KIKAO CHA WASANII CHA KISANII Sehemu ya III

tizneez
KIKAO CHA WASANII CHA KISANII
Sehemu ya III
Nyuki na inzi ni wadudu wanafanana kimaumbule,ila wanatofautina katika vitu vingi sana.Tofauti ya kwanza ni tabia, nyuki tabia yao ni kuwa wamoja katika mambo yote, uhamaji, kutengeneza asali na hata wakati wa kumshambulia adui yao ambaye atataka kufanya kitu tofauti na wao.
Inzi katika tabia huwa wapo pamoja hasa katika mizoga,vinyesi na vitu vingine vichafu, kweli huonekana wapo pamoja lakini umoja wao ni wa uongo wa hali ya juu. Maana kila mmoja hujisogeza kwenye mzoga au kinyesi kwa wakati wake huwa hawaji kwa muda mmoja. Na hata wakiskia mtikisiko wowote basi hukimbia kila mtu katika kona yake.
Hata wasanii huenda kwa wadau kila mtu kwa wakati wake, au kuna msanii aliwahi kwenda kwa mdau na wenzake? Mfano tu Afande Selle aende na Madee au Shetta aende na Ali KIba.
Wakati nyuki hata iweje daima huwa wamoja.Lakini inzi hawana umoja wao ni dakika chache zaidi.
“Wanatugawa kimakundi watumeze ona Anaconda,umoja utatoka wapi kati ya mchicha na mbuyu,wadau wana chenga nyingi kama walichezea Tukuyu” Kwa mujibu wa Roma kwenye wimbo wake wa KKK uliotoka 2014
“tunaimba sana lakini hatupati mafao jasho la msanii lakini wengine na ndio wanajenga”hii ni kwa mujibu wa Ferooz katika wimbo wao na kundi lake la Daz Nundaz Shuka Rymes miaka ya 2002.
“Nchi ambayo haitambui mchango wa sanaa,wanaoitwa wasanii mitaani wanakufa njaa bongo fleva ni utumwa ndo maana machizi wanajituma kusukuma madawa ya kulevya” Hii ni kwa mujibu wa msanii Nikki Mbishi ambaye alisema haya kwenye wimbo wake wa Natoka Tanzania, ambao ni moja kati ya wimbo wangu bora wa hiphop sasa.
Siku zinakwenda huku swala la mirabaha likiendelea kuchanganya walio wengi, wapo wanaolaumu, kusifia na hata wasioelewa mirabaha nini kitu gani. Na haya sio kwa mashabiki tu pekee hii ni mpaka kwa wasanii wenyewe, wapo wasioelewa nini wanakipigania. Ingawa wapo baadhi ya wasanii walioficha ukwel katika mioyo yao juu ya yale maadhimio yao matatu yaliyotangazwa zaidi kuliko hata haki zao juu ya mirabaha.
Lakini lazima watu wajue kwamba ukweli hauna rafiki wala hauitaji mtu, ukweli haupo upande wowote kati ya mke,mume,mweupe wala mweusi ukweli hujitenga peke yake. Na kuna nyakati unaweza ukaupenda sana ukweli na kuna nyakati pia unaweza ukauchukia sana ukweli kupita kiasi.
Ila uongo ndio unahitaji marafiki wengi walio waongo wenye kuwa wanafiki na wenye kutumia nguvu nyingi kuzuia jambo jema linalotaka kufanya hasa kwa wakati husika.
Ni vyema kufikiri kabla ya kufanya maamuzi hasa katika dunia ya leo yenye ukweli katika Nyanja nyingi.
Wapo waliowahi kupewa hotuba wazisome katika hafla mbalimbali lakini nadhani hawakuwa wanajua kile wanachokisoma.
Hebu tuwe wa kweli katika hili. Kweli unaweza kuwa kinara wa kusifia bidhaa yako kutumika bure huku ukiendelea kujisifu?
Nchi yoyote ile ili watu waweze kupata haki yao lazima waungane na wawe kitu kimoja. Wasanii wetu wa Tanzania wanapambana sasa kupata haki yao katika malipo ya mirabaha, ambayo kwa neno la Mh Nape ilibidi mapema mwezi wa kwanza mwaka huu wapate malipo hayo.
