Muungwana akivuliwa nguo huchutama –Clouds Media Group.

images

Muungwana akivuliwa nguo huchutama –Clouds Media Group.

Huwezi kupinga mtaji wa wasikilizaji na watazamaji vijana walionao Clouds Media Group, hapa nazungumzia Clouds Fm na Clouds Tv.

Watu husema mti wenye kupigwa mawe ndio wenye matunda, lakini pia kuna haja ya kutafakari msemo huu kwa miaka hii. Ni ukweli mawe yamekuwa yakipigwa zaidi katika mti wa Clouds Media Group, lakini siachi kujiuliza kwanini kila siku ni wao tu?

Vita ya Clouds na msanii/wasanii haijaanza leo wala jana, ni miaka mingi ya nyuma tangu kuanza kuchangamka kwa muziki wa kizazi kipya. Lawama zimekuwa nyingi kutoka kwa wasanii kwenda kwa Clouds Media Group.

Wapo wasanii walioweza kusema hadharani na wapo wasanii ambao husema kwa mafumbo kwenye nyimbo zao, na hukataa kabisa kutoa uchambuzi wa maneno hayo wakati ukiwa unamuhoji. Lakini wapo wasanii ambao waliamua kusema hadharani bila kujali, maana hofu kubwa iliyopo katika mioyo ya wasanii wengi kama ikitokea umeisema vibaya Clouds basi hakika utakuwa umejichimbia kaburi la muziki wako.

Hoja hii huitoa wasanii wengi ambao huwa ni wenye malalamiko kwenye mioyo yao. Ambao mimi huwaona kama ni watu wenye fikra ndogo na unafiki ndani yao, maana leo analalamika na kesho unamsikia akisifu kituo hicho kuwa ndio kimebadilsiha maisha yake kwa 100%. Hapa huwa nasema ogopa mtu anaeitwa msanii.

Ni mwaka 2001-2002 ambapo msanii Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II Sugu alikuwa ni msanii wa kwanza kueleza hisia zake juu ya Clouds Media Group ambapo ameandika katika kitabu chake cha “SUGU THE AUTO BIOGRAPHY Muziki na maisha,  From the street to the Parliament” katika sehemu ya 8 ukurasa namba 81, ameandika “Eti nisiwe na wasiwasi niende tu kwenye show kwani wangenipa pesa ambayo ningeitaka, kitu ambacho mpaka leo naamini kisingeweza kutokea kwani sidhani kama wamewahi kumlipa msanii pesa aliyotaka hata mara moja”

Swala la maslahi limekuwa ni wimbo wa taifa sasa kwa wasanii wengi, mwaka 2010-2012 tuliweza kuona vita kubwa kati ta Vinega na Clouds Media. Lugha kali ilitawala katika Mixtape za Ant Virus kuanzia Vlm 1 mpaka Vlm II. Vinega ilikuwa ni muunganiko wa wasanii zaidi ya 15 wa muziki wa kizazi kipya yani Bongo Fleva na Hiphop. Lakini kilio kikubwa katika Mixtape hizo ilikuwa ni swala zima la maslahi.

Baada ya vita hiyo mapatano yalitokea lakini kwa mtindo wa makundi matatu katika kundi hilo la Vinega. Ambapo kimsingi siwezi kuacha kuwasifu kwa kuwa watu wa kwanza kujitoa mhanga ili kuleta usawa katika muziki wa kizazi kipya.

Katika moja ya mahojiano ambayo niliwahi kufanya na D wa Maujanja mwaka 2014 alisema “Ilibidi tufanye vile mana umungu mtu ulizidi kwenye muziki, na Ant Virus imesaidia kuweka mambo sawa.”

Mapema jana Team Tizneez ilihabalisha jamii ya wapenda muziki wa kizazi kipya juu ya Ruby kutokuwepo katika jukwaa la Fiesta Mwanza. Ambapo Ruby aliongea kwa takribani dakika 6 na sekunde 10. Ila katika mazungumzo hayo alisisitiza swala zima la maslahi.

“Maslahi yamenifanya nisiende kwenye Fiesta” ambapo pia aliongeza kuwa “Show ni kubwa kuliko maslahi so naandaa vipi show yangu?”

