JAY MOE NA HILI GAME Sehemu ya I

Jay Moe_0
JAY MOE NA HILI GAME
Sehemu ya kwanza
______________________
Katikati mwa Miaka ya 2000 kituo cha Luninga cha EATV ama Channel 5 kilikuwa na kipindi kinachoitwa “In da House”. Kipindi hicho kilikuwa hakina mtangazaji maalumu ila kilikuwa na kawaida ya kumualika msanii ambaye hugeuka mtangazaji na pia kuchagua nyimbo anazozipenda.
Kuna kipindi alichaguliwa Kala Pina kuendesha kipindi hicho. Baada stori na kuchagua nyimbo mbili tatu ikafikia wakati akaamua kumwambia VJ kwamba ampigie wimbo wowote wa Immortal Technique. Kilichotokea ni kwamba yule VJ hakucheza wimbo wa Immortal bali aliucheza wimbo wa Jay Moe aliomshirikisha Mangwea uitwao “kimya kimya”.
Nilichojifunza ni kwamba kwenye hili game la Tanzania Jay Moe ni msanii pmaarufu kuliko Immortal Technique. Pia Madj wengi wa sasa ni “waweka kanda” kama Vital Maembe anawaita na sio wafuatiliaje wa muziki na ndio maana Vj akashindwa kutofautisha kati ya Immortal Technique na Jay Moe nadhani alidhani Kala Pina kasema Moe Technique ambayo pia ni “a.k.a” ya Jay Moe.
Enewei, Juma Mchopanga au maarufu kwa jina la Jay Moe ni mchanaji ambaye analijua hili game tangu hajaanza kulicheza. Inaaminika ameanza kulicheza mwaka 1998 ikiwa ni miaka ishirini tangu azaliwe mnamo tarehe 27/11/1978. Muziki huu ambao umeanza kushika kasi mwanzoni mwa miaka ya 90 kuna uwezekano mkubwa Jay Moe akiwa na miaka kumi na kitu akawa analifuatilia game kwa ukaribu kwahiyo yupo sawa anaposema analijua kabla hajaanza licheza.
Kuna taarifa zinaeleza kuwa, Mwaka 1999 alianzisha kundi lililoitwa Underground Kingdom na baadaye wakalibadilisha jina likaitwa Sewer Celibracy akiwa na Jaffarai na Mchizi Mox. Mwaka 2000, Jay moe na kundi lake walishiriki katika mashindano ya kutafuta vipaji yaliyoandaliwa na Clouds Fm huko ndiko walikokutana na Mack 2 B, Lady Lou na Solo Thang wakaunda kundi la Wateule baada ya kushinda na kupata nafasi ya kurekodi album chini ya Bongo Records.
Jay moe tangu ameanza gemu mwaka 98 mpaka leo yupo katika gemu huku kukiwa hakuna dalili zozote za kusanda. Naamini hili hata yeye alilijua mapema ndio maana akaamua kujibatiza jina la Mbakiaji. Mashabiki ni mashahidi wazuri kwamba wengi wasanii wamekuja wamemuacha na bado ngoma zake hazijachuja bado zinabamba japo zina miaka kibao.
Jay moe yupo kwenye hili game kabla Mamu hajaanza kugonga nakala za album. Mamu au kwa jina maarufu kama mdosi chini ya kampuni yake iitwayo GMC wasanii promoters Ltd iliyosajiliwa miaka tarehe 03/01/2001 (miaka mitatu baada ya Jay moe kuanza game) na kupewa 40577 ni moja kati ya kampuni za kwanza kwanza kuanza kusambaza kazi za wasanii wa Tanzania.
Album ya kwanza ya Jay Moe iitwayo “Ulimwengu ndiyo mama” iliyotoka mwaka 2002 ilisambazwa na GMC ikiwa na vibao kama “Ulimwengu ndiyo mama”, “Mi Mshamba”, “Maisha ya Boarding ft Dully sykes”, “Bishoo”, “Kama unataka demu”, “Misosi, mitungi na pamba ft Ay”, “Mpenzi kwaheri”, “Safari njema”, “Ulimwengu ndio mama rmx” na “Mvua na jua”.
“Mawazo ya Jay Moe” ni albamu yake ya pili iliyotoka mwaka 2005 na kusambazwa pia na wadosi pia (GMC) huku album yake ya tatu “Mocumentary” haikuwahi kutoka japo ilitangazwa tangu mwaka 2007. Jay moe aliwahi kusema kwamba ameshindwa kutoa album yake ya mocumentary kama alivyoahidi kutokana na kukosekana kwa mwamko kwa wasanii kutoa album badala yake wamekuwa wakitoa singo kwa sababu ya mabadiliko ya biashara ya muziki (Ayo, 2015)
Inawezekana pia album yake haikutoka kutokana na msambazaji ambaye alimsambazia album yake ya kwanza na ya pili kuachana na usambazaji wa nyimbo za muziki wa kizazi kipya. Ruge (2013) aliwahi kusema “Gmc.. sasa hivi ni mwaka wao wa pili na nusu hawajatoa hata album moja ya bongo flava wanafikiri kwa mamu pamefungwa lakini mamu anaendelea na wasanii wa Gospel na wanauza vile vile”.
Wakati Jay moe anatoa album ya kwanza “Ulimwengu ndio mama” mwaka 2002 chini ya GMC msanii mwenye album alikuwa anapokea Tsh 100 kwa kila tape ambayo ilikuwa ikiuzwa 1,200. Pia katika album ya pili “Mawazo ya Jay Moe” ya mwaka 2015 msanii mwenye album alikuwa akilipwa Tsh 200 kwa kila kanda iliyokuwa ikiuzwa Shilingi 1500 (Dudubaya, 2010)
Itaendelea…………

www.tizneez.com

Instagram tizneez

Facebook tizneez

Twtter tizneez
Imeandikwa na
Malle Hanzi
O715076444
©2016