Wapo wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wasiotambua wala kujua sauti yao katika umoja huu ni ipi. Waswahili husema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Katika swala hili la mirabaha ni wazi wasanii wamekuwa wakifanana na maisha ya inzi,(mtengano) maana vipo vikao viliwahi kufanyika kabla ya kile cha mwisho kilichotoa tamko la mambo matatu, lakini vikao vingine vilikuwa na baadhi tu ya wasanii, yani havikuwa na ushirikishwaji wa TUMA, hivyo ni kama genge au maskani ambapo tunaweza kupiga zogo tu.
TUMA ndio sauti ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambayo nasema tena wasanii wengi hata hawajui kuhusu TUMA.
Mpaka sasa TUMA ambacho ndio chama cha muziki wa kizazi kipya kina wanachama 250 ni sawa na 5% kati ya asilimia 100%. Sasa jiulize kuna wasanii wangapi katika nchi yetu mpaka chama kiwe na wanachama wachache kiasi hichi?
Bado naendelea kuwaza vingi kuhusu baadhi ya wasanii wetu waliowengi ambao wamesema vyombo vya habari viendelee kutumia kazi zao bure. Lakini je maadhimio haya hayana shindikizo kutoka kwa mtu ambaye ananufaika na hili swala la kuendelea kutumia kazi zao bure? Na je hii imetoka kwa wasanii wote? Maana maana nijuavyo wasanii wa kizazi kipya wanawakilishwa na TUMA.
Pia wapo wasanii wengine wanaoendelea kuonekana kushawishi wenzao kuona jambo hili ni jema kabisa la nyimbo kuchezwa bure katika vyombo vya habari.
“kwa hisani ya promo mnarudi utumwani” Hii ni kwa mujibu wa Nash Mc.
Wapo wanaotaka kuendelea nyimbo zao kuchezwa bure ili waendelee kunufaika na matamasha ya kila leo, wiki na hata mwaka, na hawa ndio wanatumia nguvu nyingi katika kupotosha wenzao wakubali nyimbo zao kuchezwa bure.
Leo hii ukimwambia msanii yoyote anaejitambua eti nyimbo ziendelee kuchezwa bure au wasanii/msanii alipwe na chombo cha habari hakika atakujibu anahitaji malipo yake ya mirabaha, nina hakika nalo nilishauliza wasanii zaidi wasanii ya watano wenye kadi halali za TUMA.
Ngoja turudi kwenye lengo kuu haya mengine ni kujazia ili wenye uelewe mdogo wapate kujua kiundani nini ni nini. Katika andiko la kwanza tulipata maswali mengi juu ya kikao cha wasanii cha kisanii, na yote tuliyajibu kulingana na muulizaji.
Haikushia kwenye maswali tena katika andiko la pili la kikao cha wasanii cha kisanii, hasa pale mmoja wa wasanii aliposema eti makala hii ni ya zanio,haya yalikuwa ni maoni yake, Tanzania ni nchi huru hakuna anayepingwa wala kukatazwa kutoa maoni yake.
Siku, wiki, na mwezi ndio unaishia sasa na radio zimeendelea kupiga nyimbo bure na CMEA wameendelea kutoa taarifa juu ya nyimbo zilizochezwa katika vituo mbalimbali vya radio na runinga.
Umoja usio rasmi uliondwa kutoka kwenye kikao cha mwisho naona mpaka sasa haujasema kitu, lakini waliahidi yaliyo mengi na hata msemaji asiyetambulika na TUMA aliongea mengi na hata wasiojua nyuma yake kuna nini walisifia tu. Tuachane na umoja huo maana unaongozwa kwa maneno tu, hauna katiba wala kanuni, ngoja twende kwenye mambo ya msingi.
