Baraka na Naj hawawezi kujiongoza, wanahitaji mtu/watu wa kuwaongoza.

Baraka na Naj hawawezi kujiongoza, wanahitaji mtu/watu wa kuwaongoza.

Nipe nguvu ni wimbo wetu pendwa toka kwa msanii Baraka Da Prince ambapo Imani yetu ni kubwa katika uwezo wake juu ya muziki huu wa kizazi kipya.

Ila mkwamo wake wa sasa ni kukosa uongozi katika usimamizi wa kazi zake, hivyo kujikuta yu pale pale kila leo tangu alipoachana na Rockstars4000. Katika uhalisi hapo anguko la muziki wake limeonekana kwa uwazi mkubwa, maana tangu aikache Rockstars4000 hajawahi kutoa wimbo na kuweza kufanya vyema.

Ambacho kilisikika vyema kutoka kwake ni kelele za hovyo juu ya kubaniwa, mara kupunguziwa watazamaji katika video zake ‘Youtube’ ilimradi tu hovyo na si muziki.

Lakini tukikumbuka kumbukumbu Baraka alipita katika mikono ya uongozi kama Kidway, Royal Nsyepa na mwisho Rockstars4000.

Ambapo nyakati yukatika uongozi wa hao watu hakika aliweza kufanya vyema Zaidi katika ramani ya muziki wa kizazi kipya.

Na nyakati hizi 2017-2018 yupo na ‘Bana Music’ akiwa na mpenzi wake Naj ameshindwa kuweza kufanya vyema katika muziki huu. Lakini nyakati zote “Kipofu hawezi kumuongoza kipofu mwenzake, hakika wote watadondekea shimoni”.

Ni jambo jema na zuri kwa yeye kuanzisha ‘Bana Music’ lakini ilipaswa kuwepo na mtu/watu wenye ujuzi wa namna ya usimamizi wa msanii na kazi zake za muziki ‘Uongozi’, Lakini kusimama wao kama wao hakika hilo ni anguko.

Katika nyakati hizi hakuna ambacho Baraka na Naj wanahitaji ili kupiga hatua kimuziki kama uwepo wa uongozi wenye ujuzi wa kuongoza msanii na biashara ya muziki, ni wazi Baraka na Naj hawatoshi na hawawezi kujiongoza katika muziki na biashara yake.

Lakini haitashangaza katika kupinga hili maana mswahili hakuacha nena yakuwa “Huwezi kuona msitu ukiwa msituni”

Na huenda kabisa ikawa Baraka na Naj ni wenye kushupaza shingo zao na kuona wao ni mashujaa hawana chembe ya uoga katika nyakati zijazo juu ya anguko la kimuziki, lakini wanapaswa kujua yakuwa “Kwa muoga huenda kicheko, ilihali kwa shujaa huenda kilio”.

#TuzungumzeMuziki

 

 

Attachment