Afande Sele alijibeba mwenyewe na amejiangusha mwenyewe

Afande Sele alijibeba mwenyewe na amejiangusha mwenyewe.

Hakika “Juzi na jana si kama leo” mswahili na uhalisi wake wenye uhalisia wa Sanaa ya muziki ya Afande Sele. Maana juzi yake na jana si ya leo katika wimbo wa ‘Katubamba’.

Hatuwezi kusahau juzi yake ya ‘Mkuki Moyoni’ lakini jana ya ‘Darubini Kali’, sisi ni nani tusahau Heshima, Karata Dume, na Dini Tumeletewa?. (Hatuwezi)

Afande alijibeba mwenyewe katika upana wa mashairi na midondoko kwa maana juzi na jana ya muziki haikuweza kumbeba kwa upendeleo bali kweli yenye kweli juu ya tungo zake madhubuti.

Ufalme haukuja tu, bali uwezo wake kwa nafasi yake ya juzi na jana, lakini leo hii ‘Katubamba’ amerejea na kujiangusha mwenyewe hadharani.

Ikumbukwe hatupingi mahubiri yake aliyotoa katika ‘Katubamba’ bali tunapinga jinsi wimbo ulivyo katika upana wa wimbo.

Mahubiri yake ni katika tazamo lake na haipaswi kupinga tazamo la mtu katika kile ambacho yeye anakiamini. Lakini tunawakumbusha tu “Nafsi yenye njaa huona kila kitu kitamu”

Wimbo ‘Katubamba’ si wimbo wa hadhi yake kama Afande Sele, wimbo hauna ubora wa usikivu, muimbaji wa kiitikio ambaye ni Nassa Moro hata kutamka matamshi ya Rais hawezi anasema Laisi, hakika ni fedheha.

Lakini aina ya midondoko ya Afande ni ya kutoeleweka hakika haijaeleweka, na wapo ambao wanasema hakulenga soko la muziki bali wana siasa, je!mwanasiasa yupi asiyejua upana wa ubora wa muziki hata uimbaji? (Uchanaji).

Kwa hili Afande amepotoka vyema na hakika amejiengusha hadharani msuli upo magotini sasa, na nyakati zote “Mtu mzima akivuliwa nguo hadharani huchutama”

Tafakari kaka yetu Afande Sele, kwa ‘Katubamba’ umetia aibu si aina ya nyimbo zako katika ubora, ni kheri ungeendelea kukaa kimya. Maana kimya itafanya ubaki na heshima yako.
#TuzungumzeMuziki