Hapa katika CMEA kuna wasanii walio wengi hawajui kazi ya CMEA ni nini ndio maana wapo baadhi yao walitumia nguvu nyingi kuipinga katika kikao kilichofanyika Osterbay. Ila wale waliopinga wapo waliowahi kutumia zile taarifa na wengine wakiendelea kutumia zile taarifa zitolewazwo na CMEA mpaka sasa. Licha ya wasanii wachache ambao ni vinara wa kupinga hili kwa maslahi binafsi kufuta hata zile post walizowahi kupost juu ya takwimu za CMEA. Lakini wenye kujua kazi na nafasi ya CMEA katika muziki wao wameendela kueleza mashabiki wao kwa njia ya kuweka picha ya takwimu katika kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya kueleza kazi za CMEA ngoja tuweke sawa maneno ya msanii chipukizi Nikki wa Pili “Hope yule mwandishi wa makala yenu amesikia habari za 6 telecom, sasa nadhani ile makala yake ndio ya kisanii next tym awe makini”. Tizneez haijawahi kuandika juu ya 6 telecom hata siku moja, pengine unachanganya CMEA na 6 telecom. Wacha nikusaidie 6 telecom na CMEA ni kampuni mbili tofauti kuanzia usajili mpaka uongozi. Pia CMEA na 6 telecom kila moja inafanya kazi zake katika ofisi yake na wafanyakazi wake pia ni tofauti. Na CMEA inaendelea na kazi zake vile vile. Hivyo usichanganye CMEA na 6 telecom, nadhani umeelewa sasa.
Kazi ya CMEA ni kukusanya taarifa kutoka kwenye radio na runinga ambazo zitacheza muziki wa msanii yoyote,na kama taarifa zako zipo pale CMEA basi itaonyesha kila kituo Radio na Runinga ambacho kimecheza wimbo huo. Na baada ya kukusanya taarifa hizi ndipo pale zinapopelekwa COSOTA ili waweze kukusanya mirabaha kutoka kwenye vituo husika ili msanii aweze kulipwa. Sasa hapa wanaopinga wanapinga nini? Hivi kweli wasanii wanapinga au kuna mtu nyuma ya wasanii ndio anapinga?
Pia wapo waliopinga labda kwa kutokujua wanapata asilimia ngapi katika mirabaha yao. Kazi yetu waandishi si tu kuburudisha kwa uandishi wa misemo mizuri ila hata pia kutoa elimu ya mambo mbalimbali.
Katika mafungu ya mirabaha ambayo yangekusanywa na COSOTA kupitia taarifa za CMEA, katika mgawanyo wa asilimia 100 basi msanii angechukua asilimia 60 na asilimia 10 angewekewa katika mfuko wao ambao ni kwaajili ya mambo mbalimbali kama misiba,maladhi,na hata mengineyo.Na asilimia 30 zingekwenda COSOTA na CMEA kwaajili ya uendeshaji wa mitambo pamoja na shughuli nyingine.Je katika hili nalo msanii/wasanii wanapinga nini?
“Mfa maji haishi kutapata”Ama kweli sasa naamini katika msemo huu. Hapa tena naona wale vinara kadhaa wa upingaji wa mchakato huu wanapotoa hoja zisizo na mashiko eti! Wasanii hawakupewa ushirikishwaji, hili halina ukweli.Na hili halinishangazi pia maana kipindi mchakato unafanywa kuhusu CMEA kupewa kazi hii, ushirikishwaji wa wasanii uliokuwepo kutoka kwenye vyama vyao. Licha COSOTA pia kufanya semina kadhaa ya kuelimisha lakini muitikio wa wasanii ulikuwa mdogo.
Acha wewe msanii/shabiki mmoja kushangaa kinachoendelea maana hata mmoja wa viongozi wa TUMA pia anashangazwa na yale yanayoendelea
“kinachoendelea sasa hivi sijui kwamba kuna undani gani wa hilo jambo, ndio maana hata mimi mwenyewe sasa hivi natumia muda mwingi kutaka kujua kiundani ni chanzo cha wasanii kusema hawahitaji CMEA au hawaitaji COSOTA kwasababu COSOTA sisi wenyewe tulipigania kuhakikisha uongozi wa COSOTA unabadilishwa ambapo ulikuwa na Bwana Mkinga. Maana wasanii walikuwa na malalamiko yao, na malalamiko makubwa yalikuwa hawasikilizwi walikuwa hawapati nafasi na hata mambo yao hayakuwa na ufutailiaji pia utendaji. Na ukweli tulifanikiwa maana Mh Rais aliyekuwa madarakani wakati ule Mh Kikwete alimuondoa madarakani yule bwana na ndio tukaletewa huyu dada Dorin na ukweli ni kwamba tangu muda aingie Dorin tumeona ni mtu anayetusikiliza na anafuata tunayo yataka na anatupa ushirikiano wa karibu, na hata tulivyomwambia hili (MIRABAHA) yeye ni mtu mmoja wapo ambaye amefanikisha tu, sasa tuwe na kampuni inayokusanya mirabaha na Wizara hizi mbili zimeshirikiana kukubali kwamba ni kweli wasanii wamehangaika kwa muda mrefu hawalipwi lakini sasa hivi waanze kulipwa.”Kiongozi huyo aliendelea
“Ukitaka historia ya nani alianza uliza wakina Chamudata, John Kitime, hizi harakati wamezianza muda mrefu,uliza wakina Sugu wameanza hizi harakati muda mrefu tangu miaka ya 2002-2003 wanapambana.”