Baada ya habari hiyo kila mtu alikuwa na maoni yake, wapo ambao walihoji mbona alionekana akisaini mkataba sasa kwanini hakugoma wakati anasaini? Wapo ambao wameona kama ni kiki, Lakini wapo ambao walikuwa wakiishutumu Tizneez kwanini tumeweka habari hiyo.

Jambo ambalo lilishangaza ni watu kuhoji kwanini tumeweka habari hiyo? Ni kwamba sisi ni watu ambao tunaandika kuhusu bongo fleva na hiphop tu, hivyo tuna kila sababu ya kuweka habari hiyo. Nadhani watu wangehoji kama tungeweka habari ya siasa lakini sio Ruby.

Pia sisi sio watu wa kupangiwa cha kuweka ndio maana husema tuko tofauti na blog nyingine ambazo ni wazi inaonesha hupangiwa cha kuweka kama sio kuogopa kusema ukweli uliopo.

Ikiwa wanasahau ukweli hauna rafiki wala ndugu, pia kwenye swala zima la uandishi ni vyema kusimama katika ile kweli sio kuwa mtu wa kuuma maneno kama sio sentensi.

Ni muda mchache ulipita pale ambapo Ruby aliamua kuweka kabisa video kwenye mtandao wa picha “Instagram”huku akiimba wimbo wa Lady Jaydee ambao ni Ndindindi, ambaye ni hasimu mkubwa sasa wa Clouds Media Group.

Hoja ni nyingi kwenye mitandao ya kijamii sasa, kila mtu ana mtazamo wake kwenye jambo hili.

Ni vyema Clouds kujitazama tena kama sio kutazama uongozi husika kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu. Kwanini kila siku malalamiko ya wasanii ni yale yale tu kuhusu maslahi?

Yamkini viongozi wa juu si wabaya ila hapa katikati ndio kuna zengwe, wengi wamekuwa wakitupa lawama kwa viongozi wa juu kabisa wa kampuni hiyo. Swala hili nalifananisha na “system ya kiserikali” huwa serikali inatoa misaada mingi kwa jamii husika ila ngazi ya chini ya mwisho hujinufaisha yenyewe bila kujali maslahi ya wananchi.

Lakini kama uongozi wa juu kabisa wa Clouds Media Group sio mbaya kwanini hawafanyii kazi malalamiko haya ya kila siku kutoka kwa wasanii, katika upande wa maslahi? Au hawasikii  malalamiko haya? Je wanayachukuliaje?

Katika moja ya kauli za Ruby alisema “Tunajikuta tunakuwa katika menejimenti ambazo zinajali umabavu zinaongoza wasanii kimabavu”

Lakini pia jamii ikumbuke Ruby ni zao la Clouds, na wamekuwa karibu katika kila kitu maana wao ndio walivumbua kipaji chake na kukiweka katika uso wa dunia (Kumtangaza) hivyo anachokisema Ruby ni wazi kipo na amekiona maana ni mwanafamilia halali wa Clouds.

Siku zinakwenda na jamii inazidi kuamini kuwa Clouds ni watu wasiojali maslahi ya wasanii bali yao wao. Hii ni kwa mujibu wa historia yao juu ya ugomvi na wasanii wengi kuhusu swala moja tu la maslahi.

Kuna kila sababu ya kuchutama kwa Clouds Media Group na kutazama tatizo liko wapi kama kweli viongozi wa juu hawahusiki, lakini hata kama wanajua ukweli uko wapi ni vyema kuchutama na kuanza upya ili kuweka picha nzuri katika jamii.

Bila kusahau hao wasanii wana mashabiki wao, ambao ni ngumu shabiki kubaki msikilizaji wa radio hiyo ilihali msanii wake amediliki kusema hana maslahi na show zao pia swala la kutopiga tena nyimbo za msanii ambaye hawako nae sawa kama Rama Dee, Lady Jaydee, Wagosi wa kaya, Dany Msimamo, Adili Chapakazi, G solo, Suma G na wengine wengi.

Tusiupinge ukweli katika maisha yetu, wote ni wasaka tonge kila mmoja apate anachostahili kwa nafasi yake.

Mungu ibariki Bongo fleva/hiphop./ Mungu ibariki Tizneez.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube Tizneez