Sababu moja Na Malle Hanzi

SABABU MOJA

na

Malle Hanzi
©2017
___________

Hivi umeshawahi kukumbwa na maradhi/
Ama kupokea kichapo kutoka vibaka, wezi au majambazi/
Kiasi kwamba ukashindwa hata kufanya kazi/
Ukaamua kuyahama kwa Muda yako makazi/
Ukarudi nyumbani ili ukauguzwe na wazazi/

Ukaharisha na kutapika ndani ya wiki/Ukatamani kula lakini chakula kooni hakipiti/
Ukaishia kushindia uji na juisi ya matikiti/Ukatamani Kufa ili Mola hakuepushe na kikombe hiki/

Ila

Ukasahau kwamba kuna mtu mwaka wa tatu kitandani anaugulia/
Maumivu zaidi ya yale unayoyapitia/
Hana msaada Jamaa na ndugu wamemtenga/
Anasota juu ya chaga na bado Mungu kumchukua hajapenda/

Inawezekana ukawa umepoteza ajira/
Kwa Miezi kadhaa kimaisha ukapoteza dira/
Ukawa huna chochote Cha kukuingizia ujira/
Ukalaumu kiasi Cha kumkufuru Mungu kwa Hasira/
Ukakosa fikira ukajiona taahira/

Kuna mtu Ana miaka mitano hebu fikiri/Hajawahi kupata Kazi wala kuitwa kwenye usaili/
Anasaga sorry ya kiatu kutafuta kazi/
Anaamini milango Ipo siku itakuwa wazi/

Umeshawahi kupigika na maisha haya/
Kiuchumi ukawa Katika hali flani mbaya/Ukafikia kutamani ungezaliwa mbwa ulaya/Ama uende uarabuni kufanya Kazi ya uyaya/

Ulishawahi kutazama filamu za magharibi/Ukadhani wote walioko ngambo maisha wanafaidi/
Kuna omba omba wengi tu ughaibuni/
Watu wasio na makazi na maskini wa hali duni/
Filamu ni mpangilio wa matukio ya kuigiza/Yanayotoa nuru na kutoa pia giza/

Umeshawahi kudharaulika/
Umeshawahi kunyanyasika kiasi kisichofikirika/
Ama wanapotajwa watu muhimu Mara zote unasahaulika/
Kila unachokiongea hakuna anayeshawishika/
Mazuri unayofanya yakashindwa kuthaminika/

Ukakata Tamaa na kujidharau/
Mithiri ya nyang’au ukajishusha kabisa dau/
Ukajiona huwezi malengo yako ukayasahau/
Ukaanza Kuishi Kwenye ndoto Za wengine/
Ukajitukana kwa kutokujiamini bila kujua pengine/

Pengine.

Kuwa mlemavu sio kutokujiweza/
Umesahau chongo humtamani Mwenye makengeza/
Kipofu anapotamani Angeumbwa chongo/
Ni Kama ambavyo wanaosota marekani wanavyotamani kurudi bongo/

Ulishawahi kukumbwa na madeni/
Kiasi kwamba ukawa unaomba usitembelewe na wageni/
Kwa sababu huna cha kuwapa zaidi ya Glass ya maji/
Ulishakula faida yote ukatafuna mpaka mtaji/
Kwa kufuja pesa na kukesha bar na washkaji/

Ukawa unakopa mkopo ili kulipa mkopo/Ukashindwa marejesho ukafilisiwa mali zako zilizopo/
Hukujua hata tajiri namba moja ana bonge la mkopo/

Amini wewe ni wa thamani/
Mungu hakuumba mtu bila sababu duniani/
Kujidharau ni kujigeuza kichekesho/
Hakikisha unapata sababu itakayokufanya uamini wewe ni spesho/

Kuna vikwazo vya kukatisha tamaa sana/
Kurudi nyuma ni laana songa front kaza buti pambana/
Kuna nyakati ukungu utakufanya usione mbele/usichoke kulisubiri jua mwishoni utakiona kilele/
Hata Kama Wengi uliowasikia unawaona wadwanzi/
Hakikisha unapata sababu moja ya kuniskiza Naitwa Malle Hanzi/

Aksante.

________