Kikao cha wasanii cha kisanii kuna mengi yanaendelea kuibuka siku baada ya siku, ile siku walichagua kamati ambayo hata haijulikani inafanya kazi chini ya nani. Inawezaje kufanya kazi wakati wengi waliochaguliwa sio wanachama wa TUMA? Kwa maana wanachama wa TUMA au chama chochote kile basi ni lazima mtu au mwanachama awe na kadi iliyo hai. Na hapa kama wangekuwa wanachama halali lazima wangekuwa na umoja wa kuwa na sauti moja kupitia muakilishi mmoja.Ingawa inasemekana eti!wamepeleka malamiko kadhaa kwa Mh Waziri lakini je wameenda kama chama au ameenda mtu? Hofu yangu ni maamuzi kufanyika katika hali ya urafiki unaoendelea kuimarika siku baada ya siku.
Nilishangazwa siku moja kuona maneno ya msanii Baba Levo ambaye sasa ni diwani wa kata moja huko Kigoma.” “Hao COSOTA wanapaswa kutupisha kwenye hizo office, wao wanakusanya pesa kuzigawa kwa mafungu bila kujua nani kapigwa bar na nani hajapigwa club nani hajapigwa. Wameshindwa kuzuia nyimbo zinazouzwa mitaani na watu wa kuburn na kompyuta,yani wana mapungufu milioni na kidogo so kazi ni moja waondoke watuache wasanii wenyewe tuendeshe kitengo hicho #D_ONE” hii ni kwa mujibu wa Baba Levo,ambapo aliandika katika mtandao wa picha Instagram.
Hapa narejea kauli ya Mbunge wa Mikumi sasa Mh Joseph Haule a.k.a Prof Jay “Watu viwango vidogo wanalewesha na sifa”
Huyu huyu anasema kama COSOTA wanagawa hela kwa mafungu ameshalipwa hela mara nyingi tu na COSOTA kutokana na kazi yake ya muziki. Na hela hizi alianzwa kulipwa tangu kipindi kile yupo kundi moja la TMK Wanaume. Leo Napata mashaka na kauli zake hizi, hivi kweli ni Diwani?na anaongoza watu wa aina gani? Mana najua sifa ya kwanza ya kiongozi ni kuwa mkweli.
Ni wapi imeandikwa au imeelezwa COSOTA inatakiwa iendeshwe na wasanii?. Na kwanini ni wasanii walio wengi ambao wanaonekana kuleta maneno mengi ni kutoka katika muziki wa kizazi kipya zaidi?.Pia kuhusu nyimbo za kwenye kupigwa katika bar leo COSOTA ina maafisa watano tu ambao wanaweza kufauatilia juu ya nyimbo zinazopigwa huko. Hivyo ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu ni wazi bado wanahitaji maafisa wengine wengi.
Lakini nakumbuka niliwahi kuongea na C.E.O wa COSOTA bi Dorini “Ni wazi kuna changamoto nyingi ila kama swala la mirabaha litaanza kufanya kazi basi litanyoosha mambo yaliyo mengi,ikiwemo baadae kuanza kuweka nguvu katika kukusanya mirabaha kutoka kwenye bar na kila mahali panapo stahili”
“Simshangai Baba Levo maana yupo pia msanii anaesafiria nyota anaetamani angeimiliki COSOTA
Ni bora nikasema ukweli na kumfanya mtu akalia kuliko kumwambia uongo na akafurahi, upendo ni kuelezana ukweli.
Itaendelea. KIKAO CHA WASANII CHA KISANII sehemu IV
www.tizneez.com
Twitter tizneez
Facebook tizneez
Instagram tizneez