Complex taa iliyozimika yenye mwanga kwenye muziki, Je! Wajua ameacha album mbili ambazo hazijatoka 2005 mpaka 2018?

Complex taa iliyozimika yenye mwanga kwenye muziki, Je! Wajua ameacha album mbili ambazo hazijatoka mpaka sasa?.

Kumbukumbu zinatukumbusha yakuwa 21.8.2005 uwanja wa muziki uliweza kumpoteza Complex akiwa pamoja na mwenza wake Vivian Tillya ambaye alikuwa ni mtangazaji wa Clouds Fm na msanii (muimbaji na rapa).

Ambapo ajali ya gari ndiyo chanzo cha wao kutoweka katika uso wa Dunia. Ajali hii ilitokea Mbwewe Mkoani Tanga pale ambapo wawili hawa walikuwa wakitokea Morogoro kuelekea Arusha.

Ikumbukwe walitokea Morogoro katika tamasha la Fiesta ambapo lilikuwa na semi kuu ya “Moto zaidi”.

Na safari yao ilikuwa na dhumuni la kwenda kwenye sherehesho la miaka 25 ya ndoa ya wazazi wake na Vivian (Mosi), lakini dhumuni pili ni Vivian kwenda kutambulisha Complex kama mwenza wake na waanze safari ya maisha ya ndoa.

Na twajua yakuwa “Chochote chenye asili ya kiumbe hakikosi deni la kifo” Naam! kwa nyakati kamili wametimiza vyema deni lao. (Uhalisi)

Lakini sisi ni nani kiasi tusieleza upana wa Complex katika muziki huu?. Ambapo hata wajuzi wananena yakuwa “Msipoeleza nyinyi Tizneez nani aeleze?. Hakika hakuna.

Mwanzo wa Complex katika muziki ulianza kama msanii wa hiphop, na wimbo wa ‘Moto umeshawaka’ inaaminika ndiyo wimbo wa kwanza kufanya chini ya mtayarishaji P Funk Majani ndani ya Bongo Records.

Na baada ya hapo Complex aliendelea vyema na muziki lakini pia alianza kujifunza kwa upana swala zima la utayarishaji muziki. Ila hatuwezi kusahau wimbo kama “Hakuna Hatari” chini Amit Mento ndani ya Poa Records. (1999-2000).

Poa Records ni endelezo kubwa la Complex katika upana wa ujuzi wa utayarishaji wa muziki ambapo Amit Mento ni mshiriki aliyeweza kumpa vyema darasa kwa upana mkubwa.

Hakika uwezo ulikuwa katika ukubwa, lakini hakuweza kusahau chanzo chake cha kurap katika wimbo wa ‘Tupa Mawe’ chini ya Mika Mwamba, ambapo Complex alikuwa na Zaharan.

Wimbo wa ‘Walidhani’ Complex na Zaharan tena ulithibitisha yakuwa Complex amekwiva vyema katika upana wa utayarishaji muziki na hii ni ndani ya Backyard Records.

Wajuzi wanaamini yakuwa Backyard Records ni studio ambazo Complex aliweza kufanya kazi nyingi zaidi. Wimbo kama ‘Mchanga wa macho’, Michano, na nyingine nyingi ziliweza kudhihilisha ubora wake na alama kwenye muziki huu.

Lakini ni nani mjuzi wa muziki asiyejua upana wa nyimbo kama Sema unachosema, Raha kamili Remix, Nimezama remix, Nyamaza, Safari njema, Taifa la Bongo, na Utatanishi, Hakika hayupo.

Album ya ‘Nyeti’ ya Wagosi wa Kaya ni alama kubwa zaidi katika kazi nyingi alizowahi kufanya Complex na hii ni ndani ya Aegies Records. (2004-2005).

Lakini jambo kubwa zaidi ni Complex ni uwepo wa album zake mbili ambazo hazikuweza kutoka mpaka leo hii. Ambapo sasa anatimiza miaka 13 tangu aondoke katika uso wa Dunia.

Na album hizi zipo chini ya studio za Backyard Records chini wa Samwel Mbwana almarufu kama Braton ambaye pia ni mtayarishaji lakini ni Katibu wa chama cha muziki wa kizazi kipya.

Je!wadau wana mpango gani na album hizi? Kwa wajuzi wa muziki hawana tatizo na upana wa Complex katika ubora wa uchanaji na ladha yenye usasa katika upana.

Ni wazi yapasa ifanye mipango imara na iweze kutoka vyema katika nyakati hizi, lakini changanyo la wasanii wa sasa likiwepo litaleta maana kubwa zaidi. Tukinena muziki umekuwa yapasa twende na usawia wa utoaji wa kazi za msanii husika ila endelezo la familia kufaidikia kwa kazi hizo liwepo.

Hakika ‘mtu atapita isipokuwa muziki’ Ni nani awezaye kulipa deni hili la album kwa mashabiki wa sasa?

#TuzungumzeMuziki