“ISHI KWA ULICHOKISEMA” PROF JAY

IMG_3152

“ISHI KWA ULICHOKISEMA” PROF JAY

Prof Jay ambaye ni zao la kundi la Hard Blasters ambapo inaaminika ni moja ya makundi machache ya hiphop yaliyofanya kukubaliwa kwa kasi muziki huu wa bongo fleva.

Prof jay ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi katika Mkoa wa Morogoro, jina lake kamili ni Joseph Haule. Ambaye pia ni miongoni mwa wasanii wachache ambao wamefanya wengi waimbe muziki huu wa Bongo fleva/Hiphop.

Prof jay ameshinda kiti cha ubunge mwaka 2015 ambapo ameshinda kupitia tiketi ya CHADEMA chini ya mwamvuli wa UKAWA.

Ni msanii wa pili wa muziki wa hiphop kutoka nchini Tanzania kushinda kiti cha Ubunge, msanii wa kwanza alikuwa ni MR II Sugu ambaye alishinda mwaka 2010, kupitia CHADEMA, ambapo sasa humuita Mh Joseph Mbilinyi, ambapo pia katika harakati za muziki ni watu wa karibu na wote wana mchango unaopaswa kuheshimiwa kila iitwapo leo katika Muziki wa kizazi kipya. Licha Sugu kumtangulia katika ramani ya kufahamika kimuziki hata kutoa album, maana album ya kwanza ya Sugu ilitoka mwaka 1995 ambayo iliitwa NI MIMI.

Wakati wote inafahamika shughuli na majukumu ya mbunge ni makubwa, na si rahisi kufanya mambo mawili au matatu kwa wakati mmoja, ila ni watu wachache wenye uwezo wa kufanya utatu mara tatu.

Hakika ni furaha na heshima kwa kuona muziki wa hiphop/kizazi kipya unawapeleka watu kuwa viongozi wa majimbo, ile imani ya muziki uhuni imeshakosa nafasi tena, na sasa kila mzazi hatapinga kwa mtoto wake kushiriki katika muziki wa bongo fleva/hiphop kama ilivyokuwa mwanzo wa muziki.

Chemsha bongo ilianza kumjengea kuwa na mashabiki tangu mwaka 2000, ambapo baadae kulifuatiwa na album ya Funga Kazi, chini ya kundi lake la Hard Blasters ambapo pia kulikuwemo na wimbo kama Mamsapu.

Wengi walimfahamu kwa tungo zake na hata flow zake, lakini mwaka 2001 aliamua kutoa album yake binafsi iliyoitwa Machozi Jasho na Damu. Na hakika album hii ilivuma hata kumfanya kupata tuzo ya mtunzi bora wa hiphop. Uwingi wa mashabiki ulizidi kuongozeka kwake, wimbo kama Ndio mzee, Piga Makofi, na Bongo Dar es salaam zilizidi kumpa umaarufu hata sasa kupata mashabiki ambapo ni wazi hawakuweza kuficha hisia zao hasa pale alipokua katika matamasha mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Kiukweli Pro Jay hakuishia hapo zaidi ya kuonyesha uwezo wake katika album yake ya MAPINDUZI HALISI mwaka 2003, katika album hii kulikuwa na nyimbo kama Msinitenge, Zali la mentali na Promota Anabeep ambazo zilikuwa moto wa kuotea mbali. Hakika hapa mashabiki waliendelea kuongezeka, hii ilikuwa kila hatua anayopiga basi mashabiki walipiga nae.

JOSEPH ni album iliyofuata mwaka 2006, na baadae kufuatiwa na album ya Aluta Continua.

Prof jay amekuwa msanii tofauti na wasanii wengi katika tungo zake, na mpaka sasa ni moja kati ya kipenzi cha mashabiki walio wengi.

Nakumbuka mara ya mwisho kabla ya kuwa mbunge alifanya Tamasha pale Mbagara Zakhem ambapo ni wazi mashabiki walifurahishwa na show yake na hata wengine kutaka arudie baadhi ya nyimbo. Lakini kulingana na muda haikuweza kuwa hivyo.

Je Prof Jay hatawasahau mashabiki wake wa muziki? Atawapa haki yao kila baada ya muda aliokuwa anawapa? Historia inajionyesha kwa Mr II Sugu ambaye tangu atwae ubunge ametoa nyimbo mara 2 tu, ambayo ya kwanza ni Hakuna Matata na nyingine iliyotoka mwaka jana Freedom. Je Pro jay haitakuwa hivyo? Utaratibu utakuwa ule ule?

Lakini ni mara kadhaa nimemsikia katika mahojiano yake na vituo vya radio akisema kuwa muziki upo katika damu yake na daima hatoweza kuacha muziki maana ni chachu ya mafanikio aliyofikia sasa. Hivyo itakuwa vyema kama ataishi katika kile alichokisema. Kuishi kwenye kile ulichokisema ni jambo kubwa ambalo wengi wao limewapita mbali, kwani imekuwa ni kawaida katika maisha yetu ya kila siku kwenye nyanja tofauti ambapo wengi wamekuwa wakitoa kauli tofauti na kushindwa kuziishi ndani ya muda ambao hata mahindi ya mbegu za kisasa yanakuwa hayajapevuka.Ni vyema kuishi katika kile unachokuwa umekinena, maana kila uchao hiyo ndiyo hadhi ya mwenye kunena.Naamini ukubwa wako na maneno yako Prof Jay

Binafsi natamani awakumbuke mashabiki wake na awapatie haki yao kila baada ya muda ambao alikuwa anafanya, licha ya majukumu yake sasa kuwa makubwa tofauti na zamani.

Team tizneez inakutakia kila la kheri katika Kazi yako mpya, lakini pia huku kwenye muziki ni kazi yako unayopaswa kutupatia kila baada ya muda kama ilivyozoeleka.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez