‘Media chanzo cha wasanii kuendeleza kiki’

‘Media chanzo cha wasanii kuendeleza kiki’

Muziki umekua hizi ni kauli za watu walio wengi juu ya muziki wa kizazi kipya. Kauli hizi wapo baadhi ambao wanapinga na kusema muziki haujakua ila ndio unakua.

Jambo jema la kujua ni kwamba huwezi kupingana na mtazamo wa mtu maana kila mtu ana maono yake. Ila ukitazama kwa undani yote yanaweza kuwa sawa maana kuna mambo mengi hayapo sawa lakini pia yapo mengi yaliyo sawa, Hivyo tunaweza kusema yote.  Ila haya mambo yanahitaji hoja pana na uwanja mpana wa kujadili juu ya jambo hilo.

Kumekuwa na tofauti kubwa ya utendaji wa muziki wa sasa na zamani miaka ya 2010 kurudi nyuma mpaka 1999.

Mwaka 2011 ndio mwaka ambao neno kiki lilianza, lakini mwaka 2013 ndiyo mwaka ambao neno hili lilichukua maisha mema katika muziki wa kizazi kipya.

Na sasa tunaona jinsi ambayo linaendelea kukua kila leo na mtoto kiki inaonekana sasa anaenda kuwa na nguvu njema katika muziki wa kizazi kipya.

“Daima shahidi ndiye mwenye neno” Hainipi shida kujua jinsi ambavyo mtoto kiki  anaendelea kukua kwa afya njema jinsi tu ambavyo mzazi wake anavyomtunza katika makuzi mazuri (Media)

Ni wazi mzazi wa kiki ni media, kuanzia ngazi zote yani Radio, Runinga, Blog, Magazeti (Media)

“Kuna kujua kuwa, na kujua jinsi” Neno hili linawapa tabu wengi bila maana wengi hawajui jinsi ambavyo kiki zinavyoboma muziki wa kizazi kipya.

“Kama unaujua ukweli halafu unaendelea kuishi kwenye uongo, basi ukweli huo utakuwa hauna maana” Binafsi siwezi kuishi kwa kukumbatia uongo ilihali ukweli ninaujua ulivyo.

Kiki zimebomoa mno muziki wa kizazi kipya yani Bongo Fleva/Hiphop ambao ulijengwa kwa misingi mikubwa ya kujadili muziki tu na sio upuuzi (kiki)

Imekuwa ni lazima msanii afanye jambo la kiki (Upuuzi) ili kuweza kupata kuzungumziwa katika Media. Kwa kuwa tu watangazaji na wachambuzi walio wengi wanataka kuzungumza Zaidi habari za kiki. Ukitizama kwa undani ni wazi ni watu wachache mno wa media ambao hawazungumzii habari za kiki.

Lakini nguvu yao ni ndogo maana kuna msemo unasema “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu” hivyo umoja wa wapenda kuzungumzia kiki ni mkubwa kuliko wapingaji.

Hoja ya kuzungumzia mitandao kuwa ndiyo chanzo cha kiki ni hoja ambayo nina ipinga bila kuyumbisha maneno. Ni wazi kurasa nyingi za udaku mara zote huandika mambo ambayo huyasikia kutoka kwenye Media.

Yupo moja ya mchambuzi mdogo ambaye aliwahi kuniambia “Huwezi kufanikiwa kwakuwa tu siandiki maandiko ya kiki juu ya watu Fulani” ingawa sina hakika na ufahamu wake maana sijui yeye anajua neno mafanikio ni nini, pia kipimo cha mafanikio ni kipi kwake.

“Hata kufa ni kuishi, ila ni kuishi katika kifo” Kiki zinaua huu muziki bila wajuaji kujua kuwa muziki unakufa shauri ya kiki.

Ziko wapi zile hoja za kuchambua kazi za wasanii kwa mlengo wa kujenga, ziko wapi zile hoja za kujadili kuwa album hii ni nzuri kwa upande huu au album hii ni bora mwaka huu?. Muda ambao wanatumia kujadili kiki ndiyo muda ambao tungeweza kujadili juu ya kurudisha muziki wetu kutoa album au mambo mema ya kujenga Zaidi.

Ila wengi wamesimama katika kuzungumzia kiki tu. Habari za kiki zinafanya tukose kujua nyimbo nyingi zilizotoka kwa wakati huo.

Lakini kama ‘Media’ zitaamua kuacha kuzungumza habari za kiki juu ya msanii husika hakika tutapata kuona ukubwa wa vipaji vya wasanii wengi. Na hapo ndipo kiki zitakapoisha kabisa katika muziki huu mzuri.

Kiuhalisia wapo wasanii wazuri ambao tunawakosa kuwasikia kwa kuzidiwa na nguvu ya kiki katika muziki.

Jambo la kiki katika upande wetu kama Tizneez Media Group ni wazi halina nafasi, hatuamini katika kiki ila tu muziki na kipaji cha msanii husika.

“Dhahabu ina thamani,  lakini haina maana katika kuishi Zaidi ya urembo”

 

 

Follow Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Youtube Tizneez

Tuachie maoni yako hapa