Diamond Platnumz na maisha tofauti na wenyeji wake.

Diamond-Platnumz

Diamond Platnumz na maisha tofauti na wenyeji wake.

“Ni vyema kutumia muda wako kufanya mambo yako ya kimaendeleo na kutazama maisha yako zaidi” haya ni maneno ambayo mara nyingi Diamond Platnumz hutumia katika mahojiano anayokuwa anafanya katika vituo mbalimbali vya Radio na Runinga, ndani na nje ya nchi. Naseeb Abdul Juma ambaye wengi humfahamu kwa jina la Diamond Platnumz.

Kamwambie ni wimbo wake wa kwanza kumtambulisha katika ramani ya muziki wa Bongo Fleva,hii ilikuwa ni miaka ya 2008-2009. Miaka hii kulikuwapo na wimbi la wasanii wengi wapya ambapo walipata kutambulika katika ramani hii ya Bongo Fleva.

Watu wengi walikuwa watabiri baada ya wimbo wa “Kamwambie” kutoka na kufanya vizuri, wapo waliosema amebahatisha maana ilikuwa ni kawaida kwa miaka ile msanii kutoa wimbo mmoja na kupotea.

Kwa Diamond ikawa ni upekee katika Bongo Fleva maana aliendela kutoa nyimbo nzuri ambazo zilikonga nyonyo za wapenda muziki.Mbagara,Nitarejea, Moyo wangu, Mawazo,Nimpende nani,Nataka kulewa, Kesho, baada ya vibao hivi ndipo pale kila mmoja mpenda muziki wa Bongo Fleva kusema kijana uwezo wake ni mkubwa,na pia ndipo alipoanza kuwa na kundi kubwa la mashabiki ndani ya Tanzania.

Katika kauli yake Diamond Platnumz ““Ni vyema kutumia muda wako kufanya mambo yako ya kimaendeleo na kutazama maisha yako zaidi”ni wazi anaitendea haki kauli hii kila iitwapo leo.

Diamond na upekee wake katika Bongo Fleva alikuwa msanii wa kwanza kutaja gharama za kufanya onyesha lake, wapo wengi waliosema ni muongo kwa kutaja gharama alizokuwa anatoza kwa wakati huo maana zilikuwa ni kubwa.

Licha ya Diamond kutoa ufafanuzi juu ya gharama hizo kwamba hatozi tu imradi ila ni katika kuandaa mambo mengi ikiwemo mavazi yeye na madansa wake,maana hapendi kuonekana na muonekano mmoja katika majukwaa tofauti.

Uthubutu ni kitu ambacho kila binadamu anapaswa kuwa nacho, katika dunia hii hakuna kinachoshindikana kama ukiweka uthubutu.Diamond aliweka uthubutu na juhudi katika kazi yake ya muziki ambayo sasa imemfanya aishi kifalme.

Number one ni nyimbo iliyofungua milango ya kimataifa kwa upande wa Diamond Platnumz.Wimbo huu ulifuatiwa na video nzuri iliyokonga nyoyo za mashabiki kwa mara nyingine tena. Katika mwaka huo msanii Davido alikuja katika tamasha la Fiesta ndipo alipokutana na Diamond katika tamasha hilo. Baada ya hapo Diamond alipanda ndege kuelekea Nigeria kurekodi marudio ya wimbo huu wa Number one. Na katika upekee wake Diamond hakusita kutuonyesha kile kilichokuwa kinaendelea huko Nigeria baada ya kutuweke video katika mtandao ikionyesha wakali hao wakifanya kazi hiyo.Na baada ya hapo ilikuja video rasmi ya Number one remix

Ni kawaida kwa mgeni kuishi kama vile waishivyo wenyeji wake. Lakini hii haikuwa sawa kwa Diamond Platnumz yeye hakuishi kama walivyokuwa wakiishi wenyeji wake katika Bongo Fleva.Siku, wiki, mwezi, zinakwenda na Diamond ameendelea kushika usukani katika Bongo Fleva.

Wapo waliokuwa wakisema maneno mengi wakati Diamond Platnumz akitafuta nafasi hasa katika bara la Afrika. Hakiuwa jambo la ajabu kuona akiwa na wasanii wengi kutoka Nigeria, lakini maneno ya kejeli yalitawala katika mitandao ya kijamii kwamba ni mtu wa kujipendekeza zaidi.

Hii haikuwa ikinishangaza maana ni wazi alikuwa akiishi tofauti zaidi na wenyeji wake katika muziki wa kizazi kipya yani wasanii. Wasanii wengi wa kizazi si watu wa kutaka kujiweka mbele kwa msanii mwingine wa nchi nyingine, wasanii wetu hujiona wajuaji zaidi. Na hii huwa ni sababu ya anguko la wasanii walio wengi wenye vipaji vya hali ya juu.

Ni jambo lisilopingika kushirikiana na msanii wa nchi nyingine inarahisha zaidi muziki wako kufika katika nchi yake. Na kufahamu hili Diamond Platnumz amelifanya na leo hii tunaona akizidi kusonga mbele katika nchi ambazo ni ngumu muziki mwingine kupenya, ila kupitia ushirikiano wake na msanii wa nchi hiyo ni wazi imekuwa rahisi kwake.

Hii sio kama imekuja tu,sipokuwa nI kujipanga katika kila hatua yake anayopiga.Mpaka leo bado kuna wasanii walio wengi hawajui jinsi hata ya kutumia mitandaoni ya kijamii.Kutumia mitandao ya kijamii sio tu kupost picha ya kiatu kipya, au suruali mpya,au hata kupost msichana akiwa nusu uchi. Mitandao ya kijamii unaweza kutumia kutangaza kazi zako ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Diamond amekuwa akitumia mitandao yake ya kijamii hasa katika kutangaza kazi yake kimuziki,na mambo mengi kuhusu muziki wake.

“Waswahili husema toa hela upate hela” Hakika ni upekee katika Bongo Fleva, Kabla ya Diamond ni msanii gani aliwahi kuwa na mpiga picha?.Leo hii Diamond amekuwa na mpiga picha wake ambaye katika kila tukio lake basi ni wazi baada utaona limewekwa katika mitandao yake ya kijamii.Pia ameweza kuwa na label yake ya muziki inayoiwa Wasafi Classic Baby WCB ambayo mpaka sasa ina wasanii 4 ambao ni Rich Mavoko,Harmonize, Ray Vany na Qeen Dorin. Pia label hiyo tayari imeshaanza kufanya kazi ya kurekodi matangazo katika picha na sauti.

Hakika Diamond Platnumz amekuwa na upekee katika Bongo fleva, hili ni jambo jema la wasanii wajifunze kutoka kwake. Maana sasa hata makampuni makubwa yamekuwa yakimfanya kuwa balozi katika kampeni mbalimbali hii yote sio bahati isipokuwa ni kujenga mizizi yenye kuonekana katika utendaji wa kazi yake.

Kwa mwenendo wa kuishi tofauti na wenyeji wake katika muziki wa kizazi kipya nategemea kumuona mbali zaidi ya hapa alipo.

Amka kijana ishi tofauti na wenyeji wanavyoishi.

www.tizneez.com

Twitter tizneez

Facebook tizneez

Instagram tizneez

Youtube tizneez