Hakuna muziki usiokuwa biashara

hip-hop_mic_290x165

Hakuna muziki usiokuwa biashara

“Ukitaka kuchukiwa na mjinga mwambie ukweli akikosea”Ni wazi kwangu si jambo baya kumfanya mjinga apate kujitambua, hakika muziki wa kizazi kipya umeendelea kukua kila leo.

Muziki wa kizazi kipya una historia ndefu kuanzia mwaka 1989 mpaka sasa 2016. Dj Show ndicho kipindi cha kwanza ambacho kilipiga muziki wa kizazi kipya kwa mara ya kwanza mwaka 1994, wakati huo kipindi kikitangazwa na mtangazaji Taji Liundi ndani ya studio za Radio One

Ni ukweli usiopingika nyakati hizo miaka ya 1994 mpaka upate nafasi ya kusikika katika radio hakika ilikuwa uwe na uwezo wa hali ya juu. Si kama sasa ambapo wapo wasanii wengi ambao tunawasikia ambao ni wazi sifa wanazopewa ni kuzidi uwezo wa kipaji chake katika kufanya muziki huu wa kizazi kipya.

1993 ndipo palipo toka album ya muziki wa kizazi kipya (Hiphop) ambayo ilikuwa ni mali ya kwanza Unit. Album hiyo iliitwa Kwanza Unit. Ambapo pia inaaminika hii ndio album ya kwanza katika muziki wa kizazi kipya Tanzania.

Miaka ya 1995 hakika muziki ulishika hatamu na kuona mafanikio ya wasanii walio wengi. Maana hata msanii Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II Sugu alitoa album yake ya kwanza 1995 na kusambazwa na mzee John Kitime, album hiyo iliitwa “Ni Mimi”

Lakini ikumbukwe wakati huo muziki huu wa kizazi kipya ulikuwa na kundi kubwa la wasanii wa hiphop. Hakika waimbaji walikuwa katika asilimia chache zaidi, isipokuwa wengi wao walikuwa ni wasanii wa hiphop.

Miaka ikasogea mpaka miaka ya 2000 hapa tuliona muziki ukiwavuta wengi ambao hawakuwa hata na wazo na muziki. Wengi wao ni wale ambao walihisi muziki ni uhuni, lakini wakati huo tayari walishapata kuona mafanikio aliyopata msanii Mr II sugu. Ambaye mwaka 1998 alifanya onyesho nchini Sweden ambapo alikuwa jukwaa moja na Oliver Mutukuz.

Ukitaka utafakari yaliyofanywa nyakati za nyuma na wakongwe walio wengi katika muziki wa kizazi kipya hakika ni mengi hasa katika muziki wa hiphop.

Leo hii imekuwa ni kinyume na vile ambavyo ilikuwa. Watangazaji wengi wa vipindi vinavyohusu muziki wa kizazi kipya wamekuwa wakiaminisha wasikilizaji walio wegi kuwa eti muziki wa hiphop sio muziki wa biashara. Wamekuwa na kauli zao ambazo zinaonyesha walivyokuwa na ufahamu mdogo kuhusu wanachofanya. SI mara maja kumsikia mtangazaji akisema “Fanya komesho mzazi hiyo hiphop ngumu raia hawapendi” hakika hiii ni moja ya hoja za kipuuzi ambazo zinanifanya niache kusikiliza radio maana kwangu ni chukizo.

Hivi muziki wa komesho ni muziki wa aina gani? Duniani kote kuna muziki wa komesho?

Ni uwazi usiopingika duniani kote biashara yoyote inataka matangazo. Tumesahau mwaka 2012 ni wasanii kutoka Botswana maarufu kama “Makhikhiri”walikuja Tanzania na kufanya matumbuizo yaliyo mengi tena walifanikiwa kwa kiwango cha juu kuliko hata baadhi ya matumbuizo ya nyumbani yanayohusisha wasanii wetu.

