Baraka Da Pince Ulimi uliponza kichwa

Baraka Da Pince Ulimi uliponza kichwa.

Hakika mswahili hakukosea kunena yakuwa “Jicho lililozima halistuki likiona bonde’, hakika semi hii ya mswahili inatufanya tutafakari mengi juu ya msanii Baraka Da Prince.

Mei 7, 2018 tuliandikia andiko ambalo lilieleza vyema juu ya Bana Music ambayo ni lebo yake yeye na msanii na Naj, ni kwa namna ipi waweze kufanikiwa vyema kimuziki.

Ambapo andiko hilo lilikuwa limeanza kwa kuandikwa “Baraka na Naj hawawezi kujiongoza, wanahitaji mtu/watu wa kuwaongoza”

Katika kweli yenye kweli ni andiko ambalo ndani yake limebeba mengi yenye maana juu yao. Shangazo kuu ni kwa namna ya msanii Baraka alivyoweza kutujibu kupitia mtandao wa picha ‘Instagram’ katika ukurasa wetu kwenye upande wa ujumbe binafsi.

Katika ujumbe wake msanii baraka aliamua kutumia lugha kali zenye ‘Matusi’ jambo ambalo limetushangaza mno.

Kwasababu siku zote Tizneez tunasisitiza maadili na matumizi bora yenye tija ya mitandao, katu hatuwezi kuweka bayana jumbe hizo.

Lakini tutakuwa ni watu wa hovyo kama tutakuwa ni wagumu kunena kweli sababu tu ya lugha kali zake. Na mswahili hunena yakuwa “Lifaalo kueleza lieleze, lisilofaa limeze” Hakika hili la Baraka lafaa.

Huenda Baraka akaona ni kama tumemkosoa katika andiko lile, lakini yafaa ajue na ajifunze kupokea yote kwa usawa yani kukosolewa na kusifiwa.

Lakini tunakumbuka vyema kaka yetu Afande Sele katika wimbo wa Mayowe akiwa na Jay Mo anasema “Hii ni fani na msanii sipo mwenyewe/ili nifanikiwe inahitaji nikosolewe/inapobidi nisifiwe” Na hii ndiyo maana ya ‘Liandikwalo halifutiki”

Hivyo ni vyema Baraka kuishi katika neno la Afande Sele, lakini kuchunga vyema kinywa chake, maana kinywa kinaweza kumfanya akose mengi mema kutoka kwa watu. Na sisi hatutaki kuamini semi ya mswahili yakuwa “Kinywa kinenacho mabaya, hakipo sawa”.

Sisi hatuwezi kuamini wala kukubali yakuwa Baraka hayuko sawa, bali tunaamini yakuwa hisia za hasira zimemuongoza vyema. Hivyo ni vyema aivue hasira katika kupokea mengi yenye maana katika muziki wake. Maana neno kuu pia lanena yakuwa “Hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu”

Lakini semi kuu ya mswahili yanena “Hasara humfika mwenye mabezo” lakini “Mjinga asipoelewa jambo hugadhibika,ila mwerevu hukuna kichwa” Tafakarii…

#TuzungumzMuziki