Kabla hujataka kuchukua fedha kwa wasanii je! umeandaa mazingira gani juu yao? (Basata)

Kabla hujataka kuchukua fedha kwa wasanii je! umeandaa mazingira gani juu yao? (Basata)

Hakika semi ya mswahili ya “Changu chetu, chako chako” ni uhalisi wa Basata na wasanii. Kwa upana wa Basata kutaka zaidi vya wasanii kuliko kuweka usawia wa mengi juu ya msanii. (Sanaa)

Mabadiliko ya bei katika usajili wa wasanii na mengi yahusuyo sanaa ni makubwa mno kutoka kwa Basata.

Na leo tunapenda tuzungumze pande ya msanii na kampuni katika usawia wa kutangaza biashara (Branding).

Katika kweli yenye kweli wasanii wa sasa wengi wanafaidika zaidi katika kutangaza mengi kwenye makampuni tofauti tofauti. (Kweli).

Hivyo kitendo cha Basata kutaka kuchukua Milioni 5 katika kila tangazo ambalo atashiriki msanii ni wazi ni kupoteza biashara hiyo kwa msanii.

Lakini katika ile kweli yenye kweli si kuna tozo ya mamlaka ya mapato katika malipo ya msanii tena kwa mtindo wa asilimia ambao si adui wa msanii, vipi wao Basata kupanga gawio kubwa zaidi? (Fedheha))

Hakuna kampuni ambayo itakuwa tayari kulipa pesa hiyo kwa Basata, bali kuacha kuwatumia wasanii.( Uhalisi)

Jambo hili halikuzi sanaa bali kuiua sanaa kwa upana, na kweli hii msanii gani anyanyuke na anene hadharani? hakika hakuna maana nyoyo zao daima hutazama faida ndogo na vitu vya upuuzi. (Uhalisi)

Naam! twanena laiti kama ingekuwa ni jambo la hovyo yani halina kichwa wala miguu hakika ungeona namna ambavyo wangeposti kwenye mitandao, ila uhalisi huu wa uvurugu kwa biashara yao wapo kimya. (Soni)

Lakini wapo ambao wanajua wakinena watakosa fursa ndogo ya kipuuzi ile ya kualikwa katika maeneo mengi na kuweza kuchukua picha wakiwa na glasi za juisi na baadae kuweka kwa mbwembwe mtandaoni.

Na wenyewe huandika “About Last Night” Hakika ni soni yenye soni.

Kila leo twanena yakuwa kupiga picha na glasi za juisi na viongozi wengi haiwezi kuwa mwarobaini wa sanaa, bali kunena changamoto zenu kwa upana wake.

Jambo la Basata kutaka hiyo fedha kwa makampuni baada ya msanii kushiriki katika tangazo ilipaswa wasanii mnene kwa hoja katika katazo la kupinga, lakini msanii gani anaweza nena?

Lakini chama (TUMA) viongozi mbona mmefunga vinywa vyenu? kwani kazi yenu hasa ni nini?

Kitu ambacho Basata wanapaswa kujifunza ni upana wa biashara ya sanaa na faida zake, lakini kumbukeni kumbukumbu juu ya ‘Dira’ na ‘Lengo kuu’ lenu

Maana ‘Dira’ ya Basata ni “Kuwa msimamizi na mwendeshaji mahiri wa sanaa, mapato ya sanaa na wingi wa uzalishaji wa sanaa nchini Tanzania”

Ilihali ‘Lengo kuu’ ni “Kuwezesha uzalishaji, uuzaji, utumiaji na ushiriki katika shughuli za sanaa bora”

Je! katika hiyo ya kutaka milioni 5 wamewezesha nini katika uzalishaji wa fedha hiyo? au wamesimamia na kuendesha lipi kiasi cha kuwa na uhalali wa kuchukua fedha hiyo?

Hivyo katika ‘Lengo kuu na Dira’ ni vyema kuamua hata mtu mmoja kwenda katika nchi ambazo zimeendelea kisanaa na wasanii wake wanafaidika zaidi lakini kuchangia uchumi wa nchini kwa mapana.

Hapo waende katika kujifunza yakuwa wenzetu walifanya vipi kiasi cha sanaa kufanya wasanii na watu wengine kuishi vyema?

Bila kwenda na kufanya chunguzi yakujua hakika twaambia sanaa hii itakuwa mahala pabaya zaidi maana tayari mpaka sasa ishapoteza muelekeo katika mengi. (Uhalisia)

Na daima mswahili hunena yakuwa “Kheri mrama, kuliko kuzama” Ila hakuacha kunena kwa upana yakuwa “Huwezi kuona msitu ukiwa msituni” Tafakari….

#TuzungumzeMuziki