JINAMIZI NYUMA YA MWANAZUONI

jinamiz

JINAMIZI NYUMA YA MWANAZUONI

Sanaa!Sanaa!Ama kwa hakika ni tunu iliyotukuka sana. Ni nani asiyetambua ladha ya muziki sambamba kabisa na ala zake zilizopigwa kwa ustadi wa hali ya juu. Hatuna budi kumpa sifa yule ambaye aliyegundua utamu na ladha hii maridhawa, ambayo kama haitakufanya utikise kichwa basi utatirikwa na machozi. Ama kweli muziki ni faraja ya wakati wote.

Katika nchi yetu nzuri Tanzania tumebarikiwa kuwa na vipaji vingi katika muziki, lakini napata kigugumizi kila ninapowatafakari hawa ndugu zetu ambao bila wao muziki kwetu ungebaki kuwa ndoto, ambayo hakuna mtu ambaye angependa kuona tamati yake.

Mchezea kwao hutunzwa, nasadiki sana maneno haya ya wahenga. Ingawa Napata mashaka ninapojaribu kuyaunganisha na hali ilivyo katika muziki wa nyumbani. Hivi ni kweli tunawatunza wasanii wetu? Au ndio nabii hakubaliki kwao?

Bure gharama ndugu yangu!,sidhani kama ni vyema kuendelea kufurahia jasho la ndugu zangu ili hali wao wenyewe wanateketea kama mshumaa

Ni faraja iliyoje kuona mtu anakula kwa jasho lake, na kufaidi matunda ya kazi yake. Hata maandiko matakatifu yanasema “kila anayefanya kazi anastahili ujira wake” Je ujira wa hawa ndugu zetu ni majina makubwa,na kutokea katika vyombo vya habari kila iitwapo leo?

Tuachane na hizi rapsha ambazo mara nyingi zinakuwa na mwanzo tu, mwisho wake haufahamiki. Kama kuna kitu kinachoniumiza katika huu muziki ni kuona namna Jinamizi linavyotumia wasanii kujinenepesha. Ni juzi tu jinamizi aligombana na kikundi cha watu fulani. Lugha chafu zilishindwa kuamua mzozo huo.

Hatimaye giza likaingia, na kulipo chomoza tu kwa jua kelele zilitoka kwa yule aliyekuwa kipenzi cha Jinamizi, eti kwamba usiku uliopita Jinamizi alimkaba na kumuumiza. Kama kawaida yetu sisi tulikaa chonjo tukiumana masikio. Waswahili bwana huwa hatunyimani neno! Leo hii jinamizi wakumfanyia hivi shoga yake? Jua likazama kukiwa na kimya kizito na uchovu wa kusikiliza kelele za Jinamizi na shoga yake mchana kutwa. Usiku ulikuwa shwari sana kwa maana wote wawili walikuwa hoi kwa uchovu.

Jogoo nae hakawihii kuwika, eti wanasema usiku wa balaa haukawihii kucha. Siunajua tena kila mtu alikuwa na kiu ya kujua hatma ya Jinamizi baada ya kugombana shoga yake. Ndio kumekucha sasa hata nyasi bado hazijakauka umande. Tulikusanya vikundi vikundi tukisemezana jamani Jinamizi yupo kweli? mbona kimya? Sio kawaida yake hii. Wote tuliishiwa nguvu baada ya kusikia eti Jinamizi yupo chuga anafanya utalii wa ndani na kujiliwaza baada ya heka heka za jana na shoga yake.

Kweli kimya kingi kinamshindo mkuu, haikuchukua kitambo Jinamizi kuweka bayana kile kilichompeleka huko wanapopaita wenyewe chuga.Chambo aliyekuwa kwenye ndoano yake amefanikiwa kumnasa kijana mtanashati MWANAZUONI. Kama kawaida yake, Jinamizi halikunyonyi bila lenyewe kukunyonyesha na kukunenepesha wewe kwanza. Bahati ilioje kwa Mwanazuoni aliyekuwa na kucha butu katika muziki kwa wakati ule, sasa kucha zimekuwa kidogo anashindwa kuzifisha tunaziona wazi wazi.

Mwanazuoni amekuwa nyenzo nzuri ya kutekeleza matakwa yote ya Bwana ake JInamizi, ikiwemo na lile la kukuwadia wengine waingie katika mkumbo wake (Kuwadi).

Navutiwa na uwezo wa Jinamizi katika kutambua fursa zilizo mbele yake na kutumia rasimali zinazomzunguka katika kuteleza azma yake. Hupata urahisi mno anapokutana na mtu mwenye kiu kubwa ya kujilikana na kuheshimika, hivyo hakupata wakati mgumu katika kumraghai Mwanazuoni na ahadi kedekede ikiwemo zile za kufanya matamasha makubwa na kusikika na kuonekana kwenye vyombo vya habari.

Masikini amekumbwa na nini Mwanazuoni wetu?Mwanazuoni ambaye anajua joto ya jiwe wanayoipata wasanii. Mwanazuoni ambaye amesomeshwa na jasho la walipa kodi. Amepata wapi hii kiu ya madaraka? Anatutisha. Awali tulidhani atakuwa msaada kwetu. Ama kweli umdhaniaye ndiye kumbe siye, na mgema akisifiwa tembo hulitia maji. Na ndicho kilichotokea kwa sasa, je Mwanazuoni wetu maji kayatoa wapi? Mbona mwanzo hakuwa nayo? Ooh!kumbe Jinamizi ana kucha kali kama mwewe za kuparua popote atakapo, basi itakuwa kamchimbia kisima. Bado nashindwa kupata jibu pengine na wewe unaweza kunisaidia katika hili. Mwanazuoni na Jinamizi lao ni moja? (mke na mume) Au nani kati yao anamtumia mwenzie?

Ingawa historia inaendelea kujieleza kuwa Jinamizi ni moja kati ya madubwana yaliyonufaika zaidi na yanayoendelea kunufaika na muziki bila kukausha mate katika koo lake. Kitendawili hiki ni kigumu ambacho jibu lake litafahamika itakapofika kesho. Ingawa kuna mwandishi mmoja mahiri sana aliwahi kusema “Hakuna aijuae kesho hata mtunzi wa kalenda” Basi tuendelee kusubiri maana kesho hatuijui. Lakini vyema kutafakari maana haitakupunguzia chochote.

Solo Thang aliwahi kusema kwenye nyimbo ya Afande Sele Mtazamo “Unakuwa mtumwa ili upewe promo kuuza au kama binti ukalale kwa prodyuza, mapromota wanaumana tu hawajui na kupuliza”

Itaendelea

www.tizneez.com

Instagram tizneez

Facebook tizneez

Twtter tizneez

Makala nyingine zipo kaa karibu na tizneez.com upate yaliyo mengi yanayohusu sanaa yetu, hii ni Tanzania tu.asante.

Attachment