Unaweza ukajiuliza walifanikiwa vipi? Lakini usisahau ilikuwa kila radio na runinga unayoweka lazima ukutane na wimbo wao. Na hata maeneo ya starehe ilikuwa lazima ukutane na wimbo wao. Ni wazi matangazo kuhusu nyimbo zao ilikuwa ni katika 100% hivyo walikuwa na kila sababu ya kujulikana na kila mtanzania kwa wakati ule.

Je leo hii kuna mtanzania anazungumzia kuhusu Makhirikhiri? Au kuna radio/Runinga inayopiga nyimbo zao? Je tunawasikia kama miaka 4 ya nyuma? Hivyo ni wazi hawana matangazo ndio maana hatuji kuhusu muziki wao tena.

Katika mfumo uliopo ni wazi inaonekana wasanii wa kuimba zaidi ndiyo wanafanya vyema. Ni wazi lazima ujue ukitazama vyema wasanii wengi wapo chini ya wadau fulani ambao ni wazi hao ndio wanaoendesha vituo vingi vya radio na runinga.

Hoja ya kusema kuna muziki usiokuwa biashara hakika ni hoja ya kipuuzi, na huwezi kuona kama ni hoja ya kipuuzi kama ufahamu wako wa kufikiri ni mdogo.

Ukitazama kwa ufahamu mpana tafakari juu ya muziki wa “Singeli” hakika ni aina ya muziki ulioibuka mwaka 2015 tu lakini katika mwaka 2016 ni wazi umekuwa ni gumzo Tanzania nzima. Lakini tazama jinsi muziki huu ulivyopewa nafasi hakika matangazo yake, yamekuwa makubwa ndio maana ukawa biashara leo hii. Hivyo unaposema kuwa muziki wa hiphop sio biashara wakati ni wazi hauna nafasi kubwa katika matangazo je utawezaje kuwa biashara?

Swala la mabadiliko ya wasanii walio wengi kutoka kwenye hiphop kufanya aina nyingine ya muziki imeendelea kushika kasi siku baada ya siku.Mabadiliko hayo yamegawa wasanii wa hiphop katika makundi mawili, moja ni lile linalosema waliobadilika ni “waki” na kundi jingine ni lile ambalo husema wao wanafuta misingi ya hiphop.

Lakini je mabadiliko hayo yanawasaidia kupata muda mzuri wa hewani kwenye hivyo vituo vya radio na runinga?.Maana ni ukweli usiofichika muziki wa kizazi kipya umegubigwa na mambo mengi, kiukweli umejaa na wakuda wenye ukanda, fitna na chuki. Ambapo wengi huwahubilia wasanii kufanya aina ya muziki wanayopenda wao isipokuwa mashabiki.

Lakini pia siachi kujiuliza kama kweli mashabiki hawapendi muziki wa hiphop mbona kwenye matumbuizo mengi wasanii wa hiphop ndio hufanya vyema zaidi?

“Machungu unapozimwa ili ufunikwe na asiyeweza, mbaya zaidi wanampa promo lakini kwenye show nammeza” Fidq Propaganda”

Hakika ni wazi kusema hiphop sio muziki wa biashara ni propaganda ambazo hazina msingi, ila vituo vya radio na runinga hutumia nguvu yao kubwa katika kudidimiza muziki huu ambao ni wazi ni muziki wenye nguvu katika jamii.

Ingawa katika nyakati hizi nategemea kuona wasanii wa hiphop wakitumia vyema mitandao ya kijamii kufikisha kazi zao kwa mashabiki wao. Nikki Mbishi ni mmoja kati ya wasanii ambao wanatumia vyema mtandao kufikisha kazi zake kwa mashabiki wake.

Ila ni vyema pia watu wa radio na runinga kutengeneza usawa katika kila upande, ukanda, fitna na chuki havijengi bali kuturudisha nyuma. Lakini pia dhambi ya ukanda hakika itatupeleka kwenye ukabila “Usipoziba ufa utajenga ukuta”

Tutengeneze usawa katika kila upande.

HIVI NDIVYO JINSI TEKNOLOJIA INAVYOPIGA TAFU MZIKI WETU

 

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez