JAY MOE NA HILI GAME Sehemu ya pili

CV79z_iWIAAA5CG.jpg large

JAY MOE NA HILI GAME

Sehemu ya pili
______________________
Neno “mocumentary” ambalo linabeba jina la album yake ya tatu, ambalo Jay Moe hulitamka kama “mokyumenari” limetokana na muunganiko wa maneno Jay Moe na Documentary. Utaratibu huu wa kuunganisha maneno wanamofolojia wa kiingereza huuita “Blending” ambapo sehemu ya neno moja huunganishwa na sehemu ya neno lingine kutengeneza neno jipya. Kwenye neno Jay moe amechukua Mo na kwenye neno Documentary amechukua Cumentary, akayaunganisha ikawa mocumentary. Kwa maneno rahisi waweza sema “Mocumentary” ni Documentary za jay moe au Makala za Juma Mchopanga.

Jay moe anatukumbusha kwamba yupo katika game kabla ukumbi wa Diamond Jubilee haujaanza kujazwa kwa maonesho ya wasanii mwanzoni mwa miaka ya 2000. Diamond Jubilee kwa mara ya kwanza ilijazwa na Juma Nature katika uzinduzi wa album ya Ugali mwaka 2003 (Mkoloni, 2016). Mdau mmoja alishawahi kusema “Juma Nature ni msanii pekee aliyewahi kuijaza diamond jubilee mara tatu na watu wakakosa pakukanyaga”. Leo hii msanii kuujaza ukumbi mdogo tu wa maisha club, billz n.k anaandaa msululu wa wasanii ili kumpa sapoti kwenye shoo yake na bado ukumbi unaweza usijae.

Ukiacha Juma Nature Diamond jubilee iliwahi kujazwa wasanii wengine kama Profesa Jay, Daz nundaz, Gangwe Mobb, Dully sykes na T.I.D katika uzinduzi wa pamoja wa albam zao n.k (Ngwesa & Palla, 2016).

Ni enzi hizo pia Jay moe anasema nyimbo zilikuwa hazirekodiwi kwa kompyuta katika studio nyingi kama sasa. G solo katika kitabu chake kiitwacho harakati za Bongo Fleva anasema kwamba “Studio za kwanza ambazo zilikuwa ni analogy (analojia) zilimikiwa na watu binafsi waliokuwa ndugu na zilikuwa eneo la Magomeni Mikumi na zote zilikuwa katika nyumba moja. Wamiliki hao ambao ni Paul Muuto na mdogo wake Gerry Gumbo. Walikuja kuziuza studio hizo kwa taasisi za Don Bosco ndipo ikazaliwa Don Bosco Studio mwaka 1992. Mnamo mwaka 1994 studio ya mawingu ilianza kazi rasmi…. Mwaka 1998 MJ records ilianzishwa ikimilikiwa na Master J… studio moja tu ndiyo ilitumia mfumo wa digital (dijitali) ambayo ni sound crafters. Bei za kurekodi studio za analogy ilikuwa ni Shilingi 8,000 na kwenye studio zilizokuwa digital ilikuwa shilingi 25,000” (Mwanjoka, 2011).

Wakati Jay Moe anaingia katika ulingo wa muziki wa Tanzania, ni wakati ambao muziki wa Tanzania ulikuwa umetawaliwa na muziki wa Taarabu na Dansi/Bolingo na ndio ulikuwa ukipewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari kuliko muziki wa kizazi kipya. Wenye kumbukumbu nzuri mtakumbuka katika kipindi hicho kuelekea mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 ndipo kulikuwa na ushindani katika muziki wa Taarabu kati ya Khadija Kopa na Nasma Khamis Kidogo hali iliyepelekea kuanzia mtindo wa “mipasho” katika muziki wa taarabu kutokana na kutupiana vijembe katika nyimbo.

Ikumbukwe nyakati hizi ndizo nyimbo maarufu kama ‘Mambo iko huku”, “Sanamu la Michelin” za Nasma Kidogo, “Kinyago cha Mpapure” ya Mwanahawa Ally n.k zilikuwa zimeshika chati hali iliyofanya baadhi ya waimbaji taarabu kushirikishwa na wanamuziki wa kizazi kipya kwa mfano marehemu Nasma aliwahi kushikishwa katika kibao cha Gangwe Mobb kiitwacho wape Vidonge vyao. Abdul misambano pia alishawahi kushirikishwa kuimba kiitikio cha ‘asu’.

Katika muziki wa dansi, hiki kilikuwa kipindi ambacho bendi ya African Stars ama Twanga Pepeta ilikuwa katika ubora wake bila kuwasahau Tamtam, TOT, Wajelajela (ndanda Kosovo), Msondo Ngoma n.k walikuwepo pia katika chati. Twanga pepeta ilitawala muziki wa Tanzania kwa vipindi vikuu viwili kwa kipindi hicho; wakati safu ya uimbaji ikiongozwa na Banza stone aliyejiunga na Twanga mwaka 1995 na kutamba na nyimbo kama “kisa cha mpemba” n.k. Banza alipoondoka twanga mwaka 2001, Ally choki akashika usukani na kutamba na vibao kama ‘Jirani’, ‘chuki binafsi’ n.k. Upande mwingine Muumini mwinjuma alikuwa yuko moto na bendi ya Tamtam huku akipata umaarufu na kibao chake cha “Tunda”.

Kipindi hiki pia utaona waimbaji wa muziki wa dansi walianza kushirikishwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya. Wenye kumbukumbu mnaukumbuka wimbo wa “Achana nao” wa Mad Brain na Sister P wakimshirisha Ally Choki kuimba kiitikio cha wimbo huo. Tusiusahau pia wimbo wa “Msafiri” wa Kwanza Unit ambao walimshirikisha mzee wetu King Kikii (Mzee sugu au mzee wa kitambaa cheupe), “Hapo zamani” ya Sugu ft King Kiki na Kuna msanii (Nimemsahau jina) aliwahi kutumia kiitikio cha “Napenda Nipate lau nafasi” ya Kilwa Jazz Band. Huu wimbo wa msafiri humo ndani King Kikii hakushirikishwa tu bali Master Jay (mtayarishaji wa kibao hicho) alisampo kibao hicho pia. Kuna uwezekano hiki kikawa ndio kibao cha kwanza cha muziki wa dansi Tanzania kusampuliwa na watayarishaji wa muziki wa kizazi kipya.

Asha Baraka, mkurugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta anakubaliana na Jay Moe anaposema kwamba mziki wa kizazi ndio chanzo cha kufa (kuzorota) kwa taarabu na bolingo (dansi). Katika mahojiano na Gazeti la Mwananchi aliwahi kunukuliwa akisema ukuaji wa muziki wa kizazi kipya umeathiri soko la dansi. Anasema mwanzoni mwitikio ulikuwa mkubwa kuliko sasa hata mchango wa vyombo vya habari umepungua upande wa kupiga nyimbo za dansi hewani (Matandiko, 2014).

Itaendelea………..

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

 

 

 

 

Imeandikwa na
MALLE HANZI
0715076444
©2016