“Kichwa kisicho na akili ni adhabu kwa miguu”Snura

snura-234

“Kichwa kisicho na akili ni adhabu kwa miguu”Snura

Chanzo cha maovu katika jamii zetu ni watu wema kuona matendo mabaya na kukaa kimya, hakika hiki ni kitu pekee kinachoharibu jamii kwa kiasi kikubwa “Ukimya”

Kuna watu hukaa kimya maana huona kama haiwahusu, hivyo hawana haja ya kupaza sauti zao. Lakini hakuna jambo jema kama kupaza sauti katika mchango wa kuokoa jamii katika jambo baya. Isipokuwa ni jambo baya na chukizo kupaza sauti katika mambo yasiyo na msingi yenye kuharibu jamii.”Ubaya”

Inanipa imani ya kuamini wengi wetu tuna nyoyo za unafiki ndani yetu, na hata kuona ni mbaya kusema jambo lenye ukweli ambapo itajenga ile kweli jamii zetu”Ukweli”

Tusiogope kuambiana ukweli, na tuache tabia ya kusifia ujinga ambapo hauwezi kutufikisha mahala tukiwa na heshima za hali ya juu katika sanaa yetu. Nguvu ya mambo ya hovyo (Ujinga) imendelea kuwa kubwa katika jamii zetu hasa katika mitandao ya kijamii. “Ujinga”

Nidhamu ya sanaa inashuka kila iitwapo leo, na hakika kwakuwa tuna nyoyo za uoga na hatuwezi kuambiana ukweli pale ambapo mmoja anapostosha nidhamu ya sanaa na maana halisi ya sanaa ya muziki, hakika tunazidi kukandamiza sanaa yetu nzuri ya muziki. Nidhamu iko wapi? Hivi sanaa ni kuweka mambo yasiyo ya msingi katika mitandao? Nidhamu iko wapi katika kazi ya muziki? “Nidhamu”

Katika kila jambo huanza dalili, hakika dalili za chura ya Snura zilianza kwa kasi kubwa katika mitandao ya kijamii hususani mtandao wa picha Instagram. Haikuwa jambo jema na la kupongezewa isipokuwa baya na hata kuwa ni chukizo kwa walio wengi. “Dalili”

Mengi yalisemwa katika kile alichokuwa anakifanya cha kuweka video zenye kuonyesha maungo yake ya mwili huku akicheza bila kujali. Hivi katika uhalisia hii ni nidhamu ya sanaa ya muziki? Na hapa niliona wazi anafuta ile kauli ya msanii ni kioo cha jamii, maana alichokuwa nafanya ni wazi ilikuwa ni kuibomoa zadi jamii.

Moja ya maswali niliyokuwa najiuliza ilikuwa ni huyu si mama wa watoto wawili? Je hana ndugu?hana marafiki?hana hata mtu wa kumuoenea aibu kwa kile anachokifanya?

Nyakati zikapita na hatimaye akaamua kufanya na video iliyokamili na kuonyesha mengi yanayotia kinyaa mbele ya jamii, video ambayo kama wewe ni msanii na unayo nidhamu ya kazi hakika huwezi kufanya. Lakini alifanya na hata kupata mahojiano katika vituo vilivyo vingi vya radio na runinga. Na hata kufanya matumbuizo yaliyomengi, na hakika katika matumbuizo haya ilikuwa ni vioja visivyosemekana.

Maswali yalitawala kichwa changu, je sekta husika haioni uchafu huu unaofanywa na unaendelea kila iitwapo leo? Hata kuamua kumuuliza msemaji wa Basata hivi huwa hawachukui hatua kwa msanii kuweka picha au video mbaya kwenye mitandaoya kijamii?. Lakini majibu yake ilikuwa “video zote zinapita katika bodi ya filamu si Basata, unajua watu wanatupia kila kitu Basata kwa sababu tunasikika zaidi na tupo kwenye midomo ya watu

Majibu yake yaniridhisha ila nilitafakari katika upande wa msanii zaidi maana ni wazi niliona ni mwenye kupotoka kutoka kwenye sanaa yake na kwenda upande usiofaa. Kwa kipindi hiki cha video yake nimekuwa msomaji mzuri wa maoni ya wale mashabiki wake, hakika nawapongeza maana walio wengi wameoneshwa kuto kufurahishwa na kile anachokifanya msanii wao.

Ikumbukwe si lazima kuweka video au picha mbaya na upate mashabiki, isipokuwa kazi yako ikiwa nzuri na nidhamu yako itakufanya uwe na mashabiki walio wengi. Ila kadri siku zinavyokwenda tumeaona wasanii wengi wa kike wakitumia miili yao kuvaa nusu uchi imradi kupata mashabiki. Ila je wanafikiria kuhusu heshima ya kesho yao? Sekta husika isiache kuhusika hapa kwenye hili.

Kumekuwa na maneno mengi katika mitandao ya kijamii kuhusu Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya kuchukua hatua ya kufungia wimbo wa msanii Snura pamoja na kusitisha maonyesho ya hadhara mwanamuziki huyo.

Sitaacha kuwapongeza kwa hatua hiyo nzuri na yakusifiwa, ni wazi kama taratibu na sheria zitafuatwa hakika tutakuwa na wasanii makini wenye nidhamu katika kazi zao. Lakini pia lazima ifahamike kama tunajenga taifa lenye nidhamu pia kufuri lao lisiishie kumfungia Snura tu, isipokuwa kuna mengi ambayo ni wazi wanapaswa kuyawekea kufuri tena wazi wazi bila hata kificho. Pia ikumbukwe kinga ni bora kuliko tiba, ikiwa na maana leo tayari video ya chura imeshasambaa katika maeneo yaliyo mengi nchini. Hivyo ni wazi lazima mabadiliko ya kazi yafanyike mapema kabla ya siku nyingi mbeleni.

Mashaka juu ya kufuri lao bado yapo, maana hata msanii Shilole aliwekewa kufuri lakini ndani ya siku chache tulimuona kwenye majukwaa akifanya matumbuizo. Kiuhalisia swala hili lilileta picha mbaya katika jamii, nakuona wahusika hawasimami katika kauli zao na nafasi zao. Hivyo kama hatutasimamia kauli zetu na nafasi zetu swala hili la utovu wa nihamu kwenye kazi ya sanaa litaendele kukua siku baada ya siku.

Nani mshauri wa msanii Snura? Je hakumwambia kichwa kisicho na akili ni adhabu kwa miguu?. Maana kama kichwa kinashindwa kufikiri juu ya kazi zilizo njema je utawezaje kupata mafanikio? Ni wazi utaitesa miguu yako kwenye kuzunguka kila mahala, wakati kama ukitumia zaidi kichwa utajikuta ukifanikisha mambo katika wepesi usiotarajia.

Sanaa ya muziki ina misingi yake, ishike misingi iweke mbele nidhamu yako, epuka kufanya mambo yasiyo na msingi hakika utajenga heshima kubwa ndani na nje ya muziki.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez