Hakika tuwashangae wanaomshangaa Q Chief kwa Clouds Media Group.

Hakika tuwashangae  wanaomshangaa Q Chief kwa Clouds Media Group.

“Mwenye baridi husogelea moto” Semi hii na nyingine nyingi za mswahili zinafanya tujue namna ya kutafakari mengi kila leo, lakini hata ‘kujua jinsi’ na ‘kujua kuwa’.

Jambo baya ni kupingana na uhalisia, mswahili hunena yakuwa “Uhalisia haupingwi bali kukubaliwa”.

Hakuna ambacho amekosea Q Chief bali kwenda na hali halisi yenye uhalisia, na mwenye ufahamu atakuwa na shangazo la kuwashangaa wanaomshangaa Q Chief kwa Clouds.

Vinywa vya wengi vimekuwa vikinena mengi yenye fedheha juu ya msanii Q Chief, hasa eti!amekuwa mnyonge na ni wazi amejifadhaisha kwa kueleza mengi juu ya Bdozen na Clouds Media Group kwa ujumla.

Katika kweli yenye kweli Q Chief ameonyesha kukubaliana na uhalisi, lakini kujua hekima ya mswahili yakuwa “Kweli itakuweka huru”. Hakika yu huru sasa.

Katika hali ya upana jambo la kunena yeye yakuwa anaacha muziki ni kwa hali ya kukosa nguvu ya Media na wadau wake, maana Delilah ni wimbo wake aliotoa mwezi 2 mwaka huu 2018, lakini haukufanya vyema licha ya kuwa katika kiwango bora.

Hivyo hakuwa na lakufanya zaidi ya kuendeshwa na hisia zenye hasira. Lakini hapa alisahau yakuwa “Hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu” neno kuu lanena hivyo, hekima ni kuwaza na kufanya maamuzi nje ya hasira yenyewe.

“Baniani mbaya kiatu chake dawa” semi hii ni halisi na uhalisia wa Clouds Media Group. Katika ile kweli lugha kali na maneno yenye kufedhehesha kwa upande wao ni kila leo.

Lakini katika uhalisia nguvu ya Clouds ni kubwa mno katika kubadilisha ‘jiwe kuwa dhahabu’

Q Chief alikuwa na sababu zote za kuwataka Clouds katika kumnyanyua tena kimuziki, ni wazi katika kweli yenye kweli ni rahisi mno kwa Clouds tena kwa upana wa kipawa cha msanii Q Chief.

Ni vyema tukumbuke kumbukumbu kabla hatujanena yaliyo mabaya kwa upande wa Clouds, maana Saida Karoli alikuwa nje ya uwanja kabisa lakini Clouds walimrudisha na kuonekana ni bora ndani ya uwanja.

Ni “Media” ipi Tanzania yenye kuweza kufanya jambo la kumtoa msanii gizani na kumleta kwenye mwanga kama si Clouds?

Hivyo Q Chief yukatika mikono salama ya watu ambao wamebalikiwa uwezo wa kusafisha vilivyo vichafu na kuwa visafi katika hali ya upana, hivyo ambaye anamshangaa Q Chief inabidi tumshangae vyema.

Kaka yetu Q Chief ni vyema ujue “Mtego bila chambo haunasi” sasa chambo uko nacho maana wakianza Clouds wengine wote hufuata” (Uhalisia)

#TuzungumzeMuziki