyema kujitathimini.

Waswahili husema “Kama wote twajenga nyumba moja ya nini tugombee fito” Kwa hakika hakukuwa na sababu za Ruby kuendeleza tofauti zake na Clouds Media Group ilihali wote wanajenga nyumba moja ya muziki.

Ni faraja kwetu na wapenzi muziki wa Ruby kumaliza tofauti zake na Clouds Media Group. Ambapo ugomvi wao ulianza pale ambapo Ruby alieleza yakuwa hakuna maslahi katika tumbuizo la fiesta alilopaswa kushiriki mwaka 2016.

Na baada ya hapo ndipo Clouds Media Group walipoamua kuzima habari zote za Ruby katika kituo chao.

Bila kificho jambo hili halikuwa baya kwa Clouds Media Group bali kwa mwadada Ruby. Maana siku baada ya siku ndivyo ambavyo alikuwa akishuka kimuziki.

Ni wazi Media nyingine ziliendelea kucheza nyimbo zake lakini kwa uhakika hakuweza kunufaika kama ambavyo ilikuwa awali wakati yupo Clouds Media Group.

Maneno ni mengi kutoka kwa mashabiki na wadau wa muziki kwenda kwa Ruby, wapo wasemao amekosea kuomba msamaha na wapo wasemao ni sawa kuomba msamaha

Ni wazi hakukosea kuomba msamaha bali amefanikiwa Zaidi. Hakuna jambo jema kama kujitafakari ulipokuwa na ulipo sasa. Daima sisi hupenda kuhubiri ukweli, ni wazi bila kurudi Clouds ni kipaji cha Ruby kingepotea ilihali ni kipaji kikubwa mno.

Yafaa watu wajue katika muziki wetu kipaji pekee hakitoshi bali  matangazo ya wakati wote.

Nguvu ya matangazo aliyokuwa anapewa na Clouds ni wazi hakuweza kuipata mahala pengine na hii ni kutokana na Media nyingi kukosa ubunifu wa namna ya kumuinua msanii.

Katika ile kweli Clouds kama wakiwa na msanii ambaye wanataka awe mkubwa basi tegemea kumsikia/kumuona katika matamasha yao yote ambayo watafanya lakini kumzungumzia vyema katika vipindi vyote.

Media nyingi za Tanzania hujiweka upande wa msanii mara tu msanii anapokuwa ametofautina na Clouds ilihali katika vipindi vyao hawampi muda wa kutosha na hata wakianda matamasha yao watachukue wale wale ambao kila leo wanasikika Clouds, Je!kuna haja ya Ruby kuendeleza tofauti zake ikiwa hazimleti walau mkate mdogo?

Ruby amejiafakari vyema na kwa hakika ni maamuzi mema ya kurudi Clouds maana hata waswahili husema “Ng’ombe akivunjika mguu marishoni hurejea zizini”

Lakini Clouds wanapaswa kujua yakuwa “Mtu mzima akivuliwa nguo huchutama” ni wakati mzuri wa kujitathimini juu ya tofauti zao na wasanii mara kwa mara.

 

#TuzungumzeMuziki

Follow Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Tuachie maoni yako hapa