Kweli Roma atumie mistari ya Moni? Lakini ujasiri wa Moni kunena Nikki Mbishi ni msanii chipukizi anapata wapi?

Kweli Roma atumie mistari ya Moni? Lakini ujasiri wa Moni kunena Nikki Mbishi ni msanii chipukizi anapata wapi?

Kuna nyakati msanii anaweza akanena jambo kiasi wajuzi wakaishi katika semi za mswahili na katika tafsiri ya kizazi cha sasa ikaleta chang’anyo kubwa mno.

Lakini acha iwe katika uhalisi wa uhalisia wa mswahili yakuwa “Uzuri wa godoro wa nje tu, ndani mna pamba” naam! (Ufahamu).

Hivi Moni anajua maana ya msanii chipukizi?. Kwanza neno ‘Chipukizi’ ni uzao wa neno ‘Chipukia’ na maana nzima ya neno ‘Chipukia’ ni uhalisi wa neno ‘Chomoza’ yani toka chini kwenda juu kwa hali ya kuonekana.

Hivyo msanii ‘Chipukizi’ ni msanii ambaye ameanza kuonesha wazi uwezo wake wa kisanaa ambapo uhitaji wake ni akili za watu wapenda Sanaa ya muziki kuangalia na kujadili yake hiyo, lengo kuu ni kuuza. (Upcoming Artist).

Je!Moni Centrezone ushapata maana ya msanii chipukiz hapo? Na kwa upana wa  Nikki Mbishi juu ya Sauti ya Jogoo album 2009, Kanda mseto Malcom XI 2013, na Ufunuo wa Unju Bin Unuk 2015, unapata wapi ujasiri wa kunena yakuwa Nikki Mbishi ni msanii chipukizi?.

Hakika mswahili hakukosea kunena yakuwa “Usigombane na mkwezi nazi imeliwa na mwezi’ (Akili).

Lakini neno kuu lanena “Mpe ufahamu asiye na ufahamu katika ujenzi wa kesho yake njema” basi tumeona yafaa kumpa ufahamu msanii Moni katika upana mkubwa ili apate ufahamu wa ujuzi wa msanii chipukizi na upana wa album na kanda mseto za Nikki Mbishi, ambapo yeye mwenyewe Moni  hanayo.

Lakini kweli Moni kinywa chake kinaonekana kimejaa changarawe kwa mapana yake, hivi anaweza kunena yakuwa “Roma anatumia mistari yake kwenye majukwaa”.

Hili ni chekesho kwa maana ya aina za tungo za Roma na Moni ni vitu viwili tofauti, lakini ikumbukwe wengi pamoja na wajuzi wa muziki walimfahamu Moni kupitia Roma.

Roma alikuwepo tangu 2007 na wimbo wake wa Tanzania ambapo mpaka sasa anafanya vyema. Ila hata kwenye majukwaa mengi Roma ni mwenye kutumia mistari mingi ya zamani ambayo huchukua hisia za mashabiki wengi mno.

Na kwanini Moni asiweke hadharani tungo ambazo Roma anatumia? Ifike mahala Moni akajua tofauti yake na Roma ni kubwa mno katika Sanaa hivyo kuchunga kinywa katika mahojiano mengi ni jambo lenye faida kwake.

Kunena ubaya na uongo kwa Roma haiwezi kumjenga kisanaa bali kumbomoa kwa upana na wajuzi kumpuuza vyema.  Ni vyema afanye Sanaa yake katika hekima na misingi ya simamio la kazi.

Lakini haitushangazi hii maana mswahili anena yakuwa “Mchunga peku hapendi ila hana viatu”. Tafakari…

#TuzungumzeMuziki

 

Attachment