Ray C alikuja kwa msukumo wa uwepo wa Lady jaydee, mwisho akapotea kwa msukumo wa madawa ya kulevya.

Ray C alikuja kwa msukumo wa uwepo wa Lady jaydee, mwisho akapotea kwa msukumo wa madawa ya kulevya.

‘Lakini Jide hapati anachostahili’
Alikuwa mwanamuziki akawa mtangazaji akawa mwanamuziki. Ni mwanamuziki mjasiriamali sasa. Katikati ya masela. Katikati ya machizi muziki. Katikati ya mfumo dume akatoboa. Haikuwa kazi rahisi. Katika wakati wake ilikuwa ngumu sana mwanamuziki wa kuimba akafanikiwa kuteka watu. Achilia mbali mtoto wa kike.
Toto hili la Kikurya likapasua.
Sawa alisaidiwa lakini huwezi kusadia mtu asiyejiweza akaweza. Huwezi kuwekeza sehemu ya kupata hasara.
Waliomsaidia walikuwa wanasaidia sehemu sahihi ya kupata faida.
Kama unaweza kumsaidia asiyeweza akaweza basi wangewasaidia dada zao nao wakaimba.
Hakuna mjinga wa kutupa pesa.
Katika ubora wao kina Sugu, Jay na kina Nature naye Jide alikuwa katika ubora wake.
Sauti yake imetumika sana kupamba nyimbo zao katika viitikio.
Alipambana kuteka soko katika dimbwi la wanamuziki wengi wa kiume. Akafanikiwa. Kwa miaka mingi kwenye muziki alitumia kupambana na soko la muziki. Pia alitumia muda mwingi kulilia mapenzi.
Wako wapi kina Stara na wenzao kama Unique Sister. Achana na Ray C ambaye alikuja kwa msukumo wa uwepo wa Jide. Lakini mwisho akatoweka kwa msukumo wa dawa za kulevya.
Kwa kusikiliza tungo zake mpaka Ndindindi ya juzi unagundua kuwa Jide katendwa na mapenzi kwa miaka mingi kuliko waliotendwa na dawa za kulevya.
Kikazi kibiashara na kimaisha athari za kutendwa kimapenzi hazina tofauti sana na athari za dawa za kulevya.
Hakuna alichobakisha Jide kwenye muziki ila kuna kitu muziki umebakisha kwa Jide. Heshima.
Jide anastahili heshima. Bahati mbaya Wabongo tulishatoa talaka ya heshima. Hatuna heshima panapostahili heshima.
Wanamuziki wengi sana wa kike na wa kiume wametoweka kwenye muziki. Jide bado yupo na misukosuko yake. Anakomaa kivyake. Mambo mengine tuache kusubiri mtu atangulie mbele ya haki ndipo tuangushe mamilioni ya sifa. Kama vijana wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya ugumu wa maisha. Jide tungeshamzika kwa matumizi ya dawa za kulevya kwa ugumu wa mapenzi.
Jide ana akili, ugumu wa penzi la ukweli alilokosa akageuza pesa. Stress za mapenzi zikatunga msululu wa pesa kwenye akaunti yake. Mr Nice hakukosea katika maisha yake. Kufulia kwake ilikuwa makusudi ya Mungu ili kuwasaidia kina Diamond ambao leo wanakumbuka kuwekeza. Bila mfano wa Nice hata Diamond huenda asingekuwa na makazi Madale.
Jide uwepo wake ni makusudi ya Mungu ili kina Linnah na kina Mwasiti wajue kuwa muziki ni maisha siyo lazima uwe na ajira nzuri kama Mwamvita Makamba.
Vijana wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya ugumu wa maisha. Wanajiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya kwa sababu ya tamaa ya maisha mzuri. Jide ugumu wa maisha anaumalizia kwenye mashairi. Ugumu wa mapenzi anaugeuza pesa.
Jide anastahili heshima kubwa zaidi ya kuitwa Komandoo.

Imeandikwa na Dk levy.

Follow Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Youtube Tizneez

Tuachie maoni yako hapa

Attachment