Miluzi mingi chanzo cha anguko la Mabeste

index

Miluzi mingi chanzo cha anguko la Mabeste
Muziki wa bongo fleva umeendelea kukua siku baada ya siku, ila katika kukua pia kumeendelea kutokea kwa anguko kama sio maanguko ya wasanii walio wengi wenye vipaji vya hali ya juu.
Si rahisi kuzungumzia wasanii wenye vipaji vya hali ya juu bila kutaja jina la Mabeste. Lakini pia huwezi kuzungumzia studio ambazo zimewahi kumiliki wasanii wenye vipaji vya hali ya juu bila kutaja Bhitz Record ikiongozwa na mtayarishaji bora Hermy B hakika huyu ni mtayarishaji asiye na maneno mengi isipokuwa vitendo. Ni mara chache kumsikia katika mahojiano, ukilinganisha na watayarishaji wengine.
Mabeste ni msanii aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wa “Baadae sana” ambao ulifanyika ndani ya studio za Bhitz. Hakika Pancho na Hermy B walifanya kile kinachotakiwa kufanywa ili tupate muziki mzuri wa wakati wote.
Umaarufu wa Mabeste uliendelea kukua siku baada ya siku hata pale walipokuwa wakifanya kazi na muunganiko wa wasanii wote ambao walikuwa wakiunganishwa na label hiyo ya Bhitz. Label ya Bhitz ilikuwa na wakali kama Mrap Lion, Vannesa, Gossy B,Deddy,na Mabeste. Lakini pia katika Bhitz alikuwepo Dj Choka ambaye mara nyingi sauti yake ilisikika katika nyimbo kadhaa za Bhitz crew.
Katika wasanii wote walikuwa Bhitz ni wazi na wala sio kificho jina la Mabeste lilikuwa jina linalotajwa zaidi katika vituo vya radio na runinga na hata katika vijiwe vya wapenda muziki wa kizazi kipya.
Ni wazi kama una sikio jema la kujua muziki mzuri huwezi kupinga ubora wa Mabeste wakati akifanya kazi ndani ya studio za Bhitz. Sikuwa msiri katika kusifia kuimarika kwa sanaa ya Mabeste ambapo ilikuwa inakuwa siku baada ya siku. Hakika ukafika wakati kila mmoja aliona Mabeste ni bora.
Lakini sanaa yetu ya muziki wa kizazi kipya yataka moyo. Maana wakati wewe unatumia kujenga wapo ambao wanafikiria namna ya kubomoa zaidi.
Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza hivi hawa ambao wamekuwa wapiga miluzi mizuri kwa wasanii wanajua muziki? Maana ni wazi wamekuwa wakivuruga mambo mengi ambayo kama yakiachwa yaendelee hakika kungekuwa na faida kubwa katika maisha yajayo. Wapiga miluzi wamekuwa hodari katika kulaghai wasanii walio wengi na kuwaingiza katika shimo na baadae kushindwa kutoka tena.
Kiuhalisia Mabeste anafanya juhudi nyingi kurudi katika mstari ambao alikuwa. Lakini binafsi sioni nguvu waliotumia wapiga miluzi katika kumtoa Bhitz, kutumia nguvu hiyo katika kumrudisha. Hakika hili halinipi maana yenye maana katika akili yangu, isipokuwa kutafakari ni kwanini wapiga miluzi hutumia nguvu nyingi kumtoa mtu sehemu ambayo watu huona kipaji chake?
“Hakika miluzi mingi hupoteza mbwa”. Moja ya mambo yanayowangusha vijana walio wengi ni kutokujua wapi ni mahali sahihi wao kuwepo na kufanya shughuli zao ambazo zitawaletea maendeleo.
Naamini katika kipaji cha Mabeste, naamini kufanya kwake vyema katika muziki wa kizazi kipya ni kuacha kusikiliza miluzi ya walio wengi, maana hao ndio chanzo cha anguko lake kimuziki.
www.tizneez.com
Twitter tizneez
Facebook tizneez
Instagram tizneez
Youtube tizneez