“Godzilla lawama zianzie kwa watangazaji sio Bill Nas”

0366b6a794d7e343152bd2495bed4a0b

Godzilla lawama zianzie kwa watangazaji sio Bill Nas

“Yule atakaye kupandisha ndiye atakaye kushusha”Moja kati ya maneno aliyowahi kuimba lord Eyez katika wimbo wa hawatuwezi enzi ya Nako 2 Nako. Ambapo nyakati hizo Nako 2 Nako lilikuwa kundi bora la hiphop (2007-2009)

Ni ukweli usiopingika kuna nyakati msanii Godzilla alikuwa akifanya vyema katika ramani ya muziki wa kizazi kipya. Licha ya kufanya vyema lakini pia hata kusifiwa zaidi kuliko uwezo wake kimuziki katika radio ilikuwa ni jambo tulilolizoea zaidi. Kila alichokuwa anafanya ilikuwa ni kizuri hasa kwa baadhi ya watangazaji, ni wazi alipandishwa kwa kiwango cha juu.(2010-2012)

Muziki wa kizazi kipya ni muziki uliojaa rushwa, urafiki na umkoa kwa sasa. Lakini hakuna jambo jema kama kukumbuka yaliyopita, pia watu wengi husahau kama leo ndiyo inatengeneza kesho yako.

Bonta aliwahi kusema “Achana na Sala Sala promo unayopata kubwa zaidi ya Stoppa wa Ara” Hii ni katika wimbo wake wa Nauza kura yangu.

Nyakati hizo ndiyo nyakati ambazo mtangazaji mmoja alishindwa kuzuia hisia zake na kujikuta akimlinganisha Afande Sele na Godzilla tena katika muda wa hewani. Hakika baada ya hapo ilikuwa ni mwisho wa mimi kusikiliza kipindi hicho cha radio huku nikiamini ni wazi badala ya kujifunza ni wazi napoteza uelewa wangu kama sio muda.

Ni kweli unaweza kumlinganisha Afande Sele na Godzilla? Hivi unawalinganisha katika mlengo gani?

Lakini ni wazi sikuona hata kama msanii Godzilla alimkera zaidi ya kuipokea vyema yeye kulinganishwa na Afande Sele, ambaye ndiye mfalme wa rhymes Tanzania ambapo ameshikilia taji hilo tangu mwaka 2004 mpaka sasa 2016.

Sasa Godzilla anachukizwa na nini kulinganishwa na Bill Nas?. Wakati hao hao wanaomlinganisha sasa ndiyo waliwahi kulinganisha na Afande Sele. Ambapo ni ukweli uliowazi huwezi kumfanisha kabisa Afande Sele na Godzilla.(Chukizo)

Kuibuka kwa msanii chipukizi Bill Nas imekuwa mwiba kwa upande wa Godzilla. Hakika watangazaji wale wale waliokuwa wakimsifu Godzilla wamegeuka na kumsifu zaidi msanii chipukizi Bill Nas.

Huku wakiamini eti Bill Nas ni mkali kuliko Godzilla. Kimsingi ni jambo ambalo limeonekana kumpoteza Godzilla kwa nguvu zote.

Si kificho Godzilla ameonyesha hisia zake juu ya kuchukizwa na kitendo hicho, huku akiamini Bill Nas anamuiga. Jambo la ajabu ambalo ni wazi Godzilla ameonyesha kufadhaika kwake na kuanza kutumia mitandao ya kijamii katika kueleza yaliyo mengi ambayo yanamlenga Bill Nas.

Lawama zimekuwa zikimdondekea Bill Nas kutoka kwa Godzilla. Ila Bill Nas amesema “ Kwa ufupi mimi naamini sifanani na Godzilla kabisa kila nikisikiliza muziki wangu sioni kama kuna angle nafananae Godzila kama kuzungumzia marapa ninao wakubali nishamtaja sana Godzilla”

Kama Bill Nas hamuigi wala hatumii staili ya Godzilla ni kwanini baadhi ya watangazaji wamekuwa wakitumia nguvu nyingi katika kulinganisha?

Nadhani kuna haja ya msanii Godzilla kuamka kifikra, pengine hajui kama wengi huwajaza sifa wasanii chipukizi ili waweze kuwatumia vyema hasa katika matumbuizo mbalimbali bila gharama yoyote.

Hivyo kama lawama ni vyema zianze kwa watangazaji ili waweze kubadilika waweze kulinganisha wasanii ambao wametoka pamoja katika muziki.

Ila pia ukumbuke “Ivumayo haidumu”

 

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez