Kupingwa na wazazi, kukubalika na jamii, kuwa ajira isiyo rasmi na sasa kupingwa kwa mabavu. (Muziki)

Kupingwa na wazazi, kukubalika na jamii, kuwa ajira isiyo rasmi na sasa kupingwa kwa mabavu. (Muziki)

Kwa hakika hakuna utumwa mbaya kama ule wa kujiona uko huru katika mengi yakuzungukayo kila leo.

Na hakika waswahili ni wajuzi kwa kuweka wazi yakuwa “Adhaniaye amesimama, aangalie asianguke”

Bila umakini, kufikiri, na kuheshimu Sanaa ya muziki hakika twasema itaanguka kwa upana wa mlezi kutokujua namna ya kulea. Lakini hii ni kutokana tangu kuzaliwa kwa mtoto huyu (Muziki) hakuwa kwenye mikoni ya mlezi bali mwenyewe.

Katika ile kweli tangu kuchipuka kwa muziki miaka ya 1980 na kuendelea ni wazi ni muziki ambao umepitia kupingwa kwa ngazi ya wazazi, lakini kwa nguvu ya jamii muziki ulikubali.

Na baadae miaka ya 1990 mpaka 2015 kuwa ajira isiyo rasmi kwa vijana wengi na katika uhalisia muziki umeokoa familia nyingi mno licha ya kuwepo mengi mabaya yenye kupoteza haki za msanii husika mpaka sasa 2018.

Tupo pazuri kwenye ufanyaji muziki lakini kwa wakati huo huo tu mahali pabaya Zaidi kwenye malezi ya muziki. (Hofu)

Kwa maana ya tayari mataifa mengi yamekuwa ni yenye kututazama juu ya nyimbo zetu kiasi cha kushiriki tuzo Nyingi na hatimaye kuchukua ushindi.

Lakini tupo pabaya maana mlezi  hathamini wala kuweka mikakati ya kuujenga Zaidi lakini akiwa ni mwenye kutumia mabavu Zaidi katika kuuminya muziki huu. (Fedheha)

Hakika mlezi anatumia semi mbaya ya mswahili yakuwa “Akitaka kaa, mpe moto” Hakika tunaona wasanii wapewavyo moto. Maana nyakati zote wamekuwa kwenye vilio vingi mno juu ya Sanaa yote kwa ujumla, lakini vilio vyao havisikilizwi bali kufungiwa nyimbo.

Walezi na washika mpini wa muziki wanapaswa kujua yakuwa nyakati hubadilika, na ukitaka kuumia ni kubishana na mabadiliko ya kidunia. Ni wazi hutaweza maana mabadiliko ni mabadiliko tu.

Na mabadiliko ni mfano wa pulizo lililojaa upepo na kufungwa juu kwenye mdomo wake, hakika huwezi liminya likarudi kuwa utakavyo amini litapasuka.

Ila njia pekee ya kulilinda pulizo ni kuliwekea mazingira mema lakini kulishika kwa ustarabu na uhakika ili tu lisipasuke.

Hakika ndiyo ipasavyo kati ya mlezi na msanii lakini muziki kwa ujumla haipaswi kutumia mabavu kwenye maamuzi juu ya Sanaa ya muziki, maana muziki ni silaha kubwa Zaidi yaweza kupasua popote pale kama haitashikwa kwa uhakika na ustarabu.

Ila tukitazama katika kazi 9 za Baraza la Sanaa la taifa (BASATA) moja wapo ni “Kuishauri Serikali juu ya masuala ya yanayohusu sera, sheria, maendeleo, utengenezaji na mauzo ya kazi ya Sanaa nchini Tanzania”. Je hili linatekelezwa?

 

Kuna mengi yanahitajika kwenye hii Sanaa ya muziki ambayo Sanaa hii angalau imepunguza wanyang’anyi kwenye mitaa na hatimaye kujiajiri kupitia vipawa  vyao.

Ikumbukwe unapofungua wimbo wa msanii ni vyema kufikiri yakuwa alitumia muda, pesa, akili katika uwekezaji wa kazi hiyo. Hivyo yapasa afikiriwe kwa upana.

Lakini swala la maadili lapaswa litazamwe kwa upana sio kwenye muziki, kwani katika ofisi za mlezi wa muziki kuna maadili? Maadili ya viongozi kuheshimu Sanaa yapo? Maadili ni jambo pana mno sio la juu tu kama wengi wafikiriavyo.

Lakini ikumbukwe mzazi kutumia kiboko kwa mtoto haiwezi kuwa dawa bali kumfanya awe sugu hasa kwenye dunia hii ya mtandao. Kutumia hekima na maneno ya busara na kuwaza juu ya maisha ya mtoto kutafanya awe bora Zaidi.

Tunajua fahari kubwa ni kusifiana katika maamuzi mengi yenye kuumiza ubavu mmoja ambayo kiuhalisia hayajali wala hayafikiri mapokeo ya upande wa pili.

Lakini mswahili hakuacha kunena yakuwa “Fahari mama wa ujinga” ila yapasa mjue yakuwa “Mcheza na tope humrukia”

Ni vyema kutafakari katika nyakati hizi, na ndugu zetu wasanii yafaa mjue yakuwa “Akumulikaye mchana, usiku atakuchoma”

Tafakari….!!!!

#TuzungumzeMuziki

Twitter Tizneez

Facebook page Tizneez

Instagram Tizneez

Youtube Tizneez

Tuachie maoni yako hapa

Special Thanks To Askari wa Miguu.