‘Mshale usiyo na nyoya hauendi mbali’ Babu Tale na Kalapina

index

‘Mshale usiyo na nyoya hauendi mbali’ Babu Tale na Kalapina

Wakati wa kwenda Sober kwa Chid Benz picha na video zilitawala katika mitandao ya kijamii hasa Instagram, picha na video hizo zilitoka kwa wahusika ambao walimpeleka katika moja ya Sober ambayo ipo wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Wahusika wakuu katika tukio hili alikuwa ni Babu Tale na Kalapina.

Ingawa mpaka leo sijawahi kujua maana ya kuweka video hizo na picha katika kurasa zao za mitandao ya kijamii. Lengo hasa lilikuwa nini? Na inasaidia nini kwa upande wa Chid Benz? Au walitaka kuonekana kama wanatoa msaada? Ila katika wimbo wa Sumu wa Fid Q amesema  “Humtangaza wakimpa msaada zaidi ya kumtia aibu”

Wiki chache baadaye picha na video ziliendelea huku wakieleza maendeleo yake katika mtandao wa Instagram na hata kufanya mahojiano katika vituo vya radio na runinga vichache.

Katika miezi michache mbele Chid Benz alitoka Sober, lakini katika uhalisia muda aliokaa hakika ni muda mdogo.

Na Mara baada ya kutoka Sober matangazo ya kurudi kwa Chid Benz kwenye muziki yalikuwa ni ya kiwango cha juu. Lakini ndani ya muda mchache yakapotea kama upepo uliopita. Jambo hili lilinifanya kuandika Makala ya Kurudi ghafla na kupotea ghafla kwa Chid Benz

Katika andiko hilo nilihoji mambo mengi ambayo uhalisia wake unaonekana sasa. Maneno aliyosema jana Kalapina imedhihirisha wazi “Sumu ya neno ni neno”.Ni wazi Babu Tale na Kalapina wamepishana katika maneno hii inaonyesha ni jinsi gani walikurupuka juu ya kumpeleka Chid Benz sober na hata kutoka kwake pia. Ukisoma hapa Makala ya Kurudi ghafla na kupotea ghafla kwa Chid Benz hakika utapata kunielewa zaidi.

Babu Tale alikuwa mtu wa kwanza kusema Chid Benz yuko sawa sasa na tegemea mazuri kutoka kwake, lakini pia alikuwa ni moja kati ya wengi ambao walikuwa wakiposti picha za Chid Benz ambazo zilionyesha kama akiwa amerudi katika hali ya kawaida. Ilihali katika ukweli na uwazi haikuwa hivyo. Bali jamii ililazimishwa kukubali uongo uliogeuzwa ukweli kupitia nyumba bora ya kutangaza fitna zaidi.

Ila maswali hayakuisha katika kichwa changu, mbona haraka imekuwa kubwa? Nini kifanya kuwa na haraka isiyo ya kawaida? Au kuna maslahi yanatakiwa kurudi baada ya kutoka Sober?

Mapema siku ya leo Kalapina hakusita kusema “Chidi Benz mwenyewe alikiri amepona na aondolewe Sober House, kama kweli karudia dawa bado jukumu letu ni kuhakikisha ameacha”

Hivi kweli hoja hii ni ya kusema mbele ya jamii? Je alikuwa sober kweli? Ni Sober gani muathirika anasema kama amepona na siyo mtaalamu ndiyo aseme kama muathirika amepona, hii inaleta picha gani? nini kimejifisha katika hili jambo?

Lakini wawili hawa walisahau kabisa kuwa “Mshale usiyo na nyoya hauendi mbali” Maana kama angekaa kwa muda stahiki hakika ingekuwa ni vigumu kurudi katika janga hilo. Ila wao haraka ya kutaka kupokea hongera kutoka kwa mashabiki ilikuwa kubwa kuliko kujali uzima ambao atakuwa nao kwa muda wote.

Swala la kuathirika na madawa ya kulevya ni jambo kubwa hivyo muathirika hutakiwa kukaa muda mrefu mbali na makundi ambayo yanaweza kumrudisha katika janga hilo. Hii ni kwa mujibu wa mtaalam wa tiba za madawa ya kulevya.

Ni wazi Chid Benz anahitaji kukaa zaidi ya muda aliokaa ili awe katika hali ambayo alikuwa nayo zamani na aweze kuendelea na shughuli zake za kimuziki. Na ambao wanajitoa kumsaidia ni vyema kutumia ustashi zaidi na akili za wataalamu sio kusimama pekee kama ilivyo.

Chid Benz ni msanii mzuri na wakipekee hivyo lazima watu watumie akili zaidi katika kumtoa alipo ili muziki wake ufike mbali.

Sentensi hii itumike katika kumkomboa swala lake la madawa ya kulevya “Mshale usiyo na nyoya hauendi mbali”

#TumshikeChidBenz. #ChidBenzJishike

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez