Lakini kwanini ukanda, fitna,na chuki katika muziki wa kizazi kipya?

images

Lakini kwanini ukanda, fitna,na chuki katika muziki wa kizazi kipya?

“Daima mwanzo wa ngoma ni lele” Lawama zimekuwa nyingi katika mambo mengi yanayoendelea katika muziki wa kizazi kipya yani Bongo fleva na hiphop.

Lakini kwanini wasanii hawasemi hadharani? Kwanini wanazungumza zaidi katika makundi ya WatApps? Bado wanahofu juu ya wao katika nafsi zao, lakini kwanini hawajiamini?. Lakini kwanini wana hofu ya kusema hadharani? Ni wazi wanaogopa kubaniwa kabisa. Lakini kwanini hawaamini wao wana nguvu kuliko mtangazaji na dj.

Ukanda upo kwa kiasi kikubwa, lakini kwanini ukanda umechukua nafasi katika muziki huu? Je umewahi kujiuliza mwisho wa upandeleo huu wa ukanda kutatokea nini?.Ni wazi wataanza kubaguana wao kwa wao, na ukabila kuchukua nafasi yake, kitu ambacho hatupaswi kuacha kusema kabla ya dhambi yake kuhukumu.

Naona waandishi wengi wa habari hizi za burudani na chambuzi kwa ujumla nao wamekua mabubu katika kusema hili swala. Lakini ni kwanini wamekuwa mabubu? Je! nao wapo kikanda? Ni ukweli usiopingika wapo kirafiki zaidi, na wameshindwa kutofautisha urafiki na kazi yao. Lakini kwanini wanachanganya urafaiki na kazi?

Haikuwa ngumu kwa mwandishi mmoja kuniambia “Jamaa mdau hawezi kukupa nafasi maana wewe upo na mambo mengi tofauti na yeye” Ni jambo la kushangaza. Lakini kwanini wanaandika kumfurahisha mdau?. Binasfi sipo kwaajili ya mdau, mdau wangu ni yule ambaye anasoma makala zangu na kupata elimu ikamsaidia katika shughuli zake za kila siku.

Kwanini ni mfurahishe mdau? Kwanini nisiandike ukweli utakaosaidia mambo mengi mazuri katika muziki wa kizazi kipya?. Je!Ni kwanini waandishi wana hofu kubwa na mdau? Pia siachi kujiuliza kwanini mdau hapendi kukosolewa? Kwanini anaamini katika mawazo yake tu?. Hili halina kificho mdau/wadau wamekuta muziki umeshaanza lakini inashangaza baadhi ya wasanii kuamini hakuna muziki bila mdau. Hivi kwanini wanaamini hivyo?. Kwanini wanaufisha ukweli na kuupa uongo nafasi?

Kwanini upendeleo wa ukanda na nyumba ile umekuwa sio wa kificho? Tena ni jambo lililowazi walioanzisha husema “Sisi ndio sisi tukianzisha wanafuata” Naona hata vituo vingine vya radio, Runinga hata Blogs nazo zimekuwa kikanda. Najiuliza ni kwanini watangazaji wengine hawana misimamo na wapo kwa kufuata mkumbo? Sasa lakini kwanini wanafuata mkumbo?

Ni dhahiri hata katika mambo ya kuzungumzia maswala ya wasanii wa kizazi kipya kwa ujumla yapo kikanda. Huwezi kusikia amehojiwa Afande Sele,Nikki Mbishi,Jay Mo,Dayna Nyange na wengine wengi katika kutoa tathimini fulani isipokuwa msanii aliyetoka ukanda mmoja na mtangazaji husika. Hivi ni kwanini? Kwanini kila siku ni wale wale tunawasikia katika chambuzi za vitu vinayohusu wasanii kwa ujumla?

Kwanini wamejiaminisha kwa mtu mmoja kama sio wawili? Ni wazi wamekuwa waoga wa makaratasi au? Lakini kwanini waogope makaratasi? Mpaka leo hawajui tofauti ya Elimu na Ufahamu?

Wapo wengi wana elimu na hawana ufahamu, ila wapo wasio na elimu na wanao ufahamu. Sasa kwanini wenye ufahamu hawapewi nafasi?. Bali msanii chipukizi kupewa nafasi ya kuzungumza yaliyomegi ambayo ni wazi wapo wakongwe waliopigania mengi kuhusu muziki huu wa kizazi kipya, ila tunaona vile wanavyominywa na kunyimwa nafasi hata ya kueleza machache tu. Hivi kwanini wanatenda haya? Lakini kwanini mioyo yao haioni haya kusema uongo?

Chama chenye dhamana ya kuzungumza juu ya mambo yote ya wasanii wa kizazi kipya ni TUMA yani Tanzania Urban Music Association, ambapo kikatiba Mwenyekiti au Katibu ndiye anapaswa kuzungumza juu ya maswala ya wasanii wote wa kizazi kipya. Lakini kwanini sasa hatujawahi kusikia wakihojiwa kuhusu lolote katika muziki wa kizazi kipya?. Isipokuwa msemaji wa genge fulani la muziki kupewa nafasi hiyo, lakini kwanini ? ni wazi ni katika chuki, fitna, na ukanda.

Lakini tusisahau mwaka huu 2016 tumeona wasanii wengi wamejiunga TUMA hata wale ambao walikuwa wakikipinga chama pamoja na kusema maneno ya hovyo. Ambao pia waliwahi kuanzisha genge lao ambalo walitaka liwe ndio chama cha muziki wa kizazi kipya. Lakini ni wazi TUMA ndicho chama chenye dhamana ya mambo yote ya kisanii yani muziki wa kizazi kipya. Mwanzo nilijiuliza ni kwanini wamejiunga kwa kasi? Lakini ni jambo lisilopingika uchu wa madaraka na kuandaliwa kuongoza jahazi mazingira yameshatengenezwa. Lakini ni kwanini imekuwa kama siasa kwenye hili?

Muziki wa kizazi kipya umekuwa ni muziki wa ujanja ujanja tu, sio tena kipaji chako. Ni wazi wengi unaowasikia radio na kuwaona Runingani sio kama wana vipaji kuliko wale ambao tunawasikia kwa uchache zaidi, bali urafiki na ukanda uliotawala. Lakini kwanini imekuwa hivi?

Lakini kwanini fitna za apande huyu ashuke huyu zimekuwa kubwa? Ni wazi ukiwa mwenye kujua na huendi nao katika mlengo wao lazima wafanye kila njia wakudondoshe, sasa ni kwanini huwa wanafanya hivyo? Lakini pia kama ikitokea kuna jambo fulani hujitanguliza na kutaka waonekane wema zaidi, kwanini hawatendei wema kweli? kama vile wanavyojivisha ngozi ya kondoo kumbe ndani ni chui.

Ifike mahala tuweke usawa, siachi kujiuliza kwanini wengi wamekua mabubu katika kusema ukweli huu? Wengi wao wakipewa sifa ambazo sio stahili kabisa, lakini kwa nguvu ya ukanda tumeona wakipewa.

Dhambi ya ukanda haiwezi kuishia pazuri, dhambi yake itapeleka pabaya muziki huu.

Acha kuleta ukanda wewe, amka kuwa sawa na kila upande

“Lakini kwanini”

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez