Muziki biashara na biashara ya muziki changanyo kuu kwa Izzo Bizness.

Muziki biashara na biashara ya muziki changanyo kuu kwa Izzo Bizness.

Myumbisho ni mwingi kutoka kwa msanii Izzo Bizness, hasa katika wimbo wake wa sasa wa Rimoti. Na tunaona namna ambavyo anatumia nguvu kubwa katika mtandao kwa maana ya kuutangaza vyema, ni jambo zuri.

Na katika mahojiano mengi afanyayo amekuwa akisema “Ni wimbo flani hivi wa kusakata rhumba, unaweza usielewe lakini kwenye masherehe sherehe hivi utaelewa”

Sisi tunaheshimu kila aina ya muziki kutoka kwa Izzo Bizness na tunaheshimu kwa sababu tunajua yakuwa ‘Muziki ni hisia za ndani ya msanii’.

Lakini changanyo kuu kwa Izzo ni Muziki biashara na biashara ya muziki.

Muziki biashara kwa hakika na kwa wasanii wote, na hakuna muziki usiokuwa biashara kama utapewa matangazo makubwa, uhalisi ni kwa Makhiriri, hivi walikuwa wanaimba nini? lakini nguvu ya matangazo ikafanya wakauza muziki wao.

Katika taswira kubwa inatuonyesha namna ya Izzo anavyopambana kutoa makapuka kwa kuwaza muziki biashara.

Hakuna haja ya kulazimisha makapuka hayo maana muziki wowote ule ni biashara ingawaje ni kuufanya kwa kiwango cha juu na kuupa matangazo.

Nguvu hii itumikayo kwenye wimbo wa rimoti kama angetumia kwenye wimbo wa Rafiki na Tusiwatese hakika angeelewa vyema upana wa muziki biashara.

Lakini kwanini ayumbishwe na Biashara ya muziki? katika uwazi biashara inahitaji matangazo mema ya nyakati nyingi.

Nani anamwambia Izzo kuwa muziki wake kama Utarudishwa Mbeya, Ridhi One, Bizness, Rafiki, Dangerous Boy, na nyingine nyingi kuwa si biashara?

Ni wazi anampotosha vyema tena katika hali ya kumpeleka shimoni.

Mabadiliko haya ya kimuziki hayafanani na Izzo kabisa bali kumfanya ashuke kimuziki. Na watu wanapaswa kujua yakuwa kufanya aina nyingine ya muziki si dhambi bali dhambi ni kufanya chini ya kiwango.

Maana sanaa ya muziki ni pana mno, hivyo hupaswi kuweka mipaka juu ya msanii kufanya aina nyingine ya muziki. Lakini je! anafanya kwa kiwango cha juu?

Ni wazi makapuka haya afanyayo Izzo katika kweli yenye kweli anafanya chini ya kiwango hivyo anazidi kujishusha kimuziki.

Ambacho anapaswa kujua ni namna ya yeye kuitangaza kazi yake kwa ukubwa nyakati ambazo amekuwa ametoa, mfano halisi ni wimbo wa Rafiki, hakuupa nguvu ya kuutangaza kabisa.

Izzo anakuwa bora kama anasimama katika njia yake kuu iliyomtoa (Hiphop) lakini kwenye makapuka ni wazi anadondoka vyema kisanaa, tena kwa hali ya wepesi mno.

Biashara ya muziki ni namna upangavyo katika mlengo wako, lakini muziki biashara ni vile ambavyo utaitangaza biashara hiyo, kimsingi ‘Hakuna muziki usiokuwa biashara’.

Kwa maana biashara yoyote inahitaji matangazo ili iweze kufikia vyema walaji. Hivyo Izzo abaki katika Hiphop na kusimamia matangazo vyema hakika atauza biashara yake hiyo.

#TuzungumzeMuziki