Diamond Platnumz ndani na nje kwa wakati mmoja.

Diamond Platnumz ndani na nje kwa wakati mmoja.

Na John Simwanza

Siku zote ukitaka kuijua siri ya mchezo lazima ukubali kujifunza na ndivyo ilivyo kwa msanii na mtumbuizaji wa kimataifa kutoka Tanzania Diamond Platnumz,  ambaye anaonekana kuyatumia vilivyo mafunzo yakucheza na huu muziki ndani na nje. Hamu na kiu ya kulitaka soko la kimataifa katika muziki wa Diamond bado ipo tena kwa kiasi kikubwa kwani bado hajafika pale alipo palenga na ndiyo maana juhudi zake zimekuwa zikionekana kila kukicha.

Kwakuwa penye nia pana njia jitihada za Diamond ziliweza kumfungulia milango kwa kufanya kazi na wasanii ambao tayari wapo katika soko la kimataifa. Lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kusahau wapi alipotoka hasa kwa kuwakosesha mashabiki wake muziki wenye mahadhi na vionjo vya nyumbani kwa sababu tu yakulitaka soko la nje ambalo ndio analiangalia zaidi kwa sasa.

Kucheza ndani na nje kumezidi kumpa heshima  kubwa Diamond Platnumz japo  ni ngumu mno kwa wasanii wetu walio wengi kuusoma huu mchezo wa kumudu masoko mawili kwa wakati mmoja na kwa bidhaa mbili tofauti,  ambazo zinaubora kulingana na soko husika kutoka katika kiwanda kimoja kama jinsi ambavyo anafanya Diamond Platnumz.

Diamond ana nyimbo nyingi mpaka sasa ambazo zinafanya vizuri kimataifa na ana nyimbo nyingi ambazo zinafanya vizuri nyumbani na mapokeo ya nyimbo zake yamekuwa ni makubwa kwa kila upande.

Katika hizi  nyimbo mbili ambazo amezitoa  katikati ya wiki hii ambapo moja amefanya na Tiwasavage msanii kutoka Nigeria na wimbo unaitwa Fire, nyingine amefanya  peke yake aliyoipa jina la I miss you  zimezidi kupita katika njia yake ileile ya Kulenga soko la ndani na nje.

Na hata ukiangalia  katika video utagundua  walengwa wa hizi bidhaa zilizo ingia katika masoko haya mawili ni Mashabiki wa pande mbili tofauti.

Mfumo huu wa kucheza na soko la ndani na nje  kuna kila sababu  ya wasanii kupata somo au kujifunza kupitia kwa Diamond hasa kwa wale wasanii wenye ndoto za kufanya muziki wa kimataifa na kuliteka soko ambalo tayari limepata ugeni wa msanii kutoka Tanzania.