Mwenye Nacho Huongezewa

Mwenye nacho huongezewa, asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho ananyang’anywa. Nazidi kuijengea hoja imara kauli hii ambayo awali niliona kama ni propaganda zisizo na ukweli. Lakini nilikuja kuamini baada ya kusikiliza simulizi hii ya kuhuzunisha kidogo iliyojawa na usaliti.

Alikuwako kijana mmoja, shupavu na mwenye haiba nzuri machoni mwa watu. Watu walimpenda kutokana na jitihada zake, na mabinti pia walipenda haiba nzuri iliyofanywa na mwonekano wa ngozi yake.

Ikafika siku huyu kijana alitaka kuoa mke, hivyo akatafuta familia iliyosifika kwa mabinti warembo na wenye tabia njema. Kutoka katika familia hiyo alibahatika kumpata binti mrembo UHURU.  Hakika uhuru alikuwa ni binti aliyevutia kwa umbo na hata sura.

Ikafika siku kijana anaenda kuchukua jiko, ndipo aliamua kuambatana na rafiki yake wa muda mrefu. Ambaye kwa hakika urafiki wao ulikuwa “Sugu” kwa jinsi walivyoshibana. Kutokana na uzoefu alionao rafiki yake huyu aliona utakuwa msaada mkubwa kwake katika kufanikisha lengo lake kwa Uhuru.

Kikulacho kinguoni mwako, ndicho kilichomtokea kijana huyu ambaye alitumia muda wake mwingi mpaka kumpata Uhuru. Lakini usilolijua ni usiku wa giza, kumbe rafiki yake aliamua kuacha kuuenzi urafiki wao uliogeuka kuwa Sugu kwa sababu ya Uhuru. Pepo la tamaa na kiu hatimaye vikamuingia. Akafanya kila hila ilikumpata Uhuru. Hatimaye uhuru aliokuwa anautaka sasa ameupata, lakini uhuru huu sio ule uliokuja kwa juu ya meza na majadiliano, Uhuru huu ameupata kwa mabavu na hila.

Mpaka hadithi inafika tamati hatujapata kufahamu nini chanzo cha baba mkwe kumuoza Uhuru kwa mara ya pili tena kwa watu wanaofahamiana. Lakini ndio ishakuwa tuendelea kushughulisha akili zetu katika hili. Je ni kwamba jamaa katoa posa nyingi Zaidi au baba mkwe ameamua kumuozesha Uhuru kwa huyu bwana ili kulinda urafiki wao wa muda mrefu? Yote mawili yanawezekana.

Mimi ningependa kumalizia kwa kukumbuka ule msemo usemao “Mpanda ngazi, hushuka.”