Mtazamo wa Ay una maana kwenye muziki, ila ubinafsi wa wasanii ni kikwazo.

Mtazamo wa Ay una maana kwenye muziki, ila ubinafsi wa wasanii ni kikwazo.

Ni siku kadhaa zimepita tangu msanii Ambwene Yessaya maarufu kama Ay kutoa mtazamo wenye maana kubwa katika muziki huu wa kizazi kipya. (Bongo fleva/Hiphop)

Mtazamo wa Ay ni kuwa ‘wasanii watoe nafasi ya kusafiri na watayarishaji wa muziki wa kizazi kipya (Producers). Maana katika nafasi hizo au safari wataongeza wigo wa kujifunza zaidi katika kazi zao za utengenezaji wa muziki’

Ay hakuacha kutoa mifano kwa baadhi ya watayarishaji ambao kupitia safari ambazo walizifanya kwa juhudi zao wameweza kufanikiwa na kuendelea kuwa na kazi bora wakati wote. P Funk Majani ni mmoja kati ya wachache, ila pia yupo Nahreel, Hermy B, na Marco Charl

Huwezi kupinga mtazamo mzuri na wenye neema katika muziki wetu, ila katika uhalisia kundi kubwa la wasanii limetawaliwa na ubinafsi.

“Ukweli utakuweka huru” Na nina uhakika Ay  anajua tabia za wasanii  wa kizazi kipya wa hapa nchini Tanzania.

Sio jambo la aibu kwa msanii wa  bongo fleva/hiphop kurekodi wimbo bure na kwenda kufanya video ya pesa nyingi nje ya Tanzania. Na huko  akalipa pesa nyingi na hatoacha kusifu zaidi video bila kujali akili iliyotumika katika kuandaa chanzo.

Na pia ni kawaida kurekodi au kununua mdudo kwa mtayarishaji wa nje ya Tanzania na kulipia pesa nyingi na kwenye uhalisia mdundo ukawa ni wa kawaida mno, lakini msanii hatoacha kusifu uongo wake huo, ilihali hapa nchini huwa halipi kwa mtayarishaji ambae ameweza kufanya afike hapo alipofika.

Ukitazama maisha ya muziki kati ya msanii na mtayarishaji ni wazi maisha ya msanii yametawaliwa na umimi  zaidi. (Ubinafsi)

Kama wanashindwa kulipa muda wa studio je wasanii hawa wataweza kuwalipia watayarishaji gharama za kwenda nao kujifunza? Hili lingewezekana kama wasanii walio wengi wangetua chini mzigo wa ubinafsi

Kuna wakati huwa nawaza juu ya maisha ya watayarishaji wengi ambao wameshafanya kazi kubwa ambazo zimeweza kubadilisha maisha ya msanii pamoja na familia yake. Ila katika uhalisia ni msanii gani ambae anajali maisha ya mtayarishaji?

Wapo watayarishaji wakubwa ambao kupitia misimamo yao wameweza kufaidika, ila giza lipo kwa watayarishaji wengi wa  sasa ambao wamekuwa wakitumika bure kila leo.

Kikubwa cha kufanya kwa watayarishaji ni kuchukua mtazamo wa Ay kama ulivyo na kuutekeleza wao wenyewe na sio kusubiri msanii ndio akupeleke. Kama mtayarishaji utasubiri msanii hakika hautafika , maana wasanii wana maisha ya mazuri ya kisanii hivyo yapasa watayarishaji akili ziamke.

“Amka Mtayarishaji”

Follow Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Tuachie maoni yako hapa

Attachment