KUTUZIBA MIDOMO HAITOSHI, KATENI NA NDIMI BASI

Kutafakari hekima za wazee wetu na wahenga si jambo baya hata, nadhani ni mgodi wenye utajiri wa maarifa. Nianze kwa kusema Mjumbe kamwe hauwawi, hakukuwa na sababu ya kuziba koo lake ili asipaze sauti kwa maana ni kazi bure.

Leo nimeona kuangazia swala muungwa mmoja ambaye wengi wetu tunamfahamu ambaye kwa makusudi aliamua kuturejesha katika nyakati ambazo zilikuwa zimekwisha pita, nyakati ambazo hatuna uwezo wa kuzirejea tena isipokuwa kwa mawazo tu, nyakati ambazo kwetu zimebaki kuwa historia.

Mtamaduni huyu hana nyenzo nyingine anayoitegemea ukitoa koo lake lenye kufikisha mawazo na hisia zinazoujaa moyo wake. Ni moja kati ya wachache wenye uthubutu. Najaribu kuzitafakari tungo zake hizi ambazo zimeonekana kuwa kero, lakini sioni ubaya wake kwani zilikuwa zinaturejesha nyuma na kutukumbuza awamu ile ambapo tulipewa uhuru nasi tukageuka wenda wazimu. Tulisahau kuwa muda hauna rafiki, ukifika wakati wake wa kwenda utakwenda na kuacha alama kama maji yapitavyo kondeni.

Tungo hizi zilikuwa na lengo la kutukumbusha hisani za bwana mmoja ambaye amepita hivi punde, na wala haikuwa zamani. Muungwana huyu alitenda wema na kwenda zake hakuwa na muda wa kungoja shukrani.

Kwake yeye kina KEJELI na KEBEHI aliwapa nafasi katika paa lake na kuwapachika jina MATANI. Lakini shukrani yetu siku zote ilikuwa ya punda, tulimwona punguwani. Na maneno ya shombo eti “Anatokea pwani”. Ama kweli kiburi si maungwana. Je, leo maji yametufika shingoni au utosini?

Haijalishi maji yapo wapi, nasadiki maneno ya aliyekuwa rais na mwanamapinduzi wa Cuba, hayati Fidel Alejandro Castrol Cuz katika andiko lake alilolipa jina la HISTORY WILL ABSOLVE ME. Ambapo sehemu ya andiko hilo inasema “No weapon, no violance, can vanquish the people once they decided to win back their rights.” Akimaanisha kuwa hakuna silaha wala nguvu inayoweza kuwazuia watu pindi watakapoamua kurejesha haki yao.

Kupita maneno hayo ya Fidel ni wazi kuwa silaha ya watu ni watu wenyewe, kama ilivyo kwa siasi na mtaji watu. Lakini je, kwanini tunalazimishwa kunywamaza KIMYA ili hali macho yanashuhudia kinachotokea? Kwanini tusikatazwe kuona na kusikia pia? tubaki kuwa mabubu, viziwi na vipofu. Ni nani awezaye kubadili kilio na maombolezo ya msiba kuwa nderemo na shangwe za harusi? hakika ni wazimu kama unasikia msiba nawe unaamrishwa kufunga kibwebwe na kucheza ngoma. Kwani penye kheri kuna haja ya kumwambia mtu asherehekee?

Lakini KIMYA ndicho kinachotugharimu, kimya ambacho mwalimu alituwekea bayana ili tusije shindwa mtihani huu. Kwa maana duniani kote hapajawahi tokea mwalimu anayefurahishwa na kushindwa kwa mwanafunzi wake. Ndio maana mwalimu alitumia kila liwezekanalo kutufumbulia mafumbo haya. Kupitia UHURU NA MAENDELEO mwalimu alitudokeza sifa za kiranja ambaye ataweza kutufikisha katika nchi ya ahadi, nchi ya maziwa na asali, nchi ambayo kwetu sisi imebaki kwenye tungo za marehemu Shaaban Robert (Kufikirika).

Mwalimu alimwita kiranja huyo kwa jina la “Kiongozi” na matendo yake aliyaita “Uongozi” akisema “Maana Uongozi, maana yake sio kuwakemea watu; maana yake sio kuwatukana watu au kikundi cha watu usiokubaliana nao; wala maana yake sio kuwaamuru watu kutenda hili au lile. Uongozi maana yake ni kuzungumza na kushauriana na watu, ukiwaeleza na kuwashawishi” hizi ndizo sifa ambazo mwalimu aliona yeyote aliyenazo basi atatufikisha katika nchi ya ahadi.

Tumeendelea kuishi na kumsubiri mteule atakaye tuvusha bahari ya Sham na kutufikisha katika nchi ya ahadi, nchi ambayo mwalimu aliona wanafunzi wake tunastahili kuwako na kufurahi ladha tamu ya maziwa na asali. Lakini katikati ya safari ghafla kimezuka KIMYA ambacho mwalimu alikiona tangu mwaka 1994 na akatuasa kupita andiko lake alilolipa jina la UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA. Ni andiko hili ambalo mwalimu alisema “KIMYA msidhani ni ishara ya amani”

“Mnyonge Mnyonge, lakini haki yake mpeni…”

Pius Matonya

Unaipa Nyota Ngapi?

2 Bad
User Rating:
2 ( 4 Votes )